Tarehe 14 Agosti ilikuwa ni siku ya kutimia kwa mwaka mmoja tangu mgogoro kati ya Lebanon na Israel umalizike, lakini pande hizo mbili bado zinasumbuliwa na masuala yaliyobaki ya mgogoro huo. Rais Emile Lahoud wa Lebanon akizungumza katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu mgogoro kati ya Lebanon na Israel umalizike, aliwataka watu wa Lebanon wasisahau vitendo vya kikatili vya Israel vya kutumia silaha zilizopigwa marufuku duniani dhidi ya watu wa Lebanon. Alidhihirisha kuwa, chama cha Hezbollah ni kundi lenye nguvu linaloweza kuzuia njama ya nje, hivyo alitumai kuwa watu wote wa Lebanon watakilinda chama hicho.
Maneno aliyosema rais Lahoud yameonesha vya kutosha kuwa, bado kuna uhasama mkubwa kati ya Lebanon na Israel. Rais Lahoud aliwasifu watu wa Lebanon kwa kujitolea mhanga katika kulinda ukamilifu wa ardhi na mamlaka ya nchi yao katika vita dhidi ya Israel vya mwaka jana. Alisema ingawa Lebanon ni nchi ndogo, haina jeshi kubwa, lakini itapambana na kitendo chochote cha ukaliaji kutoka nje. Alisisitiza katika vita ya mwaka jana Israel ilidondosha mabomu mengi ya cluster nchini Lebanon, ambayo yameleta hasara kubwa na za muda mrefu kwa watu na uchumi wa nchi hiyo. Alisisitiza kuwa Israel haina haki ya kushambulia ardhi, amani na heshima ya waarabu bila kujali maazimio husika ya kimataifa.
Tarehe 12 mwezi Julai mwaka 2006, wanamgambo wa chama cha Hezbollah cha Lebanon waliingia katika sehemu ya mpakani ya kaskazini kwa Israel kushambulia jeshi la Israel lililokuwa likifanya doria, kuwaua askari watatu na kuwateka nyara askari wawili wengine. Baadaye Israel ililipiza kisasi kwa kuishambulia kwa mabomu sehemu ya kusini mwa Lebanon, na kuzusha mgogoro kati ya nchi hizo mbili. Tarehe 11 Agosti baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio No. 1701 kuzitaka nchi hizo mbili zisimamishe vita, tarehe 14 Agosti Lebanon na Israel zilitekeleza azimio hilo na kusimamisha vita. Mgogoro huo uliodumu kwa siku 34 ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100 nchini Lebanon, na wengine zaidi ya 3,200 kujeruhiwa.
Lakini hali ya kusini mwa Lebanon bado ni ya wasiwasi, karibu kila siku ndege za kivita za Israel zinaingia kwenye eneo la anga ya Lebanon. Tarehe 14 usiku mwezi huu kiongozi wa chama cha Hezbollah Bwana Sayyed Hassan Nasrallah aliionya Israel isianzshe tena vita mpya. Alisisitiza kuwa chama cha Hezbollah hakipendi vita, lakini kiko tayari wakati wowote kutekeleza majukumu yake ya kulinda nchi yake.
Mabomu ya ardhini na mabomu ya cluster yaliyozikwa na kudondoshwa na Israel katika sehemu ya kusini mwa Lebanon bado hayajaondolewa. Ofisa husika wa Lebanon Bi. Dalia Faran alisema, mabomu ya cluster yaliyoachwa na Israel nchini Lebanon yamesababisha vifo na majeruhi ya wakazi 204 wa Lebanon. Mabomu hayo pia yamesababisha vifo vya watu 10 na majeruhi ya watu 27 wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, jeshi la Lebanon na kikundi cha kuondoa mabomu hayo.
Katika mgogoro huo Israel pia ilipata hasara kubwa, na askari wawili waliotekwa nyara na chama cha Hezbollah hadi leo bado hawajulikani kama wako hai au la. Shughuli za magendo ya silaha zilizofanywa na wanamgambo wa Lebanon kupitia mpaka kati ya Lebanon na Syria zimeleta tishio kubwa kwa utekelezaji wa azimio No. 1701 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
|