Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-13 16:00:34    
Mpiga piano msichana Li Ang

cri

Mpiga piano msichana Li Ang ana umri wa miaka 22, siku za karibuni kwa mara ya kwanza alifanya maonesho ya muziki wa piano mjini Beijing.

Msichana Li Ang alianza kujifunza kupiga piano katika nchi za nje tokea alipokuwa na umri wa miaka kumi na alishiriki kwenye maonesho ya muziki mara nyingi. Baada ya kuufahamu muziki wa Magharibi alianza kuwajulisha wasikilizaji wa nchi za Magharibi muziki wa Kichina.

Mnaosikia ni muziki alioupiga katika maonesho aliyofanya mjini Beijing. Kutokana na kupiga piano kwa nguvu, hata alipopewa shada la maua mkono wake wa kulia alishindwa kushika shada hilo. Baada ya maonesho kumalizika, wasikilizaji ambao walikuwa bado hawajatoka kutoka furaha yao, walimsifu sana na bila kuficha walitoa mapendekezo yao.

"Alipiga vizuri kweli kwa ufundi wake na kuonesha jinsi anavyoufahamu muziki wenyewe, lakini kutokana na umri wake mdogo, tena yeye ni msichana, nguvu mara nyingine inaonekana haitoshi. Lakini kwa ufupi, ni mpiga piano hodari."

Baba wa msichana Li Ang ni mhandisi na mama yake ni daktari, wote wanapenda sana muziki. Li Ang alieleza kuwa alipokuwa mdogo sauti aliyosikia mara nyingi ilikuwa ni vicheko na nyimbo. Wazazi wake wanapenda kuimba na yeye alipiga piano ingawa alikuwa hawezi kupiga vizuri. Alisema,

"Nilianza kupiga piano ndogo nilipokuwa na umri wa mwaka mmoja, na baba na mama waliimba pamoja. Nilipokuwa na umri wa miaka minne nilianza kujifunza kupiga piano shuleni."

Mwanzoni alifundishwa namna ya kutumia vidole na kupiga muziki wa mazoezi, alipokuwa na umri wa miaka sita kwa mara ya kwanza alipiga muziki jukwaani. Maonesho yake hayo yaliwafanya wazazi wake waamini kuwa binti yao ana kipaji cha muziki. Alipokuwa mwanafunzi katika shule ya msingi kila siku alitumia muda wa saa tatu kufanya mazoezi ya kupiga piano, wakati huo alijiwekea msingi imara wa kupiga piano.

Nchini China si rahisi hata kidogo kama wazazi wakiamua kuwasaidia watoto wao kujifunza kupiga piano, licha ya uwezo wa kifedha pia wanatakiwa kutumia muda mwingi kuwa pamoja na watoto wao wanapofundishwa na hata inawapasa waache kazi zao. Mpiga piano mwingine kijana wa China Lang Lang ambaye amekuwa mashuhuri duniani alipokuwa na umri wa miaka tisa alikuja Beijing, wazazi wake walimfuata ili kumtunza, walihama maskani yao na kuja kuishi Beijing kwa miaka mingi. Ili kumsaidia Li Ang, mama yake pia alifanya hivyo, kwamba Li Ang alipokuwa na umri wa miaka kumi wazazi wake waliamua kumpeleka binti yao nchini Marekani kujifunza kupiga piano, mama yake aliacha kazi ya udaktari na kuishi naye Marekani kwa miaka zaidi ya kumi.

Mwanzoni alipokuwa nchini Marekani alikuwa na tatizo la lugha, tofauti ya kimaisha, na njia tofauti ya kufundisha, lakini yote hayo hayakutikisa nia yake. Alisema uchaguzi wa kupiga piano unamaanisha kukabiliwa na shida nyingi. Alisema,

"Njia ya muziki ni ngumu, lakini ina maana. Kwangu mimi furaha yangu yote iko kwenye piano, siwezi kufikiri maisha yangu yatakuwaje nisipokuwa na piano. Shida ni nyingi lakini nitazivuka, kila siku napiga, kama siku fulani sikupiga piano basi naona kama nimekosa kitu fulani."

Alipokuwa na umri wa miaka 13 alifanya maonesho ya muziki kwa kushirikiana na kundi la simfoni mjini New York. Waandishi wa habari walikuwa wameanza kumfuatilia. Kuanzia mwaka 2003 Redio ya Canada CBC ilianza kupiga muziki aliopiga na kuwafahamisha wasikilizaji msichana huyo asiye wa kawaida kutoka Mashariki. Aliwahi kuwa msaidizi wa mpiga piano mkubwa Leon Fleisher katika mafunzo ya piano, alipata shahada ya pili katika chuo cha muziki cha Juilliard na sasa anaendelea na masomo ili apate shahada ya juu zaidi.

Nchini China watoto wanapofundishwa kupiga piano licha ya kuelekezwa na walimu wao, wazazi pia wanakuwa karibu nao ili kuwasaidia. Lakini nchini Marekani, walimu huwaacha wanafunzi wajifunze wenyewe na kuwalea wawe na hisia zao kuhusu muziki na kuwahamasisha wajitokeze jukwaani kufanya maonesho. Njia hiyo ilimwezesha Li Ang kugundua sifa zake na dosari zake, na alipata nafasi nyingi za kufanya maonesho. Li Ang anaona hayo ni mafanikio makubwa aliyopata alipokuwa nchini Marekani. Alisema,

"Nilipokuwa na umri wa miaka 15 hivi nilianza kufanya maonesho yangu na uzoefu wangu ulikuwa umeanza kuwa mkubwa kila baada ya maonesho. Kutokana na kuhamasishwa na wenzangu nilishiriki kwenye maonesho mengi ya muziki yakiwa pamoja na maonesho ya kibiashara. Kwa kushiriki kwenye maonesho mengi, sasa nimezama kabisa katika muziki wa piano."

Hivi sasa Wachina wanaokwenda Marekani kujifunza kupiga piano wanaongezeka, na wengi wao wanajulikana katika nyanja ya muziki duniani. Wanapojifunza kupiga muziki wa Kimagharibi pia wanajaribu kupiga muziki wa kale wa China kwa piano. Hali kadhalika Li Ang alifanya vivyo hivyo. Kwenye maonesho ya muziki wake nchini Marekani alipiga nyimbo mbili za China, mmoja unaitwa "Wimbo wa Mapenzi ya Kangding" na mwingine "Mto wa Liu Yanghe". Nyimbo hizo mbili huwa zinapigwa kwa ala za Kichina, kupiga nyimbo hizo kwa piano ni jaribio la kijasiri. Alisema,

"Nazipenda sana nyimbo hizi mbili, hata nilipokuwa mtoto nilikuwa nazisikiliza mara kwa mara. Nyimbo hizo zinafaa sana kupigwa kwa piano. Nitajitahidi kupiga zaidi muziki wa China kwa piano na kuwajulisha na kuwafurahisha wasikilizaji wa nchi za nje."

Hivi sasa, licha ya kufanya mazoezi ya kupiga piano kwa muda wa saa tatu, anapokuwa na wakati anapenda kutazama sinema na kuogelea. Kwa sasa anafanya maonesho mengi zaidi katika nchi za Amerika ya Kaskazini, na kila mwaka anafanya maonesho mara thelathini hivi. Jina lake linajulikana miongoni mwa wanamuziki, na ataanza maisha ya kuwa mpiga piano rasmi baada ya kuhitimu masomo yake.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-13