Tarehe 9 Agosti ni siku ya kimataifa ya watu wa jamii za kiasili. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alitoa hotuba ya maandishi akitaka jumuyia ya kimataifa ichukue hatua ili kuhakikisha haki na maslahi yao yanalindwa.
Bw. Ban Ki-moon alisema, hivi leo watu wa jamii za kiasili bado wanakabiliwa na hali ya kubaguliwa na kupuuzwa, ardhi yao na njia yao ya kujipatia maisha inazuiwa, na utamaduni wao utaharibiwa na pengine utatoweka kabisa. Bw. Ban Ki-moon anaona kuwa jumuyia ya kimataifa inatakiwa kuchukua hatua za kushughulika na masuala hayo.
Mpaka sasa jumuyia ya kimataifa bado haina tafsiri bayana kuhusu watu wa jamii za kiasili. Kwa kawaida watu hao ni watu wanaoishi kizazi baada ya kizazi katika nchi na sehemu fulani kabla ya watu wa makabila mengine kuingia huko, na utamaduni wao unamomonyolewa na watu wa nje, kwa mfano watu wa India barani Amerika, watu wa Maori wa Oceania na watu wanaoishi karibu na ncha ya kaskazini ya dunia. Kwa makadirio ya Umoja wa Mataifa, kuna jamii za kiasili kiasi cha 5,000 katika nchi 70 hivi, idadi yao inazidi watu milioni 370. Kutokana na kubaguliwa kwa muda mrefu, watu hao ni maskini sana na utamaduni wao uko hatarini kutoweka.
Hali mbaya ya watu hao imesababisha ufuatiliaji mkubwa wa jumuyia ya kimataifa. Mwezi Juni mwaka 1993 wakati mkutano mkuu wa kutetea haki za binadamu ulipofanyika mjini Vienna, mkutano wa kimataifa wa kila mwaka kuhusu watu wa jamii za kiasili pia ulifanyika, mkutano huo ulitaka jumuyia ya kimataifa itilie maanani kuwepo kwa watu wa jamii za kiasili, kuheshimu historia halisi na utamaduni wa jadi na kuhakikisha haki zao za kuishi sawa na wengine. Mwishoni mwa mwaka huu baraza kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kuwa kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2004 iwe "miaka kumi ya kimataifa ya watu wa jamii za kiasili", na kuifanya tarehe 9 Agosti iwe "siku ya kimataifa ya watu wa jamii za kiasili". Tokea mwaka 1985 mswada wa "taarifa kuhusu haki za watu wa jamii za kiasili" ulianza kuandikwa. Baada ya mazungumzo yenye utatanishi yaliyofanyika kwa zaidi ya miaka 20, mwezi Juni mwaka jana taarifa hiyo ilipitishwa kwenye mkutano wa kwanza baada ya shirika la kutetea haki za binadamu kuanzishwa. Lakini mswada huo ulipowasilishwa kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa uligonga ukuta. Nchi za Afrika zilitaka kurekebisha mswada huo katika sehemu nyingi. Kwa mfano, zilitaka kufuta kifungu ambacho watu wa jamii za kiasili wana haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe. Imefahamika kuwa matakwa hayo ya nchi za Afrika yanahusika na masuala ya watu wa jamii za kiasili wanaoishi Marekani, Australia, Canada na New Zealand. Nchi hizo ingawa zinajitahidi kutunga mswada huo wa taarifa, lakini zinapinga vifungu vinavyohusika na haki ya kujiamulia mambo, haki za ardhi na haki za kumiliki maliasili. Kutokana na kuathiriwa na nchi hizo, nchi za Afrika zimetoa matakwa yao ya marekebisho.
Ingawa mswada huo umekutana na matatizo, lakini juhudi za kutetea haki za watu wa jamii za kiasili hazifai kuachwa. Mwezi Desemba mwaka 2005, baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha "Programu ya pili ya utekelezaji wa miaka kumi ya kimataifa ya watu wa ajamii za kiasili", na kauli mbiu ya "miaka kumi" ya pili ni "kushikamana katika kulinda heshima". Bw. Ban Ki-moon kwenye taarifa yake ya maandishi aliitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua halisi kwa mujibu wa kauli mbiu hiyo ili kuhakikisha haki za watu wa jamii za kiasili duniani zinalindwa. Pamoja na hayo ofisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu Bw. Luise Arbour na mtoa ripoti kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa watu wa jamii za kimataifa Bw. Rodolfo Stavenhagen, walitoa taarifa ya pamoja, wakitaka mswada wa "taarifa ya haki za watu wa jamii za kiasili" upitishwe mapema iwezekanavyo katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
|