Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-07 15:36:41    
Ulinzi wa alama za kijiografia wasaidia kuhimiza maendeleo ya kilimo cha China

cri

Alama za kijiografia ni alama zinazotumika katika bidhaa zenye vyanzo maalum vya kijiografia na sifa zinazohusika na sehemu zinazotengeneza bidhaa hizo. Kwa ufupi, alama za kijiografia zinatengenezwa kwa jina la sehemu zinazotengeneza bidhaa hizo. Kwa kuwa alama hizo zinaweza kuonesha umaalum wa bidhaa, hivyo zinazifanya bidhaa hizo ziwe na nguvu zaidi za kuvutia kwenye masoko. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imekuwa inatilia maanani sana ulinzi wa alama za kijiografia, na kuzitumia ili kuhimiza maendeleo ya shughuli za kilimo zenye umaalum.

Ukitaja saa za mkononi, hakika utakumbuka nchi ya Uswisi. Ndiyo, saa za mkononi zinazotengenezwa nchini Uswisi ni maarufu duniani kutokana na kuwa zinaonekana zinapendeza, zinatunza muda vizuri na zimetengenezwa vizuri. Chapa kama saa za mkononi za Uswisi zimeonesha sehemu zinazotengeneza bidhaa, na sifa bora za bidhaa, ndiyo alama za kijiografia. Mchele unaonukia wa Thailand, punje za kahawa za Jamaica zote ni alama maarufu za kijiografia duniani.

Nchini China pia kuna alama nyingi za kijiografia zinazokubaliwa na watu, kama vile matunda ya mapea ya Korla ya Xinjiang na kitambaa cha Hariri chenye maua au mapambo yaliyofumwa cha Nanjing. Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa inatilia maanani sana ulinzi wa alama za kijiografia, na viwanda pia vinaelewa umuhimu wa alama za kijiografia. Imefahamika kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, China imeshughulikia maombi zaidi ya 700 ya alama za kijiografia, miongoni mwake 251 zimesajiliwa, na mengi kati ya hayo ni maombi kuhusu mazao ya kilimo.

Matunda ya "Mapea ya Korla" yanayozalishwa kwenye mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, kaskazini magharibi ya China, ni mazao ya kwanza yaliyopata usajili wa alama ya kijiografia nchini China. Katibu mkuu wa shirikisho la wakulima wa matunda ya matunda hayo la Xinjiang Bw. Guo Qiuzhi alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kusajiliwa kwa alama ya kijiografia ya matunda hayo kumeinua kwa kiasi kikubwa juhudi za wakulima wa huko kupanda matunda hayo.

Imefahamika kuwa, baada ya kusajiliwa kwa alama za kijiografia, kujulikana kwa matunda ya mapea ya Korla kumeongeza, hivyo wafanyabiashara wanakuja mmoja baada ya mwingine, na bei ya matunda hayo pia inapanda. Hivi sasa bei ya boksi moja la matunda ya mapea ya Korla ni Yuan za RMB 5 hadi 7 zaidi kuliko matunda ya kawaida ya mapea, na wakulima wanapata faida halisi.

Faida zinazoletwa na kusajiliwa kwa alama za kijiografia sio tu kunasaidia wakulima wa China kuongeza mapato yao. Kwa kweli kusajiliwa kwa alama za kijiografia pia kumeonesha nguvu kubwa za kuhimiza uuzaji nje wa bidhaa. Bw. Guo Qiuzhi alisema, kabla ya kusajili alama za kijiografia, ilikuwa vigumu kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa nchi za nje, kwa sababu wafanyabiashara hawakuwa na imani kubwa kwa sifa za bidhaa, hivyo mara nyingi walifanya mazungumzo ya muda mrefu bila mafanikio yoyote, lakini sasa hali ni tofauti kabisa. Alisema:

"Mwaka jana, mara tu Peru na Argentina zilipoambiwa kuwa matunda ya mapea ya Korla yanachukuliwa kuwa ni chapa maarufu ya China, na kusajiliwa kwa alama za kijiografia, zilisaini makubaliano haraka. Kusajili alama za kijiografia kunaharakisha mchakato wa mazungumzo, au kufikia makubaliano, na kiwango cha kutambuliwa na wafanyabiashara kwa bidhaa hizo kinainuka."

"Siki ya Zhenjiang yenye harufu nzuri" ambayo ni bidhaa maalum ya mkoa wa Jiangsu, mashariki mwa China, iliuzwa kwa nchi za nje kuanzia mwanzoni mwa karne iliyopita, sasa hali ya uuzaji wake kwa nje bado inafurahisha. Shirikisho la viwanda vya siki la mji wa Zhenjiang Bibi Jiangmin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kusajiliwa kwa siki ya Zhenjiang licha ya kuhimiza uuzaji bidhaa kwa nje, pia kunatoa mchango muhimu katika kulinda haki za viwanda. Alisema:

"Tumegundua kuwa watu wa sehemu nyingine walitumia 'siki ya Zhenjiang' kusajili kampuni huko Hongkong. Baada ya kusajili alama za kijiografia, siki zinazotengenezwa hapa Zhenjiang tu zinaweza kuitwa "siki ya Zhenjiang", licha ya hayo tunaweza kulinda hakimiliki yetu. Kusajili alama za kijiografia kunatusaidia sana katika upande huo."

Kwa mujibu wa sheria husika za hakimiliki ya ubunifu, baada ya kusajiliwa kwa alama fulani ya kijiografia, bidhaa nyingine zinazofanana ambazo zinatengenezwa sehemu nyingine haziwezi kutumia alama hiyo, kufanya hivyo kunaweza kulinda vizuri wanaomiliki alama za kijiografia.

Kwa kweli juhudi za China katika ulinzi wa alama za kijiografia na matokeo inayopata ni makubwa. Kwenye mkutano wa alama za kijiografia duniani uliofunguliwa mwishoni mwa mwezi Juni, naibu waziri mkuu wa China Bibi Wu Yi alisema, China inatumia alama za kijiografia kulinda na kuendeleza mazao ya kilimo, na inahimiza kwa ufanisi kuongezeka kwa mapato ya wakulima na maendeleo ya vijiji.

Msaidizi wa katibu mkuu wa shirika la hakimiliki ya ubunifu duniani Bibi Wang Binying kwenye mkutano huo alisifu kazi za ulinzi wa alama za kijiografia za China katika miaka ya karibuni. Alisema:

"Tunafurahi sana kuona kuwa, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China imekuwa inatilia maanani sana ulinzi wa alama za kijiografia, na imepata matokeo halisi. Imehimiza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kilimo, na kuongeza mapato ya wakulima. Tunatumai kuwa katika siku za usoni kazi za serikali ya China katika upande huo itakuwa na ufanisi zaidi, na kupata maendeleo makubwa zaidi."

Tarehe 11 Julai, China na Umoja wa Ulaya zilibadilishana rasmi nyaraka kuhusu alama 10 za kijiografia za bidhaa zinazoomba ulinzi wa upande mwingine. Kama nyaraka hizo zitapitishwa na Umoja wa Ulaya, basi bidhaa hizo zitakuwa na ulinzi maalum wa hali ya juu wa alama za kijiografia, ambao ni sawa na ulinzi kwa bidhaa zenye alama za kijiografia za huko. Tunaamini kuwa ulinzi wa alama za kijiografia wa China utakamilishwa katika siku za usoni, na zitazidi kuhimiza kilimo cha China.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-07