Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-14 19:38:14    
Rais Hu Jintao aanza ziara yake ya Asia ya Kati

cri

Rais Hu Jintao wa China tarehe 14 Agosti ameanza ziara katika sehemu ya Asia ya Kati. Katika ziara hiyo ya siku 5, rais Hu Jintao atafanya ziara rasmi nchini Kyrgyzstan, ambapo atahudhuria mkutano wa wakuu wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai, pia atatizama luteka ya jumuiya hiyo inayolenga kupambana na ugaidi na kufanya ziara rasmi nchini Kazakhstan.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Hu Jintao wa China kuizuru Kyrgyzstan, ambapo atafanya mazungumzo na rais Kurmanbek Bakiyev wa nchi hiyo, na nchi hizo mbili zitasaini nyaraka mbalimbali zinazohusu ushirikiano katika maeneo ya siasa, uchumi na biashara, kilimo na elimu.

Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Hui alipohojiwa na Radio China Kimataifa, alisema  "Ziara hiyo inakuja wakati China na Kyrgyzstan zinaadhimisha miaka 15 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi, na miaka mitano tangu zisaini mkataba wa ujirani mwema, urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Ziara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukuza uhusiano kati ya China na Kyrgyzstan, na hakika itaweza kuongeza uaminifu wa kisiasa, kuendeleza ushirikiano wa kunufaishana, kuimarisha ushirikiano katika mambo ya usalama na kupanua ushirikiano katika mambo ya utamaduni kati ya nchi hizo mbili."

Wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai watakuwa na mkutano tarehe 16 Agosti, huko Bishkek mji mkuu wa Kyrgyzstan. Vile vile marais kutoka Mongolia na Iran, mawaziri wa mambo ya nje kutoka Pakistan na India wamealikwa kuhudhuria mkutano huo, nchi ambazo zinasubiri kujiunga na jumuiya hiyo. Wageni rasmi wengine wa mkutano huo ni pamoja na marais wa Afghanistan na Turkmenistan, na naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Lynn Pascoe.

Wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai wanatazamiwa kusaini mkataba wa kudumisha ujirani mwema na urafiki kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Hii itakuwa ni hatua kubwa inayolenga kuhakikisha kuwepo kwa amani katika kanda hiyo, ambapo mtizamo kuhusu kudumisha urafiki na amani kizazi baada ya kizazi, utawekwa bayana kwenye mkataba huo wenye nguvu ya kisheria.

Hapo baadaye rais Hu Jintao wa China na wakuu wa nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai watakwenda Chelyabinsk, nchini Russia kutizama luteka inayolenga kupambana na ugaidi, ambayo ni ya kwanza kushirikisha nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo. Kuhusu luteka hiyo msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Hui alisema

"Nchi 6 wanachama zinatumai kuongeza maingiliano na ushirikiano katika mambo ya ulinzi na usalama kwenye luteka hiyo, kuongeza uwezo wa kupambana na ugaidi, na kukabiliana na tishio na changamoto mpya kwa pamoja, ili kufanya kazi kubwa zaidi katika kulinda amani, usalama na utulivu wa kikanda. Luteka hiyo hailengi nchi wala jumuiya yoyote, inalingana na kanuni za jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai kuhusu kutofungamana na upande wowote, kutochochea hali ya kupingana, na kutolenga upande wa tatu."

Bw. Li Hui alisema ziara ya rais Hu Jintao nchini Kazakhstan pia itasaidia kukuza uhusiano kati ya China na Kazakhstan. Alidokeza kuwa katika ziara hiyo ya siku 5, rais Hu Jintao na rais Vladimir Putin wa Russia watakuwa na mazungumzo mara mbili. Na pande hizo mbili zinatarajia mazungumzo hayo yataweza kuongeza uaminifu wa kisiasa na ufanisi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Russia, na kuimarisha mawasiliano na uratibu kati yao katika mambo ya kikanda na kimataifa.