Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-06 15:53:43    
Utamaduni, mila na hisia za watu wa kabila la wa-sani wa sehemu ya msitu wa mawe

cri

Kwenye sehemu ya msitu wa mawe ya mkoani Yunnan, wanaishi watu wa kabila la wasani, ambao ni wa tawi la kabila la wayi nchini China. Wa-sani wamevumbua utamaduni pamoja na nyimbo na ngoma za "Ashima" za sehemu ya msitu wa mawe. Katika kipindi hiki cha leo tutawafahamisha utamaduni, mila na hisia za wakazi wa sehemu ya msitu wa mawe.

Kwenye sehemu ya msitu mdogo wa mawe, kuna ziwa moja lenye maji maangavu, kwenye kando ya ziwa hilo kuna jiwe moja refu linalofanana sana na msichana wa kabila la wa-sani aliyesimama. Kila siku kuna maelfu ya watalii wanaovutiwa na jiwe hilo, na watu wanakwenda kuliangalia na kupiga picha pamoja nalo. Msichana mwongoza watalii Bi Yunhua alituambia, hili ni "jiwe maarufu la Ashima", ambalo limekuwa jina la wasichana wote wa kabila la wa-sani. Alisema,

"Wasichana wote wa sehemu hiyo wanaitwa 'Ashima', neno hilo katika lugha ya kabila la wa-yi lina maana msichana mrembo. Wavulana wanaitwa kuwa 'kaka Ahei', neno hilo katika lugha hiyo ni kaka mshupavu na mwenye bidii za kazi."

Kuna hadithi moja kuhusu "jiwe la Ashima", kulikuwa na familia moja maskini, siku moja alizaliwa mtoto mmoja wa kike mzuri sana, babu na bibi yake walimpatia mjukuu wao jina la "Ashima". Ashima alikuwa hodari sana katika kuimba na kucheza ngoma, na alipendwa na vijana wengi. Msichana Ashima alimpenda kijana mmoja yatima aliyeitwa kaka Ahei, na alisema kuwa hataolewa na kijana yeyote mwingine isipokuwa kaka Ahei. Katika sikukuu ya vijinga ya mwaka mmoja, Ahei alimposa Ashima. Mtoto wa tajiri mmoja pia alimpenda sana msichana mrembo huyo Ashima, yule tajiri alimtuma mshenga aende nyumbani kwa msichana Ashima na kuwaeleza wazazi wake kuwa anataka kumwoa msichana huyo, pamoja na juhudi alizofanya yule mshenga katika kuzungumza, lakini alikataliwa kabisa. Siku moja, Ahei aliswaga kundi la kondoo kwenda kwenye malisho ya mbali, tajiri yule alituma watu kwenda kumchukua kwa nguvu msichana Ashima na kumlazimisha aolewe na mtoto wake, lakini msichana Ashima alikataa katakata na alikubali kufa kuliko kuolewa na mtoto wa tajiri. Kijana Ahei aliposikia habari hiyo alirudi haraka ili aweze kumwokoa Ashima. Tajiri huyo alikasirika sana alipowaona Ahei na Ashima wakijaribu kuvuka mto na kutoroka, hivyo alibomoa boma la bwawa, na maji yaliwazoa vijana hao. Kwa bahati nzuri hapo baadaye Ashima aliokolewa na msichana mwenzake, lakini msichana Ashima akageuka kuwa jiwe kubwa.

Wasani wa kabila la wayi wanaishi kwenye sehemu ya msitu wa mawe kizazi hadi kizazi. Wakazi wa sehemu hiyo wanapenda kujenga nyumba zao kwa mawe, toka karne kadhaa zilizopita wakazi wa huko wanajenga nyumba zao kwa kuchukua vipande vyembamba vya mawe vya huko kujenga nyumba na barabara. Bw. Huang Xing, ambaye anafanya utafiti kuhusu mila na desturi za wakazi wa huko tokea miaka mingi iliyopita, alituambia kuwa utamaduni wa mawe kwenye sehemu ya msitu wa mawe ulianza toka zamani.

"Mababu zetu waliishi na kulima mazao ya kilimo kwenye sehemu hii yenye sura ya ardhi ya chokaa, hivyo katika miaka laki nane iliyopita walifahamu kupambana na matatizo ya mazingira ya kimaumbile kwa kutumia mawe, na walivumbua utamaduni unaohusiana na mawe, toka vyombo vya mawe vilivyotumika katika zama za mawe vya zamani hadi vyombo vya mawe vinavyotumika katika uzalishaji mali na maisha."

Karibu na kila kijiji wanachoishi wa-sani kwenye sehemu ya msitu wa mawe kuna msitu mnene, wenyeji wa huko wanauita msitu wa Mizhi. Inasemekana kuwa ndani ya msitu mnene wa Mizhi kuna malaika anayelinda kijiji cha wa-sani, endapo watu wanaingia kwenye msitu wa Mizhi, malaika atakasirika, kama akiwapa adhabu ndogo basi watu hao wataugua ugonjwa, na kama akitoa adhabu kali, watu na mifugo itakufa. Katika mwezi Novemba kwa kalenda ya kichina, wa-sani wanaishi kwenye sehemu ya msitu wa mawe, hufika kwenye msitu wa Mizhi kufanya matambiko, wakimwomba malaika alinde usalama wa watu na mifugo yao na kuwaletea mavuno mazuri ya kilimo. Hii imekuwa sikukuu muhimu ya wa-sani. Kutokana na umuhimu wa misitu ya Mizhi kwa wa-sani katika imani yao, tokea miaka mingi iliyopita wa-sani wamekuwa wakiabudu malaika wa msitu wa Mizhi na kudumisha mila kuhifadhi misitu.

Katika historia ya miaka mingi iliyopita, wakazi wa huko wamejenga uhusiano mkubwa na ardhi ya msitu wa mawe pamoja na mawe yanayoumba sura ya ardhi ya chokaa. Michoro mingi iliyochorwa na wa-sani miaka mingi iliyopita kwenye mawe ya huko kuhusu shughuli za matambiko, ngoma, uwindaji na vita za wa-sani. Ushahidi huo umedhihirisha kuwa msitu wa mawe umeungana na pande mbalimbali za maisha ya wa-sani wa huko zikiwemo za dini, hadithi, mashairi, ngoma, utarizi, mavazi, majengo, sherehe na sikukuu.

Utamaduni na mila za makabila hayo madogo zimewapa kumbukumbu nyingi watalii kutoka nchi za nje waliotembelea msitu wa mawe. Bibi Briana Lopez kutoka Australia alisema,

"Tumevutiwa sana na vitu vya hapa, sehemu hiyo ina makabila mengi madogo, kufahamu historia na utamaduni wao ni jambo la kufurahisha sana."

Wa-sani wanaoishi kwenye sehemu ya msitu wa mawe, siyo tu kuwa wamevumbua utamaduni murua katika historia, bali pia wamevumbua sanaa ya utamaduni wa makabila. Lugha na maandishi ya kipekee ya wa-sani, mashairi na hadithi zenye mambo kemkem, mavazi na mapambo mazuri ya kikabila, nyimbo na ngoma zenye furaha za kikabila, mieleka na michezo mingine ya jadi pamoja na mila ya ndoa na mazishi, vyote vinaonesha umaalumu wa utamaduni wa makabila yaliyokuweko toka miaka mingi iliyopita na umaalumu wa kijiografia wa huko. Hadi sasa ni karne nyingi zimepita, hadithi kuhusu Ashima imekuwa sehemu moja ya maisha, ndoa, mazishi pamoja na mila na desturi nyingine zinazopokezana kati vizazi vya wa-sani.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-06