Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-14 16:49:27    
Barua 0814

cri

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la posta 504 Lindi Tanzania ametuletea barua akisema, anapenda kujua hali zetu za hivi karibuni na anatumai kuwa sote hatujambo na tunaendelea na kazi za kila siku za kuwaletea matangazo wasikilizaji. Yeye mwenyewe anasema anasikitika kwa kuwa, ni muda mrefu sasa hajaweza kushirikiana na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kutokana na mabadiliko makubwa kati ya Zanzibar na hapo Lindi, muda wa siku hata wiki mbili tatu, na anakuwa katika vijiji kushughulika na biashara na kufuatilia mambo mbalimbali. Lakini hata hivyo bado anakuwa pamoja nasi, na anashukuru kwa zawadi tulizomtumia pamoja na gazeti la China pictorial. Anasema hajatupa kalamu chini na wala hajaziba masikio yake, ataendelea kuwasiliana nasi kama kawaida yake kila apatapo muda atakuwa anaandika na kutoa maoni. Vilevile anapenda kutumia fursa hii kuwafikishia salamu wasikilizaji wenzake wanaotumia salamu.

Tunamshukuru Gulam Haji Karim kwa barua yake, ingawa ni siku nyingi hatukupata barua zake, lakini tunaelewa kuwa wasikilizaji wetu wengi kama yeye wakiwemo Kilulu Kulwa, Kaziro Dutwa, Epaphara Deteba na wengineo ambao walianza kusikiliza matangazo yetu tangu zamani sana wanatufuatilia hata wakati wanapokuwa na shughuli mbalimbali. Urafiki ulioanzia kwa miaka mingi kati yetu unaendelea kuwepo, na kila mara wasikilizaji wetu wanaweza kutuandikia barua kueleza ufuatiliaji wao, kweli tunawashukuru sana.

Msikilizaji wetu Asha S. Iddy wa Jamhuri sekondari school sanduku la posta 1653 Dodoma Tanzania ametuletea barua akisema, anatumai kuwa sisi ni wazima wa afya na tunaendelea vizuri na shughuli za kila siku. Anatushukuru kwa kumtumia majibu na upendo tunaomuonesha. Anasema yeye alianza kusikiliza Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa mwaka 2005 huko mjini Dar es Salaam, lakini aliporejea nyumbani Dodoma alikuwa anaipata matangazo yetu mara chache mno, na kwa sasa bado haisikiki vizuri. Na pia wakati mwingine hajui ni masafa gani matangazo yetu yanapatikana. Anapenda sana kusikiliza idhaa hii ya Kiswahili, lakini kwa sasa kikwazo kikubwa kwake ni matangazo kutokuwa na usikivu mzuri.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Asha S. Iddy kwa barua yake inayotueleza kuhusu upendo wake kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, na kutuelezea hali kuhusu usikivu wa matangazo yetu kwa sehemu aliko. Ni kweli, tunafahamu kuwa matangazo yetu hayasikiki vizuri katika sehemu kadha wa kadha, idara husika za Radio China kimataifa zinafanya juhudi kuyatatua matatizo fulani fulani. Mpaka sasa hatuna la kufanya ila tu kuwaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie, mpaka tutakapoweza kurekebisha hali hii.

Msikilizaji wetu mwingine ni Bw. Mutanda Ayub Shariff wa sanduku la Posta 172 Bungoma nchini Kenya. Yeye ameanza barua yake kwa salamu kwa wafanyakazi wa Radio China Kimataifa na anatumai kuwa wote tu wazima na tunaendelea kuchapa kazi kama kawaida. Anasema pamoja na kuwa katika shughuli zake sehemu mbali mbali hajawahi kukosa hata siku moja kuwaza jinsi ya kufanya ili matangazo ya Radio China Kimataifa yang'are duniani kote.

Anafurahi kwa sasa anavyoendelea kutusikia katika mawimbi ya FM 91.9 na anatarajia kuendelea kupata habari nzuri zaidi kupitia mawimbi hayo, anasema ila tu usikivu wa matangazo katika mkoa wa magharibi Bungoma unakuwa wa shida. Anasema pamoja na yote hayo upendo alioonao kwa Radio China Kimataifa umemfanya ajitolee sana na kuweka maslahi yake kando na kuwa na upendo kwa Radio China kimataifa. Wakati wa kipindi cha mwisho yaani kuanzia saa mbili hadi saa tatu usiku, mpangilio wa vipindi unampa nguvu na furaha, kwani ni vizuri sana na wakati mwingine kipindi cha salamu zenu kinawekwa mwisho.

Kuhusu burudani ya muziki anasema ni jambo nzuri iwapo kama itawezekana nyimbo ziwe za mchanganyiko wa kiafrika na kichina. Mapendekezo yake kwa Radio China Kimataifa kwa sasa ni kuajiriwa wahariri wengi na Afisa uhusiano ambaye atashughulikia uhusiano kati ya wasikilizaji na wafanyakazi wa Radio China Kimataifa. Pia naona kwa sasa mawasiliano yameimarika sana japokuwa shida ipo katika jarida la urafiki kwani toka mwaka jana mpaka sasa bado halijatoka. Anamaliza barua yake kwa kusema kuwa juhudi zake za kutaka kukutana na mhariri wa Nairobi ili aweze kutoa maoni na mapendekezo yake bado hazijafanikiwa, lakini ataendelea.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharif kwa mapendekezo aliyotoa kuhusu matangazo yetu. Tunafurahia kama anafurahishwa na matangazo yetu, kwani hilo ndio lengo letu hasa. Na kuhusu suala la Ofisa anayeshughulikia uhusiano kati yetu na wasikilizaji wetu, yupo na anafanya kazi kwa bidii kila siku akishughulikia barua pepe, barua, kutuma majarida na zawadi mbalimbali pamoja na kadi za salamu kwa wasikilizaji wetu, kwa hiyo usiwe na hofu na hilo

Idhaa ya kiswahili 2007-08-14