Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-01 19:19:02    
Teknolojia ya utabiri wa tetemeko la ardhi ya China

cri

Katika maafa mbalimbali ya kimaumbile, tetemeko la ardhi linachukua nafasi ya kwanza kwa kusababisha uharibifu mkubwa. Nchi nyingi zimeweka mkazo katika utafiti wa teknolojia ya utabiri wa tetemeko la ardhi, China ni moja ya nchi hizo. Imefahamika kuwa baada ya juhudi za miaka mingi, hivi sasa China inachukua nafasi ya mbele katika eneo la utabiri wa tetemeko la ardhi kote duniani.

China ni moja kati ya nchi zinazokumbwa na matetemeko ya ardhi duniani. Takwimu zilizotolewa na idara ya tetemeko la ardhi ya China zinaonesha kuwa, theluthi ya matetemeko ya ardhi yaliyotokea kwenye nchi kavu duniani yametokea nchini China, na mikoa ya China yote iliwahi kukumbwa na tetemeko la ardhi lenye ngazi zaidi ya tano kwenye kipimo cha Richter. Kwa hivyo, serikali ya China imeendelea kujitahidi kufanya utafiti wa teknolojia ya utabiri wa tetemeko la ardhi, kukusanya data za matetemeko ya ardhi na kujenga vituo vya kufuatilia matetemeko ya ardhi.

Mpaka sasa China imefanikiwa kutoa tahadhari zaidi ya mara 20 za tetemeko la ardhi zilizosaidia kihalisi kupunguza hasara kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa hayo. Kwa mfano, mwaka 1975 China ilifanikiwa kutoa utabiri wa tetemeko kubwa la ardhi lililotokea kwenye sehemu ya Haicheng mkoani Liaoning, na hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa binadamu kutoa taarifa ya utabiri wa tetemeko la ardhi iliyosaidia kihalisi kupunguza hasara zilizosababishwa na maafa. Mkuu wa idara ya tetemeko la ardhi ya China Bw. Chen Jianmin alisema:

"tulitoa utabiri sahihi kabla ya kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi na kusaidia kihalisi kupunguza hasara zake. Wataalamu wanaona kuwa, bila utabiri huo, tetemeko hilo la ardhi lingeweza kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki moja. Lakini tetemeko hilo lilisababisha vifo vya watu 1300, watu wengi walinusurika."

Lakini mafanikio hayo hayakupatikana kwa urahisi. Mwaka mmoja tu baada ya kufanikiwa kutabiri tetemeko la ardhi la Haicheng, tetemeko kubwa sana la ardhi lilitokea huko Tangshan na kusababisha vifo vya watu laki 2.4. Hasara kubwa namna hii zinahusiana moja kwa moja na kutokuwa na utabiri sahihi.

Bw. Chen Jianmin alisema janga hili limetoa onyo kwa watafiti wa tetemeko la ardhi wa China. Utabiri wa tetemeko la ardhi ni mgumu zaidi kuliko watu wanavyodhani. Bw. Chen Jianmin alisema, ugumu wake unatokana na kuwa tetemeko la ardhi hutokea kwenye sehemu zenye kina cha kilomita 15 chini ya ardhi. Katika zama za hivi sasa ambazo sayansi na teknolojia zimepata maendeleo makubwa, ingawa binadamu wanaweza kutazama nyota zilizo mbali kabisa ulimwenguni kwa kutumia darubini za kiunajimu, lakini hivi sasa kwa kutumia vifaa na teknolojia za kisasa kabisa, tunaweza kuchimba kina cha kilomita 12 tu chini ya ardhi. Kwa hivyo hatuwezi kuchunguza moja kwa moja chanzo cha tetemeko la ardhi.

Hata hivyo, watafiti wa tetemeko la ardhi wa China hawasiti kufanya juhudi kutokana na matatizo mbalimbali yanayowakabili. Baada ya ujenzi wa miundombinu na utafiti kwa miaka mingi, hivi sasa vituo zaidi ya 1200 vya usimamizi wa tetemeko la ardhi vimejengwa kote nchini China, na mtandao wa kisasa wa usimamizi wa tetemeko la ardhi unaofunika nchi nzima umekamilika kwa hatua ya mwanzo. Mtafiti wa taasisi ya utabiri katika idara ya tetemeko la ardhi ya China Bw. Zhang Guomin alisema, hivi sasa asilimia 10 hivi ya utabiri wa muda mfupi wa tetemeko la ardhi wa China unaweza kuwa wa sahihi, kiasi hicho kinachukua nafasi ya mbele kote duniani. Bw. Zhang Guomin alisema:

"kwa mfano tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 1996 huko Jiashi mkoani Xinjiang, tulitoa tahadhari kwa wakati na kuhamisha wakazi laki 1.5 kwa dharura."

Mbali na hayo, kwa kutumia data za matetemeko ya ardhi zilizopatikana katika muda mrefu uliopita, China imetoa ramani nne za China zinazoonesha sehemu zenye uwezekano wa kukumbwa na tetemeko la ardhi, kutoa ushauri kwa usanifu wa majengo ya makazi, na kutoa tathmini ya usalama kwa miradi mikubwa ya ujenzi zaidi ya elfu moja ukiwemo mradi wa magenge matatu, reli ya Qinghai-Tibet, majumba na viwanja vya michezo ya michezo ya Olimpiki.

Pamoja na maendeleo hayo yaliyopatikana, mkuu wa idara ya tetemeko la ardhi ya China Bw. Chen Jianmin alisema, China, na nchi nyingine duniani hivi sasa bado ziko kwenye mchakato wa mwanzo katika eneo la utabiri wa tetemeko la ardhi, usahihi wa utabiri huo bado uko kiwango cha chini sana.

Bw. Chen Jianmin pia alionesha wasiwasi wake kuhusu hali ambayo majengo mengi ya makazi vijijini hayana uwezo wa kuhimili tetemeko la ardhi. Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 60 ya hasara zilizosababishwa na tetemeko la ardhi hutokea zaidi kwenye sehemu za vijijini, hali hiyo inatokana na upungufu wa uelekezaji na usimamizi wa kiufundi katika shughuli za ujenzi vijijini.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imejitahidi kusukuma mbele mradi wa ujenzi wa makazi yanayohimili tetemeko la ardhi kwenye sehemu zenye uwekezano wa kukumbwa na tetemeko la ardhi nchini China. Kama vile kwenye sehemu ya Hetian mkoani Xinjiang, wakulima wengi wa huko wanaishi katika nyumba zilizojengwa kwa udongo, lakini hivi sasa wakulima laki kadhaa wamehamia kwenye makazi mapya yanayoweza kuhimili tetemeko la ardhi. Ofisa anayeshughulikia mradi huo kwenye sehemu hiyo Bi. Guli Sita alisema:

"mpaka sasa familia laki 5.96 za wakulima zimehamia kwenye nyumba zinazohimili tetemeko la ardhi."

Kwa mujibu wa mpango uliowekwa, ifikapo mwaka 2008, wakulima na wafugaji wote mkoani Xinjiang watahamia kwenye makazi kama hayo, na mradi huo pia utatekelezwa kwenye sehemu nyingi zaidi kote nchini China.

Mbali na kutilia maanani uwezo wa kuhimili tetemeko la ardhi kwa makazi ya vijijini, ili kutatua suala la utabiri wa tetemeko la ardhi, China itasawazisha na kuboresha mtandao wa hivi sasa wa vituo vya usimamizi wa tetemeko la ardhi, kukamilisha kumbukumbu za data kuhusu tetemeko la ardhi na kujenga vituo vya kisasa vya utafiti na majaribio ya teknolojia ya kuhimili tetemeko la ardhi na kupunguza hasara zake.

Ingawa kazi ya utabiri wa tetemeko la ardhi ni ngumu, lakini mkuu wa idara ya tetemeko la ardhi ya China Bw. Chen Jianmin ameonesha matumaini yake makubwa kwa shughuli hiyo. Alisema, hivi sasa idara hiyo ina watafiti zaidi ya elfu 7 wakiwemo wanachama 12 wa taasisi ya sayansi ya China, anaamini kuwa suala hilo ngumu hatimaye litatatuliwa hatua kwa hatua.