Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-09 18:42:22    
Jumuiya ya kimataifa yafanya juhudi nyingine kwa ajili ya utatuzi wa suala la usalama wa Iraq

cri

Kamati ya ushirikiano na uratibu wa usalama wa nchi jirani za Iraq tarehe 8 iliitisha Mkutano huko Damascus, mji mkuu wa Syria, kujadili hali ya usalama wa Iraq na usalama wa sehemu za mipaka kati ya Iraq na nchi jirani zake. Wajumbe kutoka Syria, Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Jordan na Iraq walihudhuria Mkutano huo. Wajumbe wa Umoja wa nchi za kiarabu na Umoja wa Mataifa pamoja na mabalozi wa kudumu wa nchi wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa nchini Syria wakiwa wachunguzi pia walihudhuria Mkutano huo. Hizi ni juhudi nyingine zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa ili kujaribu kutatua suala la usalama wa Iraq.

Kutokana na habari zilizodokezwa kutoka kwenye Mkutano huo, wajumbe waliohudhururia Mkutano huo walifuatilia zaidi masuala kama yafuatayo:

Kwanza ni namna ya kuisaidia Iraq kupambana na nguvu za ugaidi nchini humo. Hivi sasa jumuiya ya kimataifa imekuwa na maoni ya pamoja kwamba vita iliyoanzishwa na Marekani dhidi ya Iraq ni athari mbaya kubwa ambayo iliziingiza "shughuli za ugaidi za kundi la al Qaida" nchini Iraq. Wakati huo huo kwa kuwa jeshi lililoundwa wakati wa utawala wa Saddam na kikosi cha askari polisi cha wakati huo vimekataliwa kushiriki kwenye serikali mpya, hivyo wapo wachache tu maofisa na askari wenye uzoefu wa mapigano katika jeshi jipya na kikosi cha askari polisi cha hivi sasa, wengi kati yao wanashindwa kubeba majukumu yao ya hivi sasa. Ndiyo maana kuwaandaa askari wa kikosi cha usalama na askari polisi wa Iraq kumekuwa kazi ya dharura. Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa nchi za kiarabu Hasham Yousuf alisisitiza kuwa, majeshi ya nchi za nje nchini Iraq yanapaswa kubeba wajibu wa kuhakikisha usalama, na kuhakikisha haki za binadamu za raia wa Iraq na kusaidia kuandaa kikosi cha usalama cha Iraq. Aidha washirika wa Mkutano huo wameona kuwa, nchi jirani za Iran, hasa Iran, Syria na Saudi Arabia zinapaswa kuchukua hatua zenye ufanisi za kuwazuia watu wenye silaha wasijipenyeze kuingia nchini Iraq, na kukata chanzo cha "ugaidi". Waziri wa mambo ya ndani wa Syria Bassam Abdel Majid tarehe 8 alisema kwenye ufunguzi wa Mkutano kwamba Syria imeweka vituo vya ukaguzi kwenye mpaka kati ya Syria na Iraq ili kuwazuia wakazi haramu na vitu vilivyopigwa marufuku visiingie nchini Iraq, tena kuweka vizuizi kwa watu wanaotaka kuingia nchini Syria.

Aidha washirika wa Mkutano huo wametoa mwito wa kukomesha mapema iwezekanavyo migogoro ya madhehebu nchini Iraq, kutimiza maafikiano ya kitaifa na kuharakisha mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo. Baada ya kuanza kwa vita vya Iraq migogoro kati ya wairaq wa madhehebu ya Suni, Shia na wakurd inatokea bila kusita. Sababu inatokana na uadui wa watu wa madhehebu ya Shia na wakurud dhidi ya watu wa madhehebu ya Suni wakati wa utawala wa Saddam, pia ni kutokana na kuingilia kati kwa nguvu ya nchi za nje. Na migogoro kati ya madhehebu ya kidini kwa kiasi fulani imeonesha matakwa tofauti ya kisasa ya madhehebu hayo. Tokea mwaka huu uanze, mawaziri 6 wanaomwunga mkono kiongozi wa madhehebu ya Shia Bw Moqtada al Sadr, mawaziri wengine 6 wa chama cha Accordance cha madhehebu ya Suni pamoja na mawaziri watano wa chama cha Iraqiya List kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Iyad Allawi, kwa nyakati tofauti walisusia serikali, na kuwafanya nusu ya mawaziri wa serikali ya Iraq kusita au kuacha kazi zao kwa muda. Ndiyo maana washirika wa Mkutano walitoa mwito kuwataka wairaq wazingatie zaidi mambo makuu na kuacha migogoro. Aidha nchi zinazohusika za kiarabu na kiislamu pia zinapaswa kufanya juhudi za kusaidia kutimiza maafikiano ya kitaifa ya Iraq nzima badala ya kuunga mkono watu au vyama vya madhehebu.

Na washiriki wa Mkutano pia wametaka kupata ufumbuzi wenye ufanisi ambao si kama tu unaweza kulinda utulivu wa Iraq, bali pia unasaidia kuondoa mapema majeshi ya nchi za nje. Walidhihirisha kuwa, hali ya usalama nchini Iraq kwa hivi sasa inahusiana sana na kuwepo kwa majeshi ya nchi za nje nchini Iraq. Mkutano huo umeonesha matumaini ya jumuiya ya kimataifa ya kuitaka Iraq iweze kutimiza usalama na utulivu mapema iwezekanavyo. Lakini hivi sasa kuna utatanishi mwingi katika suala la usalama wa Iraq, utatuzi wa suala hilo unaitaka serikali ya Iraq na jumuiya ya kimataifa zichukue hatua zinazofuata hali halisi.