Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-07 14:43:03    
Barua 0805

cri

Kwanza tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, hivi karibuni mwandishi wetu wa habari aliyeko Nairobi Kenya amekuwa akipigiwa simu mara kwa mara akiambiwa kuwa, karibu nusu mwaka umepita sasa wasikilizaji hao hawajapata barua au bahasha na vitu vingine kutoka kwa Radio China Kimataifa. Kwa kweli tunasikitishwa na hali hii, kwani mfanyakazi mwenzetu anayeshughulikia Barua Bw Huang kila siku anafanya kazi kwa makini sana kuhakikisha kuwa kila msikilizaji anatumiwa kadi za salamu, barua na hata zawadi tunazowatumia wasikilizaji wetu. Kutokea kwa hali hiyo, inawezekana ni kutokana na kuchelewa kwa barua posta. Na sisi pia tunachelewa kupata barua kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Peris Lily Shipenzi wa sanduku la Posta 2519 Kakamega Kenya, ameanza barua yake kwa kutusalimia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa akiwa na matumaini kuwa tunaendelea kuchapa kazi ya kurusha matangazo vizuri na kwa wakati. Kwa upande wake anasema yeye ni mzima na anaendelea na ujenzi wa taifa bila kusahau kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa kwa habari na vipindi vinavyoelimisha na kuburudisha. Pia anatoa pongezi kwa namna lugha ya Kiswahili inavyotumika kwa ufasaha na kwa kuongezwa muda wa matangazo na vipindi kupitia KBC na katika matangazo ya FM. Anasema uamuzi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kujenga uhusiano mzuri na kutoa nafasi ya mawasiliano kati ya Radio China Kimataifa na wasikilizaji wake.

Pamoja na hayo anasema lengo la barua yake hii ni kuomba uanachama wa CRI ili aorodheshwe miongoni mwa wasikilizaji wetu na anasema atafurahi sana iwapo atapata nafasi hii ambayo si rahisi kuipata, ili aweze kushirikiana na wasikilizaji wengine kupitia katika vipindi mbalimbali kama vile salamu na chemsha bongo. Hivyo anaomba kutumiwa namba ya uanachama, kadi za salamu, majarida au magazeti yanayoelezea historia ndefu ya Radio China Kimataifa na Taifa la China, Beji ya CRI, Kalenda na zawadi nyinginezo. Anasema ana matumaini kuwa tutamtumia zawadi hizo kwani tutatilia maanani kuwa ni mara yake ya kwanza kutuandikia na kutusalimia, na zawadi tutakazomtumia zitakuwa changamoto kwake ili ashiriki kikamilifu kutoa maoni, mapendekezo na fikra zenye mantiki kwa lengo la kuboresha zaidi vipindi vyetu katika ngazi ya kimataifa.

Pia anapenda kuwasalimu wafuatao, Dada Phoebe Muwala ? Humjunya Krabas, Yakub Saidi Idambira ? Kakamega, Mbaraka Mohamed Abucheri ? Kakamega, Dada Miriam Akata ? Namakara Kabras, Mbarouk Msabah ? Dubai, Shemeji Zebadayo Muwala ? Humjunya, Mtoto Rufaida Mbarak ? Kakamega, Ujumbe wake unasema, Tushirikiane kupitia CRI, jukwaa la manufaa na maendeleo. Mwisho anatutakia kila la kheri na baraka kwa mwaka 2007 na 2008.

Tunamshukuru Bwana Peris Lily Shipenzi kwa barua yake tunamkaribisha kwa mikono miwili awe mwanachama wa Radio China Kimataifa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu kwa makini na kutoa maoni na mapendekezo ili kutusaidia kuandaa vipindi vyetu vizuri .

Msikilizaji wetu mwingine ni Yakub Saidi Idambira wa sanduku la Posta 2519 Kakamega, Kenya. Yeye pia ameanza barua yake kwa salamu kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, akiwa na matumaini kuwa ni wazima na tunaendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia wasikilizaji kwa kutangaza vipindi mbalimbali vyenye kuelimisha, kutoa habari na kuburudisha. Anasema yeye ni mzima wa afya na anaendelea na shughuli za ujenzi taifa na kuendelea kuitegea sikio Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ili apate uhondo na kuburudisha moyo wake. Baada ya salamu hizo Bw. Yakub anasema lengo la kutuandikia barua, kwanza ni kutaka kutufahamisha kuwa alipokea zawadi ya Fulana maridadi yenye nembo ya Radio China Kimataifa. Hivyo anapenda kutumia nafasi hii kushukuru sana kwa zawadi hiyo ambayo imemfanya awe na furaha tele na kuona kitendo hicho kimedhihirisha wazi kuwa Radio China Kimataifa ni yenye kusema na kutenda, na siyo ya ahadi na maneno matupu.

Anapenda kutoa changamoto kwa Radio China Kimataifa kuendeleza utaratibu huo ambao umeipa sifa kutoka kwa wasikilizaji wake wengi kote duniani na kuonesha kuwa taifa la China ni la watu wastaarabu na wenye ukarimu mkubwa kwa watu wengine na hasa wasikilizaji wake wazuri walioko sehemu mbalimbali. Pia anasema anatumai kuwa ukarimu huo utaendelea kwa manufaa ya wasikilizaji na hasa wanaoshiriki kwenye chemsha bongo. Na ushauri wake kwa wale ambao hawajabahatika kupata zawadi wasife moyo bali waendelee kufanya bidii katika kushiriki mara nyingi, kwani huenda baadaye watabahatika. Anapenda kutufahamisha kuwa mwanachama mwenye namba 608 hayupo nasi, hivyo anaomba namba hiyo tumpe msikilizaji wetu maarufu Mbarak Mohamed Abucheri.

Anatumai kuwa tutampa namba hiyo na kumfahamisha kwa barua kuhusu suala hilo. Namba nyingine ambayo anapenda tumpe mwanachama mgeni Peris Lily Shipenzi ni namba 805 kwani anasema mwenye namba hiyo hana nafasi ya kuwasiliana na Radio China kimataifa kutokana na kuwa na shughuli nyingi. Pia anaomba tuwasiliane naye kwa njia ya barua ili kumfahamisha kuhusu mabadiliko hayo. Anasema kwa wakati huu yuko mbioni kuwasajili wanachama wapya wa Radio China Kimataifa mkoani magharibi, ili kufanikisha usikilizaji wa matangazo na vipindi vya Radio China Kimataifa.

Mwisho anasema anapenda tuanzishe utaratibu wa kutoa kadi za uanachama ili kusaidia katika uratibu. Kwa upande wa kadi za salamu anaomba tusiegemee upande mmoja bali tuwe na usawa na anatarajia hali hii tutairekebisha. Katika barua yake nyingine aliyotuandikia Bw. Yakub Saidi anatoa pole kwa wafanyakazi na wataalamu wa kichina ambao wamekumbwa na matukio ya kutekwa nyara katika sehemu mbalimbali ambapo wamekwenda kutoa huduma za kijamii kama vile kujenga barabara, kuchimba visima vya mafuta na shughuli nyingine zenye manufaa kwa maendeleo ya jamii. Hivyo ana huzuni na masikitiko makubwa kutokana na wataalamu wa kichina kuuawa kinyama bila makosa yoyote. Anasema vitendo hivi kwa hakika ni vya aibu na vinaonesha kutokuwa na utu na pia vinaonesha ukosefu wa kutokumjua mungu kwa kiasi kikubwa. Anayaomba mataifa makubwa kuweka mikakati ya kuwa na usalama madhubuti ili kuwavutia wawekezaji na pia watalii kutoka sehemu mbalimbali kutembelea nchi mbalimbali salama.

Matumaini yake kwa mataifa husika ni kufanya juhudi katika kuimarisha na kudumisha usalama na amani katika mataifa yao ili kulinda hadhi na sifa nzuri za mataifa hayo. Anasema ukosefu wa usalama umechangia kwa kiasi kikubwa kwa wawekezaji kuogopa, kukosekana kwa maendeleo na kusababisha ukosefu wa ajira kwa watu wengi. Hivyo basi anasema ni muhimu kuzingatia suala la usalama popote pale iwe nyumbani, shuleni, kazini na hotelini kwa ajili ya kutoa huduma bora. Anawapa pole ndugu na jamaa wa wataalamu waliouawa na anawaomba wawe na moyo wa subira na uvumilivu.

Pia anawahimiza wataalamu wengine wasivunjike moyo kutokana na kuwepo kwa usalama mdogo bali wajitahidi na kuendelea kufanya kazi zao na utafiti bila kukata tamaa na mungu atawasiadia, kwa vile wanafanya kazi ya manufaa kwa ajili ya watu wengi bila ya ubaguzi, uchoyo na chuki bali kwa moyo mmoja ukarimu, bidii na kujitolea. Anatarajia kuwa wataalamu hao watatiwa moyo na kuhamasishwa ili waendelee kutoa mchango wao wa maendeleo kwa kuhakikishiwa usalama. Mwisho anasema kwa niaba ya wasikilizaji wenzake anatoa salamu za pole kwa jamaa na Jamhuri ya watu wa China kwa jumla kutokana na matukio yaliyowapata wataalamu wa kichina, anasema poleni nyote na maisha marefu taifa, watu, na wataalamu wa China na vilevile anaitakia Radio China Kimataifa pamoja na wasikilizaji wetu maisha marefu.

Tunamshukuru sana Bwana Yakub Saidi Idambira kwa barua yake inayotueleza mengi na kutoa ufuatiliaji wake kwa wafanyakazi na wataalamu wa China wanaofanya kazi katika nchi za nje, ambao mara kwa mara walikumbwa na tishio la mashambulizi. Kweli ufuatiliaji wake unatutia moyo sana, wasikilizaji wetu wengi wana hisia za upendo kwa wananchi wa China, hii inatuhimiza tuchape kazi vizuri ili kuwahudumia vizuri wasikilizaji wetu. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu. Na kuhusu malalamiko ya kipindi cha salamu zenu, kweli tunajitahidi sana kuweka uwiano kuhakikisha kuwa wasikilizaji wote wanaotuma kadi za salamu wanapata nafasi, kama ukisikia kuwa tumesoma zaidi kadi za upande fulani, basi ni kutokana kuwa tumepokea kadi hizo nyingi na si kwa sababu ya upendeleo. Lakini tunakushukuru sana kwa maoni yako.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-07