Gazeti la The Sunday Times la Uingereza tarehe 12 lilichapisha matokeo ya uchunguzi wa maoni ya raia uliofanyika hivi karibuni yakionesha kuwa, uungaji mkono wa raia kwa chama cha Leba kinachoongozwa na waziri mkuu Gordon Brown umefikia asilimia 42 na umezidi kwa asilimia 10 kuliko ule wa chama kikubwa cha upinzani cha wahafidhina, kiwango hiki kimefikia kile cha kabla ya vita vya Iraq.
Matokeo hayo yamepatikana katika uchunguzi uliofanywa na Shirika la uchunguzi wa kiraia la YouGov ambalo ni Shirika maarufu sana. Mwezi Novemba mwaka 2002, chama cha Leba kilichokuwa kinaongozwa na Tony Blair kilipata matokeo hayo mazuri, lakini baadaye Blair aliamua kushiriki kwenye vita vilivyoanzishwa na Marekani dhidi ya Iraq, uamuzi wake ulilaumiwa vikali na wananchi wa Uingereza, ambapo uungaji mkono wa raia kwa chama cha Leba ukabwagwa chini, tena ulikuwa uko chini kwa miaka kadhaa mfululizo. Ilipofika mwezi Juni mwaka huu kabla ya Blair kujiuzulu, uungaji mkono wa raia kwa chama cha Leba ulikuwa wa asilimia 28 tu, hii ni upungufu wa asilimia 9 kuliko ule wa chama cha wahafidhina.
Tarehe 27 Juni Brown alishika wadhifa wa waziri mkuu badala ya Blair, baadaye uungaji mkono wa raia kwa chama cha Leba umekuwa ukifufuka siku hadi siku. Wachambuzi wanaona kuwa, matokeo hayo yanahusiana na juhudi alizofanya Bw Brown katika muda wa mwezi mmoja na nusu uliopita tangu ashike madaraka.
Kutokana na inavyojulikana, Bwana Brown aliposhika wadhifa ndipo Uingereza ilipokabiliwa na matukio mbalimbali. Mwishoni mwa mwezi Juni, jaribio la mashambulizi ya ugaidi lilitokea huko London na Glasgow, hata tahadhari kote nchini Uingereza iliongezeka na kuwa kwenye ngazi ya juu kabisa ya "hali ya hatari". Katika mtihani huo mkali wa mara ya kwanza kwa serikali ya Brown, Bwana Brown kwa upande mmoja aliwakumbusha raia kwamba, Uingereza inakabiliwa na tishio kubwa la ugaidi linalotokea kwa mfululizo, na kwa upande mwingine kutokana na hali ya kujipenyeza kwa magaidi kwenye hospitali za Uingereza, Bwana Brown alizitaka hospitali zote za matibabu na utunzaji wa afya zithibitishe upya utaratibu wa kazi zao za ajira, na kufanya uchunguzi mkali zaidi kuhusu hali ya waajiriwa wao kutoka kwenye wahamiaji wenye uwezo mkubwa. Kutokana na maendeleo ya haraka ya kugunduliwa kwa hali halisi ya matukio, hali ya nchini Uingereza ilitulizwa kwa haraka, Bwana Brown alipata mafanikio katika mtihani wake wa kwanza.
Lakini matata mengine yalitokea baadaye kwa mfululizo. Baada ya kuingia mwezi Julai, sehemu kubwa ya Uingereza ilikumbwa na mafuriko makubwa ambayo hayakutokea katika miaka 60 iliyopita, hata baadhi ya sehemu, maji na umeme vilikatika, raia walipata hasara kubwa za mali. Bwana Brown alifanya ukaguzi mara mbili katika sehemu zilizokumbwa na maafa makubwa, na kujikosoa kwa wakazi wa sehemu zilizokumbwa na kukatika kwa maji na umeme, tena aliahidi kuwa serikali itajikosoa kutokana na matatizo yaliyoonekana katika maafa hayo ya mafuriko, ili matukio kama hayo yasitokee tena katika siku za baadaye. Na ilipofika mwanzoni mwa mwezi Agosti, ambapo mafuriko makubwa yalikuwa bado hayajaondoka kabisa, tukio la ugonjwa wa midomo na kwato lilitokea katika Jimbo la Surrey, Uingereza. Bwana Brown alirudi London kabla ya kumalizika kwa likizo yake ili kushughulikia tukio hilo.
Bwana Brown siyo mwanasiasa nyota. Kwa mara ya kwanza alipohudhuria Mkutano wa "maswali na majibu" kwenye bunge, kwa muda fulani, alikumbwa na kigugumizi chini ya shutuma kali kutoka kwa chama cha upinzani, hata mamia na maelfu ya watazamaji wa televisheni walikuwa na wasiwasi juu yake. Lakini kila anapokumbwa na "utatanishi", Bwana Brown alitumia mbinu zake kuufanya utatanishi huo uwe fursa ya kuweza kumwongezea sifa. Hasa katika kukabiliana na matukio ya dharura, Brown mwenye utulivu na ukali na anayefuata hali halisi hakuwafanya waingereza watie mashaka juu ya uwezo wake wa uongozi, na vyombo vya habari pia vilimsifu siku hadi siku.
Katika hali hiyo, watu wengi wanamshauri Brown aitishe uchaguzi mkuu kabla ya mpango uliowekwa, ili kuongeza nafasi za kupata ushindi.
|