Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-21 16:51:43    
Jeshi la anga la Russia laonesha tena nguvu zake

cri

Tarehe 19 ndege za kivita za Russia zilipaa angani kutoka kwenye manowari ya "Jemadari Kuzniezov". Hii inamaanisha kuwa jukumu la ndege za kivita zinazoruka na kurudi kwenye manowari yenye ndege limerudi tena. Kabla ya hapo, ndege 14 zikiwemo ndege za makombora, ndege za kulinda safari ya manowari na ndege za kuongeza mafuta angani, zimeanza tena kufanya doria baada ya kuacha kufanya hivyo kwa miaka 15.

Habari kutoka kituo cha televisheni cha taifa cha Russia zinasema, kitendo hicho cha kuanza tena kufanya doria kilitangazwa na rais Putin tarehe 17 wakati wa luteka ya majeshi ya nchi za Jumuyia ya Ushirikiano ya Shanghai. Rais Putin alisema tarehe 17, ndege za kivita za Russia zilikuwa angani kwa muda wa saa 20, na katika muda huo ndege hizo ziliongezwa mafuta angani na kufanya ushirikiano na jeshi la baharini. Alisema, mwaka 1992 Russia ilisimamisha doria ya ndege za makombora kwa upande mmoja, lakini inasikitika kuwa sio nchi zote zilizofanya uamuzi kama huo, hali hiyo ni tishio kwa usalama wa Russia. Kutokana na sababu hiyo ameamua kurudisha tena doria, anatumai kuwa nchi nyingine zitaelewa hatua hiyo.

Tarehe 9 Julai amirijeshi mkuu wa jeshi la baharini Bw. Vladimir Masorin alitangaza kuwa Russia imeamua kutenga ruble zaidi ya milioni 900 ili kujenga kituo kipya cha nyambizi za nyukilia, na inapanga kutenga fedha nyingi ili kujenga kituo cha manowari kwenye maji kama ni maandalizi ya kupanga manowari zenye ndege.

Imefahamika kuwa hivi sasa Russia ina ndege 80 za mabomu zinazoweza kusafiri mbali, kati ya ndege hizo, nyingi ni ndege zilizotengenezwa miaka ya Urusi ya zamani, ambazo zinaweza kubeba silaha za nyukilia. Hivi sasa Russia ina mpango wa kuzifanyia ndege hizo mabadiliko, huku ikitengneza ndege mpya za makombora za masafa marefu.

Hivi karibuni Russia kwa mara nyingi imeonesha nguvu zake za kijeshi. Tarehe pili, mchunguzi wa Russia akitumia chombo cha kupigia mbizi alizama chini kwa mita 4000 na alisimika bendera ya taifa la Russia chini ya bahari ya ncha ya kaskazini ya dunia. Tarehe 17 ndege 11 zilifanya mazoezi ya kivita kwenye upande wa magharibi wa Norway, hayo ni maonesho makubwa ya nguvu za angani za Russia tokea mwanzo wa miaka ya 90 ya karne iliyopita. Zaidi ya hayo, hivi karibuni mazoezi ya kivita ya Russia yamekuwa yanafanyika hapa na pale, na mazoezi hayo ni makubwa na hayakutokea kabla ya hapo.

Wachambuzi wanaona kuwa sababu za kuanza tena kwa ndege za kivita za Russia kufanya doria ni kama zifuatazo:

Kwanza ni kuonesha nguvu zake. Tokea mwanzoni mwa mwaka huu, Marekani imekuwa inapanga kuweka mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora kwenye sehemu ya Ulaya ya Mashariki bila kujali upinzani wa Russia, uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukawa mbaya, kwa hiyo kwa makusudi Russia inataka kuonesha hasira yake kwa Marekani na kuitahadharisha Marekani na NATO kwamba, Russia ina nguvu za kutosha kupigana nazo na kuzionya zisifanye vitendo bila kufikiri kabla. Pili ni kuwa katika miaka ya hivi karibuni uchumi wa Russia umekuwa unakua kwa kasi, hali ya kisiasa ni tulivu, kwa hiyo ina msingi wa kiuchumi katika mapambano dhidi ya Marekani na nchi za Magharibi. Tatu ni kwa ajili ya uchaguzi mkuu nchini Russia. Russia inataka kuonesha nia yake ya kurudisha tena hadhi yake ya taifa kubwa kwa kudhihirisha msimamo wake mkali dhidi ya nchi za Magharibi, ili kupata uungwaji mkono wa wananchi na kuleta hali nzuri ya uchaguzi mkuu.

Hivi sasa Russia na Marekani zinatofautiana katika masuala mengi, na uhusiano kati yao umekuwa ukididimia. Russia inaishutumu Marekani kupanga mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora katika Ulaya ya Mashariki, na Marekani inaishutumu Russia kwa hali mbaya ya haki za binadamu. Hivi karibuni bei ya mafuta imepanda, hali hii inaiwezesha Russia yenye mafuta mengi kuongeza fedha katika mambo ya kijeshi. Wachambuzi wanaona kuwa nia ya Russia kurudisha doria ya ndege za kivita ni kutaka kuonesha nguvu zake, na nia ya kutaka kurudisha hadhi yake ya taifa kubwa duniani, lakini uhusiano kati ya Russia na Marekani utaendelea kuwa na migongano na mazungumzo.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-21