Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-20 15:25:04    
Mlima Aersha-lulu ya kijani iliyoko kwenye milima ya Xinganling

cri

Mlima Aershan, ambao unasifiwa kuwa ni lulu ya kijani iliyoko kwenye sehemu ya mashariki ya mkoa huo, uko kwenye sehemu ya kati ya milima inayojulikana kwa jina la Xinganling yenye umbali wa zaidi ya kilomita 200. Sehemu yenye mandhari nzuri ya Mlima Aershan ni pamoja na bahari ya misitu, chemchemi ya maji moto, mlima wenye barafu na theluji, mbuga ya majani, mabaki ya volkano, mito na maziwa. Mwogoza watalii dada Chen Hongyuan alisema,

"Jina kamili la Mlima Aershan ni Halunaer, katika lugha ya Kimongolia, neno la 'halun' lina maana joto, na neno la 'aer' lina maana maji matakatifu, kwa hiyo Mlima Aershan haukujulikana kutokana na mlima, bali ni kutokana na maji cha chemchemi ya mlimani."

Sasa tunawafahamisha kuhusu chemchemi za huko, ambazo zilifanya Mlima Aershan uwe maarufu hapa nchini China. Chemchemi za Mlima Aershan ni nzuri sana, na ni nadra kuonekana hapa duniani, kuna jumla ya chemchemi 76 zilizoonekana nje kwenye maeneo manne. Katika kipindi cha jiolojia cha "zama za Mesozoic", matabaka ya ardhi yaliyopo kwenye sehemu ya Mlima Aershan yalikatikakatika, na maji yaliyoko chini ya ardhi yalipenya hadi kwenye nyufa za mawe chini ya ardhi kwa kupitia matabaka ya ardhi yaliyokatikakatika, baada ya kupashwa moto na joto la ardhini na kuchanganywa na madini yaliyonyeyuka ndani ya maji, hivyo maji ya chemchemi za Mlima Aershan ni yenye joto na yenye vitu vya madini ndani yake.

Kuna hadithi moja nzuri inayohusu chemchemi za Mlima Aershan. Zaidi ya karne kadhaa zilizopita, kulikuwa na mfalme mmoja aliyekuwa anasumbuliwa na magonjwa, siku moja alikuwa mgonjwa mahututi, wakati watu waliokuwa ndani ya jumba la mfalme walipokuwa wakijiandaa kwa ajili ya mazishi ya mfalme, mtawa mmoja mwenye elimu kubwa alifika kwenye jumba la mfalme, na aliwasihi waganga wa mfalme wampeleke mfalme kuoga kwenye maji moto ya chemchemi. Mfalme ambaye alikuwa amezirai, alipelekwa kwenye Mlima Aershan na kuogeshwa kwa kufuata agizo la yule mtawa, ilipofika siku ya 14 miujiza ilitokea, mfalme alipona kabisa. Kuanzia hapo wagonjwa wengi walikuwa wanakwenda kwenye Mlima Aershan, na kuoga kwa maji ya chemchemi.

Ingawa chemchemi zilizoko kwenye Mlima Aershan hazina uwezo mkubwa kama zilivyoelezwa katika hadithi hiyo, lakini maji ya chemchemi za Mlima Aershan baada ya kupimwa na idara husika, yalionekana kuwa ni maji yenye madini mengi ikiwemo shaba, manganese na strontium pamoja na madini yenye mionzi ya radium na uranium, ambayo yanamanufaa kwa afya ya watu, hususan kwa wagonjwa wa yabisi na wanaoumwa miguu na viuno kutokana na kujeruhiwa.

Jumba la makumbusho ya chemchemi la Mlima Aershan lina kundi kubwa la chemchemi. Jumba la makumbusho hilo lina eneo la zaidi ya mita za mraba 5,700 pamoja na chemchemi 37 za maji moto. Kwenye chemchemi yenye maji moto zaidi, mwongoza watalii Bw. Wang Bin alieleza kuhusu uwezo wa maji ya chemchemi, akisema,

"Maji ya chemchemi hiyo ni yenye ujoto mkubwa zaidi kati ya chemchemi 37 hizo, watu wenye ugonjwa wa yabisi au matatizo kwenye miguu wanaweza kukaa hapa kwa siku 21 au 22 kwa ajili ya matibabu."

Uwezo wa kipekee wa matibabu wa chemchemi za Mlima Aershan umewavutia watalii wengi wa nchini na hata wanaotoka nchi za nje. Bibi Katyusha kutoka Russia alisifu sana matokeo ya matibabu ya maji ya chemchemi za Mlima Aershan, akisema,

"Nilipata habari kuhusu chemchemi hizo kutoka idara ya utalii ya kampuni ya mafuta ya asili ya petroli ya Manzhouli, ni umbali wa zaidi ya kilomita 2,000 kufika hapa kutoka Russia, hii ni safari yangu ya tano kuja hapa kwenye Mlima Aershan, kwangu mimi, siyo tu kuwa kunywa maji ya chemchemi kunanisaidia, hata kukaa ndani ya bwawa lenye maji moto ya chemchemi kunatibu ugonjwa wangu. Baada ya kuambiana katika miaka mitatu iliyopita, sasa watu wa Russia waliofika hapa ni wengi zaidi kuliko wachina."

Wasikilizaji wapendwa, baada ya kuelezwa kuhusu chemchemi za maji moto, sasa tunawapeleka kwenye mabaki ya volkano kwenye Mlima Aershan. Kundi la volkano la Halaha la Mlima Aershan, ambalo ni moja ya makundi ya volkano maarufu nchini China, linapakana na kundi la volkano la Haerxingeer la nchi ya Mongolia. Ziwa la Tian, ambayo katika lugha ya China ni "ziwa la mbinguni", ni ziwa la volkano lililoko kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 1,300 kutoka usawa wa bahari. Maji ya ziwa hilo ni maangavu na ya rangi ya buluu kali, upepo mwororo ukivuma alama kama mawimbi inatokea juu ya maji, hiyo inawafanya watu wajione kama wako peponi. Mtalii kutoka mkoa wa Guangdong Bw. Liu Hao alisema,

"Ni ajabu sana, hapa panaonekana siyo sehemu ya duniani."

Mwongoza watalii dada Chen Hongyuan alisema, ziwa lilitokea kwenye mdomo wa volkano linaitwa pia kuwa ziwa Maer, kwa kawaida kina cha ziwa la volkano ni kutoka mita kadhaa hadi mita kumi kadhaa. Dada Chen Hongyuan alisema, maajabu kadhaa ya ziwa la Tian yanafanya jina la ziwa hilo la volkano lifahamike sana kwenye sehemu ya Mlima Aershan,

"Kwanza ni kina kisichojulikana cha ziwa la Tian, wataalamu walikuja kupima kina chake mwaka 2004, lakini hawakufanikiwa; Pili ni kuwa ingawa hakuna mfereji wa maji ya kuingia wala ya kutoka, lakini maji ya ziwa hilo hayapungui wala kuongezeka; tatu ni kuwa samaki wanaowekwa ndani ya ziwa la volkano hufa; la mwisho ni kuwa, ziwa la Tian liko kwenye kilele cha mlima, kama ukiangalia ziwa hilo kutoka kwenye ndege, linaonekana kama kito cha sappire kilichowekwa kwenye kilele cha mlima."

Baada ya kuangalia mabaki ya volkano, msikose kuangalia sura ya ardhi ya mawe yaliyoganda kutokana na maji ya mawe yaliyotoka ndani ya volkano. Milima Shitanglin iko karibu na ziwa la Tian, ambayo ni mawe yaliyoganda kutokana na maji ya mawe kutoka ndani ya volkano, baada ya kuliwa na maji ya mvua, upepo na jua ikawa na sura ya kipekee ya kimaumbile. Baadhi ya mawe yanaonekana kama upanga mrefu uliosimamishwa na kuelekezwa mbinguni, mengine ni kama askari shujaa walioshika mikuki mikononi, mawe mengine ni kama simba wanaokimbia kwa kasi na mengine ni kama wazee waliosimama mlimani.

Jambo linaloshangaza ni kuwa kwenye Shitanglin, ambayo kimsingi hakuna udongo, inaonekana miti ya misonobari, mizizi mikubwa inayazunguka mawe ya volkano na kupenyeza chini kwenye nyufa za mawe. Miti hiyo mifupi inaonekana kama maua ya yungiyungi yaliyoota kwenye theluji, na kuleta uhai kwa Mlima Aershan.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-20