Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-14 14:06:05    
Mji wa Penglai wafanya juhudi ili uwe mji maarufu wa kutengeneza mvinyo nchini China

cri

Watu wanapozungumzia mvinyo hukumbuka mji wa Porto nchini Ureno ambao ni mji maarufu wa utengenezaji wa mvinyo. Mji wa Penglai ulioko mkoani Shandong ni mji maarufu wa kutengeneza mvinyo nchini China. Kutokana na hali nzuri ya kimaumbile, mji huo umekuwa mmoja kati ya miji inayotengeneza mvinyo kwa wingi nchini China.

Mji wa Penglai uko kwenye latitudo 37.5 kaskazini, unatazamana na bahari za Huanghai na Bohai. Kutokana na hali ya unyevunyevu, ardhi yenye rutuba na mwangaza wa kutosha wa jua?sehemu hiyo ina hali nzuri ya kupanda mizabibu kwa ajili ya utengenezaji wa mvinyo. Naibu meya wa mji wa Penglai Bw. Mu Qinghe alisema hivi sasa mji huo una hekta elfu 47za mashamba ya mizabibu, na unatengeneza tani elfu 80 za mvinyo kwa mwaka. Bw. Mu alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, mji wa Ponglai uliendeleza eneo la kilimo cha mizabibu, na utengenzaji wa mvinyo pamoja na shughuli za utalii kwenye mashamba ya mizabibu, umejenga njia ya mizabibu yenye urefu wa kilomita 18 kwa ajili ya utalii, na hekta elfu 8 za mashamba ya mizabibu ya aina nzuri."

Mizabibu mingi mjini Penglai ilipandwa katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, hivi sasa imeingia kipindi kizuri cha uzalishaji wa zabibu. Katika miaka ya hivi karibuni, mji huo uliingiza mizabibu ya aina nyingi nzuri kutoka nchi za nje, na kukuza mizabibu ya aina nzuri zaidi kwenye msingi huo."

Bw. Yang Fengguang ni mtaalamu hodari wa kilimo ambaye amepanda matunda kwa zaidi ya miaka 40. Alisema kupanda mizabibu ya aina nzuri ni msingi wa kutengeneza mvinyo wenye sifa nzuri. Hali nzuri ya kimaumbile na teknolojia ya kisasa ya upandaji wa mizabibu imeusaidia mji wa Penglai kutengeneza mvinyo wenye sifa ya kipekee. Alisema,

"Mvinyo una ladha ya zabibu. Sifa ya mvinyo inategemea sifa ya zabibu kwa kiasi kikubwa, hivyo ukitaka kutengeneza mvinyo mzuri, ni lazima upande mizabibu wewe mwenyewe."

Ili kuendeleza utengenezaji mkubwa na wa kisasa wa mvinyo, mji wa Penglai umeanzisha eneo la vielelezo vya kilimo vya mizabibu. Mwaka 2002 idara husika ya mji huo ilitunga vigezo viwili kuhusu teknolojia ya upandaji wa mizabibu na mizabibu ya utengenezaji wa mvinyo isiyo na uchafuzi.

Mwandishi wetu wa habari alikutana na Bw. Fu Xianbin ambaye alikuwa anafanya kazi mashambani. Bw. Fu alisema ana mashamba ya mizabibu hekta 1, hivi sasa mashamba hayo yamekodishwa kwa kampuni ya utengenezaji wa mvinyo kwa Yuan elfu 7 kwa mwaka. Anashughulikia upandaji wa mizabibu tu, na kampuni inampatia mimea, dawa za kemikali, mbolea na vifaa vya umwagiliaji maji.

Bw. Fu alisema licha ya mapato ya kukodisha mashamba, kila mwaka anaweza kupata Yuan elfu 12 kwa kuuza zabibu. Mapato yameongezeka kwa mara moja kuliko zamani. Alisema,

"Zamani nilipanda mizabibu kwa kutumia mbinu za kizamani, nilizingatia zaidi kiasi cha mavuno, lakini hivi sasa nazingatia zaidi sifa ya zabibu."

Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na kupanda kwa bei ya zabibu, wakulima wengi walipanda mizabibu bila ya mpango, na uzalishaji uliongezeka kwa kiasi kikubwa. Lakini zabibu zilizozalishwa hazikuweza kufikia kigezo cha kutengeneza mvinyo wenye sifa nzuri. Bei ya mizabibu ilipungua kuwa Yuan 0.1 kutoka Yuan 2 kwa kilo, wakulima wengi walipata hasara kubwa.

Hivi sasa wakulima hawazalishi mizabibu bila ya mpango tena. Makampuni mengi maarufu yakiwemo kampuni ya Zhangyu ya mji wa Yantai, kampuni ya biashara ya chakula na mafuta ya China COFCO na kampuni ya Xintian yalianzisha vituo vya kuzalisha mizabibu na utengenezaji wa mvinyo mjini Penglai. Makampuni yanasaini mikataba na wakulima, yakinunua zabibu kwa mujibu wa mikataba, na kutuma wataalamu kuwafundisha wakulima namna ya kupanda mizabibu.

Hivi sasa mji wa Penglai umeanzisha idara ya kwanza ya utafiti wa utengenezaji wa mvinyo nchini China. Serikali inafanya juhudi kuyahimiza makampuni ya mvinyo yatengeneze mvinyo wa kiwango cha juu. Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2010, mji huo utakuwa na hekta laki 1.7 za mashamba ya mizabibu yenye sifa nzuri, na utatengeneza mvinyo wa kiwango cha juu wenye uzito wa tani laki 2.5.

Mvinyo ni bidhaa inayoweza kuonesha utamaduni mkubwa. Kuendeleza utalii unaohusika na mvinyo ni lengo muhimu kwa sehemu zinazotengeneza mvinyo kwa wingi duniani. Licha ya njia ya utalii wa mizabibu yenye urefu wa kilomita 18, mji wa Penglai pia umejenga bustani za mizabibu na kituo cha maonesho ya mvinyo. Bustani ya mizabibu ya Nanwangshangu ya kampuni ya COFCO itafunguliwa kwa watalii mwezi Oktoba mwaka huu. Katika bustani hiyo kuna mashamba makubwa ya mizabibu, vyumba vya kuhifadhia mvinyo chini ya ardhi, vyumba vya mafundi wa kuonja mvinyo, klabu ya utamaduni na mvinyo na maduka ya mvinyo. Mfanyakazi wa bustani hiyo Bi. Si Yuan yuan alisema,

"Katika bustani hiyo watalii wataweza kuchuma zabibu wao wenyewe, na kutengeneza mvinyo wakielekezwa na wafundi wa kutengeneza mvinyo. Hata wanaruhusiwa kukodi sehemu ya kuhifadhi mvinyo ili wakati wanapofanya sherehe ya siku za kuzaliwa kwao waanweza kwenda bustani hiyo na kuchukua mvinyo walizohifadhi ili kuonja pamoja na marafiki zao.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-14