Tarehe 31 Julai waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice huko Sharm El-sheikh nchini Misri alikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na nchi wanachama wa Kamati ya Ushirikiano ya Nchi za Ghuba, na kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo aliahidi kujishughulisha na amani na utulivu wa Mashariki ya Kati. Watu wanapounganisha ahadi zake pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na rais George Bush tarehe 16 Julai ya kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya Mashariki ya Kati, hawana budi kujiuliza, je ni kwa nini katika siku za karibuni Marekani imekuwa inahubiri sana amani ya Mashariki ya Kati?
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya mkutano tunaweza kugundua kwamba Marekani na nchi hizo za Kiarabu zimeafikiana kimsimamo kuhusu suala la Mashariki ya Kati.
Kwanza nchi hizo zote zinataka kusukuma mbele mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel. Kwenye taarifa hiyo pande zote zinasisitiza umuhimu wa kutimiza amani yenye haki katika sehemu ya Mashariki ya Kati na kukariri tena kuanzisha nchi ya Palestina huru inayoishi kwa amani na Israel katika msingi wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na "Mapendekezo ya Amani ya Nchi za Kiarabu". Nchi za Kiarabu zimefurahia mapendekezo ya rais George Bush ya kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya Mashariki ya Kati. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Bi. Condoleezza Rice na waziri wa mambo ya nje wa Misri Bw. Ahmed Abul Gheit, Bi. Condoleezza Rice alisema, atazihimiza Palestina na Israel zifanye mazungumzo kuhusu uhusiano wa pande mbili wakati atakapofanya ziara katika nchi hizo mbili. Bi. Condoleezza Rice alisema suala la Palestina na Israel ni lazima lizingatie "Pendekezo la Amani la Nchi za Kiarabu", mpango wa ramani ya amani ya Mashariki ya Kati na makubaliano yaliyokuwa yamesainiwa na pande mbili. Alisema kabla ya mkutano wa kimataifa, ni lazima ziwekwe kanuni husika ili kuhakikisha mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati unapata maendeleo, na pande zote ni lazima zitumie fursa hiyo kusukuma mchakato wa kisiasa katika sehemu ya Mashariki ya Kati.
Msimamo wa Marekani na ahadi za Condoleezza Rice zinaonesha kuwa Marekani inajitahidi kupiga hatua kubwa katika suala la amani kati ya Palestina na Israel. Vyombo vya habari vinaona kuwa sababu ya Marekani kufanya juhudi hizo inatokana na malalamiko yanayozidi kuongezeka siku hadi siku nchini Marekani kuhusu sera ya Marekani ya Mashariki ya Kati. Mwaka 2001 Rais George Bush alipoeleza kazi yake muhimu katika kipindi chake cha madarakani aliahidi kulifanya suala la amani la Mashariki ya Kati lipate maendeleo halisi ikiwa ni pamoja kusaidia kuanzisha nchi ya Palestina. Lakini mpaka sasa katika suala hilo rais huyo hajafanikiwa lolote, ahadi zote alizotoa mwaka huo zimekuwa hewa. Marekani inatambua kwamba mgogoro kati ya Palestina na Israel ni suala muhimu la kanda ya Mashariki ya Kati, na ni chanzo cha vurugu za kanda hiyo, bila suala hilo kutatuliwa maslahi katika kanda ya Marekani itaathirika vibaya.
Pili, kwenye taarifa hiyo Marekani imeonesha kuwa jeshi la Marekani nchini Iraq litaendelea kuwepo kwa miezi 17 yaani mpaka mwishoni mwa mwaka kesho. Nchi za Kiarabu zinataka sana Marekani iondoe jeshi lake mapema iwezekanavyo kutoka Iraq na kuharakisha mchakato wa maafikiano ya kisiasa nchini Iraq, wananchi wa Marekani wanazidi kupiga kelele wakitaka serikali yao iondoe jeshi nchini Iraq. Kwa hiyo kuweka ratiba ya kuondoa jeshi ni jambo linalolazimika kwa serikali ya Marekani. Kadhalika, katika sehemu ya Mashariki ya Kati kutimiza hali ya usalama na utulivu pia ni sharti la kimsingi kwa Marekani kuweza au kutoweza kuondoa jeshi lake. Hii ndio sababu ya kuwa Marekani inataka kupiga hatua kubwa katika suala la Palestina na Israel.
Wakati Marekani inapohubiri amani ya Mashariki ya Kati pia haikusahau kuonesha nguvu zake za kijeshi. Hivi karibuni, ofisa wa serikali ya Marekani alidokeza kuwa Marekani itazisaidia nchi sita kubwa zinazozalisha mafuta kwa wingi zilizoko kwenye Ghuba ya Uajemi kwa kuzipatia silaha zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 20. Sambamba na hayo itatoa misaada ya ushirikiano kwa Misri na Israel kwa muda wa miaka 10.
Idhaa ya kiswahili 2007-08-01
|