Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-08 10:58:27    
Shughuli za software ya China zafuata njia ya uvumbuzi wa kujitegemea

cri

Kutokana na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia, teknolojia na shughuli za software zikiwa ni sehemu muhimu katika shughuli za upashanaji wa habari, zimekuwa eneo muhimu linalohusiana na maendeleo ya uchumi na jamii ya China. China ikiwa ni nchi inayoendelea, imethibitisha njia ya kuendeleza shughuli hizo kwa uvumbuzi wa kujitegemea.

Katika miaka ya hivi karibuni, shughuli za software za China zimekuwa zinaongezeka kwa kasi, mwaka 2006 pato la jumla la shughuli hizo limefikia Yuan bilioni 480. Uwezo na nguvu ya ushindani ya shughuli hizo vimeongezeka kidhahiri. Kwenye maonesho ya 11 ya software ya kimataifa ya China yaliyofanyika hivi karibuni, makampuni ya software ya China yameonesha bidhaa na teknolojia zao mpya.

Kampuni ya software ya UFIDA ya China ni kampuni kubwa kabisa ya kusanifu software za usimamizi nchini China. Hivi sasa software za kampuni hiyo zinatumiwa na makampuni zaidi ya laki 5 kote nchini China na kwenye sehemu ya Asia na pasifiki. Software za aina ya ERP (Enterprise Resource Planning) ni bidhaa muhimu ya kampuni hiyo, software hizo zinasaidia makampuni kusimamia kwa ufanisi data kuhusu wateja, malighafi na nguvukazi, pamoja na shughuli za mambo ya fedha, uuzaji na usambazaji wa bidhaa, ili kuinua ufanisi wa usimamizi wa makampuni. Katika maonesho ya 11 ya software ya kimataifa ya China, kampuni ya UFIDA imeonesha software zake mpya za usimamizi wa kampuni zenye hakimiliki kamili. Maneja wa usimamizi wa chapa wa kampuni hiyo Bw. Shu Liwen alisema, kampuni ya UFIDA inaweza kusanifu software tofauti za usimamizi kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya makampuni. Bw. Shu Liwen alisema:

"software za U8 ni kubwa na muhimu kwenye uzalishaji wa bidhaa zetu, ambazo ni software za usimamizi wa nguvukazi na uuzaji wa bidhaa kwa ajili ya makampuni madogo na ya wastani. Kwa makampuni makubwa, tunatoa software za mpango wa jumla wa usimamizi ambazo ni software zenye uwezo kamili zaidi kote nchini China, na zinatumiwa na makampuni makubwa zaidi ya elfu moja."

Bw. Shu Liwen alisema, katika miaka mitatu ijayo, kampuni ya UFIDA inapanga kutoa software za usimamizi za aina nyingi zaidi, pamoja na huduma bora za ufuatiliaji, ili kutimiza ongezeko jipya la shughuli za huduma za software hizo.

Ikilinganishwa na software za ERP zinazozidi kupevuka, shughuli za software za kutengeneza katuni zimeanzishwa nchini China katika miaka ya hivi karibuni. Hivi sasa makampuni ya China yametoa software ya aina hiyo yenye hakimiliki, uwezo wake unafanana na software maarufu za 3DMAX na MAYA. Kwa kutumia software hiyo ya China, watumiaji wanachagua nukta kadhaa tu kwenye skrini ya kompyuta, mfumo wake utaweza kuonesha matokeo mbalimbali, yakiwemo mtitiriko wa maji, mawimbi, moshi na moto.

Kwa kutumia software hiyo ya kisasa, China itaweza kutengeneza filamu nyingi za katuni zinazopendeza. Naibu maneja mkuu wa Kampuni ya burudani ya utamaduni ya Yuanchuangdongli ya Guangdong Bi. Liu Manyi alisema, hivi sasa bidhaa za katuni za kampuni hiyo zinaweza kushindana kiteknolojia na zile za nchi zilizotangulia katika eneo hilo zikiwemo Marekani na Japan. Bi. Liu Manyi alisema:

"tunaweza kutengeneza katuni za aina mbalimbali na sura za wahusika wa katuni zimeonekana ni nzuri zaidi. Utungaji wetu una mtindo wetu wa kipekee."

Bi. Liu Manyi alisema, maendeleo yaliyopatikana kwenye kampuni hiyo yanatokana na uungaji mkono wa serikali ya China kwa shughuli za utengenezaji wa katuni kwa kujitegemea. Kwa mfano, mwezi Oktoba mwaka 2006, serikali ya mji wa Guangzhou iliamua kutenga Yuan milioni 150 katika miaka mitano ijayo kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa vituo vya utengenezaji wa katuni na software husika, kuhimiza uvumbuzi na kuyasaidia makampuni hayo yakue na yawe ya kimataifa.

Ingawa mafanikio makubwa yamepatikana, lakini shughuli za software za China pia zinakabiliwa na masuala mbalimbali, kwa mfano shughuli hizo na makampuni yake bado ni ndogo, inachukua hisa ndogo katika sekta ya software duniani, na bado ina pengo kubwa kuliko ile ya nchi zilizoendelea. Kwenye maonesho ya 11 ya software ya kimataifa ya China, naibu waziri wa upashanaji wa habari wa China Bw. Lou Qingjian alisema, muda wa miaka mitano ijayo ni kipindi muhimu kwa maendeleo ya shughuli ya software ya China. Mahitaji ya matumizi ya software katika sekta mbalimbali na maendeleo ya kasi ya mtandao wa Internet yote yanatoa fursa muhimu kwa maendeleo ya shughuli hiyo nchini China. Ili kuunga mkono zaidi maendeleo ya shughuli hiyo kwa utulivu, China itaendelea kuimarisha utungaji wa sheria husika, kuinua uwezo wa uvumbuzi kwa kujitegemea, kuimarisha maendeleo ya pamoja ya software na hardware na kuhimiza shughuli hiyo iwe ya kimataifa. China pia itaendelea kuongeza nguvu ya kushughulikia software zilizorudufiwa kwa njia haramu na zile zenye kusudi baya, ili kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya shughuli ya software. Bw. Lou Qingjian alisema:

"Software na huduma za upashanaji habari zinachukua hisa kubwa zaidi katika biashara kote duniani, China ikiwa ni ni nchi inayoendelea, inataka kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na nchi mbalimbali duniani na kusukuma mbele kwa pamoja maendeleo ya shughuli ya software ya China."

Idhaa ya kiswahili 2007-08-08