Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 2 Agosti alimaliza ziara yake fupi kwenye sehemu ya Palestina na Israel. Vyombo vya habari vimesema katika zaidi ya miaka miwili iliyopita tangu Rice ashike wadhifa wa waziri wa mambo ya nje, amefanya ziara mara kwa mara kwenye sehemu ya Palestina na Israel. Katika ziara zilizopita, Rice alisisitiza mara kwa mara kuwa alikwenda kusikiliza na kuelewa misimamo ya Palestina na Israel, lakini safari hii mara kwa mara alizitaka pande hizo mbili zianzishe mazungumzo halisi, akifanya maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati utakaoitishwa chini ya pendekezo la rais George Bush wa Marekani.
Kutokana na hali ya hivi sasa, mafanikio makubwa aliyopata Rice ni kuziwezesha pande mbili Palestina na Israel zifikie makubaliano kuhusu namna ya kuanzisha mazungumzo ya amani. Zamani mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw Mahmoud Abbas siku zote alitaka kufanya mazungumzo na Israel kuhusu masuala ya mipaka, hadhi ya Jerusalem na haki ya kurudi nyumbani kwa wakimbizi wa Palestina, na alikataliwa na Israel. Lakini safari hii chini ya usuluhishi wa Bi. Rice, waziri mkuu wa Israel Bwana Ehud Olmert amekubali kufanya mazungumzo na Palestina kuhusu "masuala kadhaa ya kimsingi", na Bwana Abbas amekubali pendekezo alilotoa Bw Olmert kuhusu pande hizo mbili kujadili kwanza "Taarifa ya kikanuni" kabla ya kujadili vilivyo hadhi ya mwisho, na kufikia makubaliano ya jumla kuhusu kuanzishwa kwa nchi ya Palestina.
Hali hii hakika imetandika njia kwa ajili ya kufanya mazungumzo mengi zaidi kabla ya kuitishwa kwa Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati. Rais George Bush wa Marekani alitoa mwito wa kuitisha Mkutano huo mwezi uliopita, ili kuhimiza mchakato wa amani ya Palestina na Israel. Mkutano huo unatazamiwa kuitishwa mwezi Novemba mwaka huu. Bi. Rice tarehe 2 huko Ramallah alisema, mwito wa Rais George Bush wa kuitisha Mkutano huo ni kwa ajili ya kupata matokeo halisi ili kuhimiza kuanzishwa kwa nchi ya Palestina. Palestina na Israel zimekubali kufanya mazungumzo kabla ya kuitishwa kwa Mkutano huo, na kujitahidi kufikia "Makubaliano ya kikanuni", na kuthibitisha mambo ya jumla ya kuanzishwa kwa nchi ya Palestina, hii hakika itaweka msingi kwa mafanikio ya Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati.
Ili kuhimiza Palestina na Israel zifanye mazungumzo, Bi. Rice amefanya kazi nyingi katika ziara yake. Nchini Israel alizihimiza pande hizo mbili zitumie fursa kutimiza amani ya mashariki ya kati. Nchini Palestina, alifanya mazungumzo na mawaziri wote wa serikali mpya ya Palestina, ili kuonesha uungaji mkono kwa serikali mpya ya Palestina ambayo imeboresha uhusiano na Israel hivi karibuni. Tena Bi. Rice alikubali kutoa dola za kimarekani milioni 8 kwa serikali mpya ya Palestina ili kuisaidia kufanya mageuzi ya kikosi cha usalama.
Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, kama Bi. Rice atafaniikiwa kuzihimiza Palestina na Israel zifikie makubaliano ya kikanuni kuhusu suala la kuanzishwa kwa nchi ya Palestina, hakika hii itakuwa ni hatua kubwa kwa mchakato wa amani ya Palestina na Israel ambao ulikwama kwa siku nyingi. Lakini wachambuzi wamesema pia kuwa, vitendo alivyofanya Bi.Rice haviwezi kuonesha umuhimu mkubwa katika kukomesha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya nusu karne kati ya Palestina na Israel. Ingawa Palestina na Israel zimekubaliana kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kikanuni, lakini masuala makubwa kuhusu hadhi ya Jerusalem na haki ya kurudi nyumbani kwa wakimbizi wa Palestina bado hayataweza kutatuliwa, ambayo yatawekwa kando tu kwa muda, na migongano kati ya pande hizo mbili kuhusu masuala hayo huenda itazifanya juhudi zote ziwe bure. Aidha, Marekani na Israel kuendelea kulifanya kundi la Hamas linalolidhibiti kanda la Gaza liwe kwenye hali ya upweke, hii pia haisaidii kujenga nchi ya Palestina. Waziri mkuu wa Israel Bw Ehud Olmert alisema wazi kwamba ni lazima kulitenga kundi la Hamas, na kundi la Hamas linamlaani Rice kuzidisha mfarakano ndani ya Palestina badala ya kusaidia kujenga nchi ya Palestina. Lakini kama hakuna ushirikiano wa kundi la Hamas, ni vigumu kuanzishwa kwa nchi ya Palestina, na pia ni vigumu kutimiza amani kwenye sehemu ya Palestina na Israel.
|