Katika maonesho ya biashara ya kimataifa yaliyofanyika mwezi Oktoba mwaka jana huko Nairobi, nchini Kenya, watu wengi wakiwemo wafanyabiashara wa huko walijazana kwenye banda la bidhaa la China, na wengi wao walipotoka walibeba mifuko mikubwa na midogo iliyojaa bidhaa kutoka China. Sasa zaidi ya nusu mwaka umepita, ili kufahamu hali ya kupendwa kwa bidhaa zilizotengenezwa nchini China, mwandishi wetu wa habari alifanya mahojiano na mfanyabiashara mmoja wa huko anayeuza bidhaa kwa jumla Bw. Dinesh.
"Kuna watu waliosema kuwa nyundo za aina hii zilizotengenezwa nchini China zinaweza kutumiwa kwa siku 3 tu, hebu wewe angalia nyundo hiyo tunayoitumia nyumbani, sasa karibu imetimiza miaka miwili, si bado ni imara kama hapo mwanzoni?"
Bw. Dinesh alionesha mpini wa nyundo aliyoishika mkononi, ambao umechafuka sana na kubadilika kuwa wa rangi nyeusi kutokana na kutumika kwa siku nyingi, huku alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa bidhaa zote zilizowekwa kwenye rafu zilizokuwa nyuma yake, zilitengenezwa na China.
Bw. Dinesh ni mfanyabiashara wa huko, ambaye amefanya biashara ya uuzaji kwa jumla wa vifaa vya ujenzi na vitu vinavyotumika katika maisha ya watu tangu miaka 21 iliyopita, duka la Bw. Dinesh ni duka la vifaa vya ujenzi linalochukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa nchini Kenya. Asilimia 80 hivi ya bidhaa anazouza zinatoka China, bidhaa hizo zinauzwa haraka kutokana na kuwa bei nafuu. Aliichukulia nyundo kama mfano. Bw. Dinesh alisema, bei ya nyundo hiyo ya China aliponunua ni Shilingi 88 za Kenya (dola I ya kimarekani ni sawa na Shilingi 65 za Kenya), kutokana na ushindani mkali, hivi sasa bei ya nyundo ya aina hiyo ni Shilingi 90, na faida yake ni Shilingi 2; Lakini nyundo za aina nyingine zilizotengenezwa nchini Uingereza, bei yake wakati aliponunua ni Shilingi 700, hivi sasa zinauzwa kwa Shilingi 850 kila moja, na faida ya kila nyundo ni Shilingi 150. Hivi sasa nusu ya idadi ya watu wa Kenya wanaishi chini ya kiwango cha umaskini, na uwezo wao wa kununua bidhaa bado ni mdogo. Mshahara wa kila mwezi wa mfanyakazi wa kawaida nchini Kenya ni kiasi cha Shilingi 6,000, fedha zilizobaki baada ya kukatwa huduma za jamii, zinatumika kwa watu wa familia moja (kwa kawaida ni yenye watu wanne), hivyo pato la familia ni dogo sana likilinganishwa na mahitaji. Katika hali hiyo, bidhaa za China zenye bei nafuu zimekuwa bidhaa zinazopendwa zaidi na watu wa kawaida.
Bidhaa bora za China zenye bei nafuu ni kitu muhimu cha kuvutia wateja wa Kenya, faida kubwa inatokana na kuuza bidhaa kwa bei nafuu na kwa wingi ni kitu muhimu kwa bidhaa za China kuwavutia wafanyabiashara wa Kenya. Hivyo bidhaa za kutoka China zimechukua nafasi kubwa kwenye soko la Kenya.
Nchini Kenya, bidhaa nyingi zinazouzwa kwa jumla na wafanyabiashara wa Kenya zinatoka China, ambazo kutoka misumari hadi vyombo na mitambo mikubwa ya kilimo, kutoka viatu na kofia hadi vipuri vya magari na vyombo vya umeme vinavyotumika nyumbani, zimeonekana katika maduka na supamaketi za Kenya.
Ofisa wa idara ya ubora wa bidhaa nchini Kenya alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kutokana na maagizo husika ya Kenya, bidhaa zote za nchi za nje haziruhusiwi kuingia nchini Kenya kabla ya kupita katika upimaji na ukaguzi wa idara ya ubora ya Kenya, wakati baadhi ya vyombo vya umeme vinavyotumika nyumbani vinavyosafirishwa kwenda Kenya vinapaswa kupitia ukaguzi katika nchi zinazozalisha kabla ya kupakiwa kwenye meli. Ukaguzi huo ni mkali, na mbinu zinazotumika pia ni za kisasa.
Bw. Dinesh alisisitiza "Sisi wafanyabiashara tunafuata kabisa sheria ya nchi, bidhaa tunazouza zote zinapitia ukaguzi wa idara ya ubora ya Kenya, na zote zinalingana na kiwango kilichowekwa."
Bw. Dinesh alionesha nyundo aliyoishika mkononi huku akiongeza kuwa, huku hali ya ubora wa bidhaa ikiwa ni ya kulingana, bei za bidhaa za China ni theluthi moja, robo, na hata sehemu moja kwa kumi ya bidhaa za aina hiyo za kutoka nchi za Ulaya na Marekani, hivyo bila shaka bidhaa zinazopendwa zaidi ni zile za kutoka China.
|