Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-07 15:18:18    
Mazungumzo kati ya Marekani na Iran hayawezi kuboresha hali ya Iraq katika muda mfupi

cri

Baada ya maduru mawili ya mazungumzo ya ngazi ya kibalozi yaliyofanyika kati ya Marekani na Iran mwezi Mei na Julai, tarehe 6 Agosti wajumbe wa nchi mbili walikutana mjini Baghdad na kufanya mazungumzo ya pande tatu, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa Iraq. Baada ya mazungumzo, mabalozi wa Marekani na Iran nchini Iraq walikutana. Vyombo vya habari vinaona kuwa mazungumzo hayo ni sawa na mazungumzo ya maduru mawili yaliyopita, mazungumzo yaliyofanyika tarehe 6 Agosti hayakupata mafanikio makubwa.

Mazungumzo ya tarehe 6 Agosti yaliamuliwa kufanyika na mabalozi wa Marekani na Iran walipokutana tarehe 24 Julai. Mada ya mazungumzo hayo ni kujadili muundo wa kamati ya usalama ya pande tatu na mpango wa kazi. Vyombo vya habari vinaona kuwa mazungumzo hayo ni mwanzilishi wa kamati hiyo ya pande tatu. Baada ya mazungumzo, mabalozi wa Marekani na Iran nchini Iraq walifanya mazungumzo tena kutokana na mwaliko wa mshauri wa usalama wa taifa la Iraq Bw. Mowaffak al-Rubaie.

Kwa mujibu wa msemaji wa ubalozi wa Marekani nchini Iraq, ujumbe wa Marekani uliongozwa na ofisa anayeshughulika na mambo ya kisiasa na kijeshi katika ubalozi wa Marekani nchini Iraq. Msemaji alisema mazungumzo yalikuwa ya wazi na makini, na pande zote zilikubali kuwa mazungumzo yataendelea. Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Sean McCormack alisema, mazungumzo ni ya kiujenzi. Lakini mjumbe wa Iran aliposifu uwazi wa mazungumzo hayo pia aliishutumu Marekani kwamba kutokana na Marekani kuikalia Iraq, hali ya usalama nchini Iraq inazidi kuwa mbaya.

Vyombo vya habari vinaona kuwa ingawa pande mbili za Marekani na Iran zote zinataka mazungumzo yaendelee, lakini pande mbili hazikutaja mazungumzo yajayo yatafanyika lini. Pamoja na hayo, baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa saa nne, pande tatu hazikueleza chochote kama zimefikia makubaliano kuhusu utaratibu wa kazi wa kamati ya usalama ya pande tatu. Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wanaona kuwa si mazungumzo ya ngazi ya kibalozi kati ya Marekani na Iran au mazungumzo hayo ya kamati ya usalama ya pande tatu, yataweza kuboresha hali ya usalama nchini Iraq katika muda mfupi. Sababu ni tatu zifuatazo:

Kwanza, Marekani na Iran zinaendelea kuwa na tofauti kubwa kuhusu suala la usalama wa Iraq. Marekani inashutumu Iran kutoa msaada wa silaha kwa watu wenye silaha wa madhehebu ya Shia nchini Iraq na kuwafundisha watu hao. Marekani inataka Iran isimamishe kutoa msaada wake kwa watu wenye silaha wanaopambana na jeshi la Marekani nchini Iraq. Iran inasisitiza kuwa hali mbaya ya usalama wa Iraq inasababishwa na ukaliaji wa Marekani nchini humo. Kuhusu tofauti hizo pande mbili zinagongana moja kwa moja bila kurudi nyuma. Katika hali kama hiyo, kuanzisha kamati hiyo ya usalama ya pande tatu hakutasaidia kitu.

Pili, Uhusiano mbaya kati ya Iran na Marekani unaendelea na hakuna dalili yoyote ya kuboreshwa. Manowari tatu zenye ndege za Marekani zimepangwa kwenye Ghuba ya Uajemi, na habari nyingine zinasema rais George Bush wa Marekani anataka kuishambulia Iran kabla ya kipindi chake cha urais kumalizika. Isitoshe, watu wanne wa Marekani wenye asili ya Iran wanashikiliwa nchini Iran kwa tuhuma za ujasusi, wanadiplomasia watano wa Iran wametiwa mbaroni na jeshi la Marekani nchini Iraq kwa tuhuma za kuharibu utulivu wa Iraq. Mambo hayo yote yatakuwa na athari mbaya kwa mazungumzo yanayofanyika hivi sasa.

Tatu, Hali ya vurugu nchini Iraq inatokana na mambo mengi, migogoro kati ya madhehebu ya Suni, Shia na wa-Kurd, uharibifu unaofanywa na watu wenye siasa kali wa Al-Qaida na tofauti kati ya vyama vya kisiasa nchini Iraq, yote hayo yanachangia hali mbaya ya usalama nchini Iraq. Na Sababu nyingine ni majeshi ya nchi za nje kuikalia nchi hiyo ya Iraq, kwa hiyo mradi tu majeshi ya nchi za nje yakiendelea kuwepo nchini humo, hali mbaya ya usalama wa Iraq itaendelea kuwepo.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-07