Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-31 18:16:05    
Cote d'ivoire yakaribisha mwanga wa amani

cri

Baada ya mazungumzo magumu na juhudi zisizolegea kwa pande mbalimbali zinazohusika katika miaka mitano iliyopita, wananchi wa Cote d'ivoire waliochoshwa na balaa la vita, sasa wanakaribisha mwanga wa amani waliokuwa wakiusubiri kwa muda mrefu. Sherehe ya kuanzisha mchakato wa kunyang'anya silaha ambayo ni ishara ya muungano mpya wa sehemu za kusini na kaskazini ilifanyika tarehe 30 Julai huko Bouake, kaskazini ya nchi hiyo.

Sherehe hiyo ilifanyika kwenye uwanja wa michezo wa Bouake, ambapo rais Laurent Gbagbo wa Cote d'ivoire na waziri mkuu Guillaume Soro walitupa bunduki mbili kwenye moto uliokuwa unawaka, ili kuonesha mchakato wa kunyang'anya silaha umeingia kwenye kipindi cha utekelezaji halisi. Rais Gbagbo aliwatangazia watu wapatao zaidi ya elfu kumi waliokusanyika kwenye uwanja wa michezo kuwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Cote d'ivoire vimekomeshwa rasmi. Marais wa Burkina Faso, Togo, Afrika ya kusini, Mali, Benin na viongozi na Wanadiplomasia wa nchi nyingine za Afrika walishiriki kwenye sherehe hiyo, na kushuhudia wakati wa amani ulivyowadia.

Sherehe ya kunyang'anya silaha si kama tu imeleta matumaini ya amani kwa wananchi wa Cote d'ivoire waliochoshwa na vurugu za vita, bali pia kumeonesha dhamira ya serikali ya Cote d'ivoire na makundi ya upinzani ya kujipatia amani. Kutokana na "Makubaliano ya amani ya Ouagadougou" yaliyosainiwa na pande hizo mbili, pande hizo mbili zimekubaliana kuvunja majeshi ya makundi ya upinzani na kundi la wanamgambo linaloitii serikali, na kujenga makao makuu ya pamoja ya uongozi wa jeshi; baadaye kiongozi wa kundi la upinzani Bwana Guillaume Soro akateuliwa rasmi kuwa waziri mkuu wa serikali ya Cote d'ivoire.

Waziri wa ulinzi wa Cote d'ivoire Bwana Michel Amani N'Guessan alijulisha kuwa, kuanzia siku ya kufanyika kwa sherehe hiyo hadi tarehe 30 Agosti, nchi hiyo itatumia muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi ya kunyang'anya silaha. Lakini hata hivyo hadi hivi sasa ingawa makundi ya upinzani yote yamekubali kuweka chini silaha, lakini watu bado wana wasiwasi fulani kutokana na matatizo yaliyotokea katika mchakato mzima wa amani ya Cote d'ivoire na utekelezaji wa makubaliano ya amani katika siku zilizopita.

Tokea vita vya wenyewe kwa wenyewe vitokee nchini humo mwezi Septemba mwaka 2002, ingawa pande mbalimbali zilizopambana zilisaini mara kwa mara makubaliano ya amani, zikijaribu kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kurudisha amani, lakini makubaliano hayo hayakuweza kutekelezwa kihalisi. Mwezi Januari mwaka 2003, chini ya uhimizaji wa Ufaransa, vyama vikubwa na makundi ya upinzani ya Cote d'ivoire vilisaini makubaliano ya amani kwenye kitongoji cha Paris, na kuanzisha mchakato wa amani. Lakini katika mchakato wa utekelezaji wa makubaliano, pande mbalimbali zilipambana bila kusita na kusababisha kutoweza kutekeleza mpango wa kunyang'anya silaha, na kukwamisha kufanyika kwa uchaguzi wa rais kama ilivyopangwa. Hali kadhalika "Mapatano ya Accra" yaliyosainiwa mwezi Julai mwaka 2004 na "Makubaliano ya amani ya Pretoria" yaliyosainiwa mwezi Julai mwaka 2005, yote hayakutekelezwa.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wengi wanafuatilia kwa makini matokeo ya mchakato wa kunyang'anya silaha. Hasa mwezi uliopita, ndege iliyokuwa imembeba waziri mkuu wa nchi hiyo Bw Guillame Soro ilipotua kwenye uwanja wa ndege ilishambuliwa kwa makombora, hii imeonesha kuwa bao kuna na wapinzani ambao hawaungi mkono kuafikiana na serikali.

Hivi sasa jukumu kubwa kabisa linaloikabili serikali ya Cote d'ivoire ni kufanya uchaguzi wa rais mapema iwezekanavyo. Mwanzoni mwa mwezi huu, rais Gbagbo alisema serikali ya Cote d'ivoire ina uwezo wa kufanya uchaguzi mkuu ulio wa kidemokrasia, haki na wazi kabla ya miezi mitatu ya kwanza mwakani. Wachambuzi wanaona kuwa, namna ya kufanya uchaguzi katika hali ya uhuru, haki na utaratibu, na watakaoshindwa kupokea matokeo ya uchaguzi au la, yote hayo yatakuwa ni mtihani kwa busara na ushujaa walio nao wanasiasa wa Cote d'ivoire.