Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-17 14:49:56    
Hatua mbalimbali ilizoahidi China zainufaisha Afrika ya Kusini

cri
Mwandishi wetu wa habari hivi karibuni alifahamishwa kuwa, hatua nane ilizoahidi China kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Novemba mwaka 2006 hapa Beijing zinatekelezwa kwa utaratibu, utekelezaji wa hatua kadhaa umezinufaisha kidhahiri sekta mbalimbali nchini Afrika ya Kusini.

Tarehe 3 mwezi Novemba mwaka 2006, kampuni ya chuma na chuma cha pua ya China na kampuni ya Samancor Chrome ya Afrika ya Kusini zilisaini rasmi makubaliano kuhusu kuanzisha kampuni ya ubia?tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2006 kampuni hizo mbili na benki ya maendeleo ya taifa zilisaini makubaliano ya mfumo wa ushirikiano kati ya pande hizo tatu.

Kutokana na makubaliano hayo, kampuni ya chuma na chuma cha pua ya China ilitoa dola za kimarekani milioni 200 kununua asilimia 50% ya hisa za mgodi wa Chromium wa kampuni ya Samancor Chrome ya Afrika ya Kusini na viwanda vya uyeyushaji wa chuma cha chromium, na kuanzisha pamoja kampuni ya ubia. Kiasi cha uzalishaji wa chuma cha chromium kwa kampuni hiyo kinafikia tani laki 2.8 kwa mwaka.

Meneja mkuu wa kampuni hiyo ya ubia Bw. Nan Fengzhi alieleza kuwa, tarehe 13 mwezi Juni mwaka huu meli ya kwanza ya iliyobeba shehena za chuma cha chromium kilichozalishwa na kampuni hiyo ilifika nchini China na kuuza bidhaa zake. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni kampuni hiyo ilizalisha tani elfu 43 za chuma cha chromium, kati ya hizo tani elfu 32 zilisafirishwa kuja China.

Balozi wa China nchini Afrika ya Kusini Bw. Zhong Jianhua alisema mradi huo wa ushirikiano kati ya kampuni ya chuma na chuma cha pua ya China na kampuni ya Samancor Chrome ni mfano wa mradi wa kunufaishana, ambao unafuata moyo wa mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing. Ushirikiano huo unaweza kuboresha hali ya upungufu wa maliasili ya chromium nchini China, pia unaweza kukidhi mahitaji ya soko la maliasili kwa nchi za nje. Kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa uzalishaji wa kampuni hiyo, kampuni hiyo hakika itaongeza nafasi nyingi za ajira, na kuhimiza zaidi maendeleo ya sekta husika za Afrika ya Kusini.

Tarehe 4 mwezi Aprili mwaka huu, China na Afrika ya Kusini zilisaini makubaliano manane yenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani milioni 143. Kutokana na makubaliano hayo, China itaagiza mvinyo, sufu na shaba kutoka kwa Afrika ya Kusini.

Afrika ya Kusini ni nchi kubwa inayozalisha mvinyo, na mvinyo wake tayari unauzwa kwenye soko nchini China kuanzia mwaka 2004. Ikilinganishwa na mvinyo wa nchi nyingine, mvinyo wa Afrika ya Kusini una umuhimu wa kuwa na bei nafuu na sifa nzuri. Lakini kutokana na ziada kubwa ya bidhaa duniani, kupungua kwa uuzaji wa bidhaa nje na matumizi ya nchini, wafanyabiashara wanaozalisha mvinyo nchini Afrika ya Kusini wanakabiliwa na changamoto ya kushushwa kwa bei ya mvinyo. Naibu balozi wa China nchini Afrika ya Kusini anayeshughulikia mambo ya uchumi na biashara Bw. Ling Guiru alisema, China iliamua kuagiza mazao ya kilimo kutoka kwa Afrika ya Kusini katika wakati huo, hii inaonesha nia ya serikali ya China kuhusu kufanya juhudi za kutekeleza maoni ya pamoja yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing.

Bw. Ling Guiru alisema katika hatua nane ilizoahidi China kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing, kuna hatua nne zinazohusiana na Afrika ya Kusini. China itatoa Yuan milioni 20 katika kuandaa watu wenye ujuzi, hivi sasa pande hizo mbili zinajadili mpango halisi, na mpango huo utatekelezwa mwaka huu. China itaisaidia Afrika ya Kusini kujenga kituo cha mafunzo ya ufundi wa kazi, hivi sasa pande hizo mbili zinajadili mambo husika ya mradi huo. China pia itaisadia Afrika ya Kusini kujenga kituo cha ushirikiano wa ufundi wa kilimo, hivi sasa kikundi cha wataalamu wa kilimo wa China kinafanya ziara ya ukaguzi nchini Afrika ya Kusini, na kuthibitisha kwanza kuanzisha kituo cha mafunzo ya ufundi wa kufuga samaki. Mwezi Februari mwaka huu, China ilitoa msaada wa fedha kwa kituo cha mali ya urithi cha Afrika na chuo kikuu cha Pretoria.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Afrika ya Kusini alipozungumzia ushirikiano kati ya China na Afrika ya Kusini, alisema ikiwa nchi yenye usitawi wa kiuchumi barani Afrika, Afrika ya Kusini bado ina nguvu kubwa ya maendeleo. Afrika ya Kusini inataka kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na China katika sekta za uchumi, biashara, na uwekezaji kwenye nchi hizo mbili, kufanya mawasiliano katika sekta za sayansi na teknolojia na kuandaa watu wenye ujuzi, na kuongeza uwezo wa ushindani. Alisema Afrika ya Kusini inataka kujifunza uzoefu wa China kuhusu namna ya kutatua suala la umaskini wakati wa kufanya mageuzi ya kiuchumi.

********************************

Habari nyingine zinasema waziri wa kilimo wa Kenya Bw. Kipruto Rono Arap Kirwa Hivi karibuni alisema, China na Kenya zina fursa nyingi za ushirikiano katika sekta ya kilimo. Bw. Kirwa alisema kilimo ni sekta muhimu ya uchumi wa Kenya, lakini maendeleo yake bado yako nyuma. Hivi sasa uzalishaji wa mazao ya kilimo wa Kenya unategemea zaidi uzalishaji wa wakulima wa familia moja moja, na uwezo wake wa kutengeneza zaidi mazao ya kilimo bado ni mdogo, hivyo mazao ya kilimo ya hatua ya mwanzo ni mazao muhimu ya Kenya yanayouzwa nchi za nje. Hii imesababisha mazao ya Kenya kutokuwa na nguvu ya ushindani katika soko la dunia.

Bw. Kirwa alisema kama Kenya ikitaka kubadilisha hali ya kilimo, serikali inapaswa kuchukua hatua ili kuongeza nguvu ya uzalishaji, kuimarisha uhusiano kati ya kilimo na sekta za utalii, utengenezaji wa vyakula na vinywaji, na nishati ya viumbe, na kuongeza nguvu ya ushindani ya mazao.

Bw. Kirwa alisema China na Kenya zinafanya ushirikiano wenye ufanisi katika sekta ya kilimo, na China imewaandaa wataalamu wengi wa kilimo kwa Kenya. Alisema Kenya na China zote ni nchi wanachama wa WTO, na mustakabali wa ushirikiano kati yao katika biashara ya kilimo ni mzuri. Alisema Kenya ina mazingira mazuri yanayonufaisha maendeleo ya wawekezaji wa nchi za nje, pia Kenya inapenda kufanya ushirikiano na China, kuuza kahawa, chai, maua na mazao mengine kwa China.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-17