Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-06 16:11:25    
Utamaduni wa kiasili wa Tibet wahifadhiwa vizuri

cri

Tibet ni mkoa uliopo kusini magharibi mwa China, mkoa huo sio tu unavutia kwa kuwa na milima yenye theluji na maziwa yenye maji maangavu bali pia unavutia kwa utamaduni wake, kasri la Potala, hekalu kubwa la Jokhang na opera ya Kitibet yenye historia ya miaka mingi.

Mliosikia ni wimbo waliokuwa wanaimba wafanyakazi wakati wanapofanya ukarabati wa kasri la Potala. Katika lugha ya Kitibet, neno "aga" maana yake ni udongo wa mfinyanzi. Wafanyakazi wanatandaza udongo huo juu ya paa au sakafuni na kupigapiga kwa mawe au mbao mpaka uwe mgumu na laini kama marumaru. Mpaka sasa wanaendelea kutumia ufundi huo katika ukarabati wa kasri la Potala.

Kasri la Potala lilijengwa katika karne ya saba kwa ajili ya mfalme wa Tibet Songtsen Gampo kumwoa binti wa mfalme wa Enzi ya Tang Wen Cheng, baadaye likawa makazi ya kiongozi wa dini ya Buddha ya Kitibet. Tokea miaka elfu kadhaa iliyopita kasri hilo ni mahali patakatifu kwa waumini wa dini ya Buddha na pia ni alama muhimu ya utamaduni wa Tibet kutokana na kuwepo kwa miaka mingi.

Mkurugenzi wa ofisi ya utunzaji wa kasri la Potala Bw. Jampa Kelsang ni mtaalamu mashuhuri wa hifadhi ya mabaki ya kale, ameshughulika na hifadhi ya kasri hilo kwa miaka zaidi ya 20. Alisema, katika kasri hilo kila chumba kina hadithi yake, na kila picha iliyochorwa ukutani inaeleza tukio moja katika historia, kwa hiyo kazi ya kutunza mabaki hayo ni jukumu kubwa la serikali. Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita hadi sasa serikali imetenga fedha Yuan zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa kasri hilo. Ukarabati mkubwa wa pili ulioanzia mwezi Juni mwaka 2002 ulifanyika zaidi katika kuimarisha msingi wa jengo hilo kubwa na kuhifadhi mapaa yake. Alisema,

"Ukarabati mkubwa wa pili unafanyika zaidi katika kuimarisha msingi wa jengo la Potala na mapaa yake. Kwa sababu bila msingi imara jengo hili kubwa haliwezi kuwa salama, kazi nyingine muhimu ni kutunza mapaa yake, kwa sababu mvua ikivuja na picha zilizochorwa ukutani zikilowa zitaharibika, kwa hiyo kazi ya kuimarisha paa ni ya lazima."

Ili kuzuia uharibifu kwenye jengo hilo kutokana na kutembelewa na watalii wengi, kuanzia tarehe mosi Mei mwaka 2003 watalii wanazuiliwa kwa idadi chini ya 2300 kwa siku, watalii wakiwa na kikundi chao hawaruhusiwi kukaa ndani ya kasri hilo zaidi ya muda wa saa moja, na lazima wawasilishe ombi lao na kupata kibali kabla ya kutembelea. Bw. Jampa Kelsang alisema, serikali imechukua hatua nyingi za kutunza kasri la Potala.

Licha ya mabaki ya kale, utenzi na opera ya Kitibet pia vinatunzwa vizuri. Kazi ya kukusanya na kuhariri "Utenzi kuhusu Mfalme Gesar" ilimalizika mwaka jana. Gesar alikuwa shujaa wa kabila la Watibet, alikuwa mtu jasiri, mwenye maadili na mwenye kutetea haki. Utenzi huo umesimuliwa kwa zaidi ya miaka elfu moja, ni utenzi mrefu kabisa duniani. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita serikali ya China iliunda kikundi cha wataalamu na kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kukusanya na kuhariri utenzi huo, na vyuo vikuu vingi vimeanzisha idara ya utafiti wa utenzi huo.

Mtaalamu Tsering Phuntsog wa taasisi ya utafiti wa sayansi ya jamii mkoani Tibet alisema, hivi sasa taasisi yake imeanzisha mradi wa kurekodi utenzi huo unaoimbwa na mzee mmoja mwenye umri wa miaka 85. Mzee huyo alianza kuimba utenzi huo toka alipokuwa na umri wa miaka 11. Bw. Tsering Phuntsog alisema,

"Hadi leo 'utenzi kuhusu mfalme Gesar' umechapishwa kwa namna nyingi tofauti, lakini hakuna hata aina moja inayoeleza hadithi kamili na kuweza kuimbwa. Kwa hiyo tumedhamiria kumchagua msanii mmoja mzee kueleza hadithi kamili kwa kuimba na kurekodi."

Katika sikukuu ya Shoton ya kila mwezi Agosti, serikali ya Tibet inawashirikisha wasanii wengi kufanya maonesho ili kuenzi utamaduni wa jadi wa Kitibet. Miongoni mwa wasanii wanaoimba na kuuelezea "Utenzi kuhusu Mfalme Gesar" kuna wazee na vijana.

"Opera ya Kitibet ni mkusanyiko wa aina nyingi za sanaa, inachezwa kwa kuimba, kuongea na kucheza dansi. Opera ya Kitibet katika sehemu ya Juemulong karibu na Lhasa, mji mkuu wa mkoa wa Tibet, imekuwa na historia ya miaka 300. Mwaka jana opera hiyo imeorodheshwa katika urithi wa utamaduni wa China. Kutokana na uchumi unavyokua kwa kasi opera ya Kitibet inastawi na kuvutia zaidi.

Chung Da ni mchezaji wa opera ya Kitibet, mwaka 2001 alianzisha kundi la wasanii wa opera ya Kitibet. Alieleza,

"Katika kundi letu, mchezaji mkubwa ana umri wa miaka zaidi ya 80, na mdogo ana umri wa miaka 14. Tunacheza katika majira ya joto, katika majira ya baridi sote tunarudi nyumbani kwetu. Katika kipindi chenye watalii wengi, tunakwenda mjini Lhasa kucheza opera yetu, mapato ni mazuri."

Katika kundi hilo la wasanii kuna wakulima zaidi ya 20. Baada ya reli ya Qinghai-Tibet kujengwa, tulisaini makubaliano na kampuni moja ya utamaduni kucheza opera ya Kitibet kwa ajili ya watalii, mapato ya wakulima hao sasa yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Naibu mkuu wa serikali ya mkoa wa Tibet Bw. Deng Xiaogang alisema, katika miaka mingi iliyopita, serikali kuu, serikali ya mkoa na serikali za mitaa mkoani Tibet zimefanya juhudi kubwa kutunza na kustawisha utamaduni wa Kitibet kwa hali na mali. Alisema,

"Kazi yetu ni kutunza na kustawisha utamaduni wa Kitibet. Baada ya reli ya Qinghai-Tibet kujengwa, watalii wanaongezeka haraka, tumechukua hatua nyingi kuwaonesha na kuwafahamisha utamaduni wetu."

Mtaalamu wa taasisi ya utafiti wa sayansi ya jamii mkoani Tibet Bw. Tsering Phuntsog alisema, reli ya Qinghai-Tibet inawasaidia Watibet kufahamu mambo mengi nje ya Tibet na imeleta watalii wengi mkoani humo, na kutokana na mawasiliano hayo utamaduni wa Kitibet unaenea na kujulikana zaidi duniani.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-06