Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-02 15:08:56    
Ngoma za makabila madogo zawajumuisha vijana kutoka sehemu mbalimbali

cri

Katika Chuo Kikuu cha Makabila Madogo madogo cha China, kuna kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi. Japokuwa vijana hao wanatoka kwenye makabila mbalimbali na wanasomea kozi tofauti, lakini wamekusanyika pamoja kutokana na kupenda kucheza ngoma za makabila madogo madogo.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia sasa hivi ni muziki wa ngoma ya kabila la Wawa wenye umaalum wa kipekee uitwao "Sigangli". Wacheza ngoma ni wa kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makabila Madogo cha China. Asilimia zaidi ya 80 ya wanafunzi hao ni wa makabila madogo madogo nchini China. Mkuu wa kikundi hicho ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Bwana Tan Rui. Alisema:

"Kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi kilianzishwa miaka 11 iliyopita. Wacheza ngoma wote ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makabila Madogo cha China, ambao wanatoka makabila madogo zaidi ya 20, kama vile kabila la wauygur, wamongolia, watibet, wayi, wadai, wahani, na wahui."

Bw. Tan Rui ni mhani kutoka mkoa wa Yunnan, kusini magharibi mwa China. Alisema miaka 11 iliyopita, kikundi hicho kilipoanzishwa hakikuwa na ukumbi wa kufanyia mazoezi. Lakini hivi sasa kimekuwa na ukumbi wake maalum wa kufanyia mazoezi. Na ngoma zinazochezwa na kikundi hicho ni za kiwango cha juu zikilinganishwa na zile za vikundi vya ngoma vya vyuo vikuu vingine vya Beijing.

Kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi kiliwahi kujifunza ngoma na kufanya maonesho ya uchezaji wa ngoma kwenye mikoa ya Yunnan, Tibet, Hongkong na Macau. Mwezi Mei mwaka huu ili kusherehekea maadhimisho ya kutimia kwa miaka kumi tangu Hongkong irudi China, kikundi hicho kilialikwa kufanya maonesho kwa wiki moja katika vyuo vikuu na shule mbalimbali za Hongkong. Ngoma za makabila madogo ya China na ngoma za kisasa zilizochezwa na kikundi hicho zilipendwa sana na wanafunzi wa Hongkong. Mwanafunzi msichana m-hui kutoka mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang wa Guangxi Tan Shan alisema:

"Ngoma iitwayo 'machozi ya maua ya mipopi' tuliyocheza iliwahi kupata tuzo ya kwanza katika mashindano fulani, ngoma hiyo inaonesha madhara yanayosababishwa na dawa za kulevya kwa watumiaji wa dawa hizo."

Kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi ni hodari katika kucheza ngoma zinazoonesha hali ya makabila madogo madogo. Ngoma moja iitwayo "Taifa la China" imechezwa kwa miaka 11, ngoma hiyo inaonesha usanii wa ngoma za makabila madogo mbalimbali nchini China. Ngoma hiyo si kama tu ni ngoma inayokitambulisha kikundi cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi, bali pia ni alama ya kuwaunganisha vijana wa makabila madogo madogo wa Chuo Kikuu cha Makabila Madogo cha China. Mwanafunzi wa kabila la wa-hani aliyecheza ngoma hiyo kwa miaka mitatu Bw. Huang Ming alisema:

" 'Taifa la China' ni ngoma yenye mchanganyiko wa ngoma za makabila yote madogo madogo nchini China, ngoma hiyo ilipewa tuzo ya nafasi ya kwanza katika tamasha la kwanza la maonesho ya michezo ya sanaa la wanafunzi wa vyuo vikuu."

Bw. Huang Ming alifahamisha kuwa, wanachama wengi wa kikundi hicho ni wanafunzi wa makabila madogo madogo kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Watu wa makabila madogo madogo nchini China ni hodari sana katika kucheza ngoma na kuimba nyimbo, ngoma na nyimbo ni sehemu muhimu ya maisha yao.

Ingawa Bw. Huang Ming anaishi mjini, lakini alipokuwa mtoto alijiandikisha katika kasri la watoto kujifunza ngoma za makabila madogo ya wadai na wahani. Bi. Tan Shan wa kabila la wahui kutoka mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang wa Guangxi alisema, mazingira ya maskani yake ya kupenda kucheza ngoma na kuimba nyimbo yamemwezesha kupenda sana utamaduni wa makabila madogo. Alisema:

"Kila inapofika sikukuu ya 'tarehe 3 Machi', wavulana kwa wasichana wa makabila ya wazhuang, wamiao na watong waishio katika vijiji vya milimani huimbiana nyimbo na kucheza ngoma. Naona utamaduni wa makabila madogo madogo una maana nyingi, na kucheza ngoma ni njia nzuri kuonesha vizuri hisia za watu."

Wacheza ngoma wanafunzi hao walisema kuwa, kila wanaporudi kwenye maskani yao wakati wa likizo, huwa wanafuatilia sana ngoma zenye hali ya kiasili za makabila madogo madogo, kama vile mienendo na umaalum wa kuchezea ngoma, na mavazi na mapambo wanayovaa wacheza ngoma, huwa wanayanunua na kurudi nayo chuoni ili kuzifanya ngoma zao za makabila madogo zipendeze.

Wanafunzi wengi wa kikundi hicho cha ngoma za makabila madogo cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makabila madogo cha China, si wanafunzi wa kozi ya uchezaji wa ngoma, hivyo wanapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi. Aliyejiunga na kikundi cha ngoma za makabila madogo kutoka kabila la watibet Bwana Sanjidong alisema:

"Nimesoma katika Chuo Kikuu cha Makabila Madogo cha China kwa miaka 7, katika kipindi hicho sifa na fursa zote nilizopewa, na uwezo wangu wote ulihusiana na kikundi cha ngoma za makabila madogo, na kutokana na wenzangu wote niliowafahamu nilipokuwa katika kikundi hicho. Siwezi kusahau kabisa maisha yangu nilipokuwa katika kikundi hicho."

Idhaa ya kiswahili 2007-08-02