Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-21 19:06:37    
Barua 0819

cri

Msikilizaji Medadi. S. Mpondamali wa sanduku la Posta 2005 Mabamba, Kigoma, nchini Tanzania, ametuletea barua yake akitueleza kuwa yeye anafurahishwa sana na matangazo yetu, lakini tatizo ni kuwa huwa anabahatisha mara chache kupata matangazo yetu, kwa sababu hajui muda wa matangazo yetu ni saa ngapi. Hivyo anaomba tumtumie ratiba ya matangazo yetu na ikiwezekana na picha za watangazaji na kalenda, pamoja na majarida yanayohusu matangazo yetu.

Naye msikilizaji wetu Asha Kheri Ally wa sanduku la Posta 60508 Dar es Salaam, Tanzania, ameanza barua yake kwa salamu nyingi kwa wasikilizaji na wafanyakazi wa Radio China kimataifa. Anasema lengo la barua yake ni kutaka kujua hali zetu, na kututakia baraka na mafanikio katika shughuli zetu mbalimbali za kila siku. Anamaliza kwa kusema anashukuru kwa kumtumia barua na zawadi nyingine kila wakati. Anafurahi sana kuona tunawafuatilia sana wasikilizaji wetu na kuwaalika kuitembelea China. Anamaliza barua yake kwa kusema na yeye atajitahidi siku moja aje kuitembelea China.

Tunamshukuru sana Bwana Medadi. S. Mpondamali kwa barua yake, ambayo ametueleza kuwa usikivu wa sehemu alipo si mzuri, kweli siku hizi matangazo yetu kwenye masafa mafupi yanaweza kusikika vizuri katika sehemu nyingi za Afrika ya mashariki, lakini hayasikiki vizuri kwenye sehemu kadha wa kadha, tumepata malalamiko mengi kuhusu hiyo kutoka kwa wasikilizaji wetu, tumetoa ripoti kwa ofisi husika ya Radio China Kimataifa, lakini tuna imani kuwa, baada ya kufanya juhudi za aina mbalimbali tutaweza kuboresha matangazo yetu, hivi sasa tunawaomba tu wasikilizaji wetu wawe na uvumilivu, samahani sana.

Msikilizaji wetu Kennedy Nyongesa Barasa Wanakuta wa sanduku la Posta 172 Bungoma Nchini Kenya ametuletea barua akianza kuipongeza Radio China kwa kuendeleza lugha ya Kiswahili. Pamoja na pongezi hizo katika barua yake pia ametuandikia mambo kadhaa ambayo yeye anasema ni utangulizi wa historia ya Kiswahili. Anasema lugha yoyote hasa iliyo hai na inayokua, inatokana na mazingira maalumu ya watu na utamaduni wao. Kiswahili ni lugha ya Afrika mashariki iliyoenea na kujulikana kwa watu wengi zaidi katika Afrika mashariki kuliko lugha nyingine yoyote ya Afrika. Anaendelea kusema kuna wakati na baadhi ya watu wanadhani kuwa lugha hii ni ya kigeni, yaani asili yake si Afrika. Lakini hivi leo ni wachache ambao wana mawazo kama hayo.

Anasema wengine bado wameshikilia kuwa utamaduni wa Kiswahili ni wa kigeni, na kamwe hakuna watu wanaoitwa waswahili. Kama ambavyo lugha ya Kiswahili imekuwa ni lugha ya Afrika, utamaduni wake nao vile vile una asili kamili ya kuwa ni lugha ya Afrika. Anasema ukifananisha misamiati ya Kiswahili na ya makabila mengine utaona kuwa inataka kufanana, ingawa si sawa sawa kabisa, maana misamiati hiyo itakuwa ni ya makabila mawili tofauti.

Anasema tofauti kama hiyo vile vile inaweza kuonekana kati ya makabila mbalimbali. Pia anasema utamaduni wa Kiswahili na mazingira yake, hasa ni sehemu ya nchi iliyopakana na maji ya Pwani. Kama ambavyo watu ambao asili yao ni bara hili la Afrika wanaitwa waafrika, na kama ambavyo waafrika wengi wanaopatikana katika sehemu kubwa ni wabantu, basi wabantu wa pwani ya Afrika mashariki na visiwa mbalimbali vilivyo jirani na waswahili, wao wana makabila yao na ndani ya makabila hayo kuna mgawanyiko wa makabila madogomadogo. Mwisho anamaliza barua yake kwa kusema tusishangae kuona watangazaji wa Radio China kimataifa na kwingineko ambako lugha ya Kiswahili ilikuwa haitumiki, lakini kutokana na maingiliano ya watu yamefanya lugha ya Kiswahili itumike. Hivyo anatoa pongezi kwa Radio China Kimataifa kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Kenedy Nyongesa kwa barua yake ya kuelezea maoni yake kuhusu kuenzi lugha ya Kiswahili. Ni kweli Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa inajiahidi kutumia vizuri lugha ya Kiswahili kuandaa matangazo yake ili kuwahudumia wasikilizaji wake walioko barani Afrika. Ingawa kuna wakati tunakutana na matatizo fulanifulani ya kutafuta maneno au misamiati ya Kiswahili wakati tunapotafsiri taarifa au makala mbalimbali, lakini tunaona lugha ya Kiswahili ni lugha tunayopenda kuitumia, ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa ni chombo cha mawasiliano kati yetu na wasikilizaji wetu. Kutokana na kujifunza lugha hii tunaweza kuelewa mengi kuhusu mambo ya nchi za Afrika na kuwaelewa na kujenga urafiki na wananchi wa nchi za Afrika, ni matumaini yetu kuwa tutashirikiana na wasikilizaji wetu katika kuendeleza zaidi Lugha ya Kiswahili, ili lugha hii ya Afrika iweze kung'ara zaidi duniani.

Msikilizaji wetu mwingine ni Bw. Mutanda Ayub Shariff wa sanduku la Posta 172 Bungoma nchini Kenya. Yeye ameanza barua yake kwa salamu kwa wafanyakazi wa Radio China Kimataifa na anatumai kuwa wote tu wazima na tunaendelea kuchapa kazi kama kawaida. Anasema pamoja na kuwa katika shughuli zake sehemu mbali mbali hajawahi kukosa hata siku moja kuwaza jinsi ya kufanya ili matangazo ya Radio China Kimataifa yang'are duniani kote.

Anafurahi kwa sasa anavyoendelea kutusikia katika mawimbi ya FM 91.9 na anatarajia kuendelea kupata habari nzuri zaidi kupitia mawimbi hayo, anasema ila tu usikivu wa matangazo katika mkoa wa magharibi Bungoma unakuwa wa shida. Anasema pamoja na yote hayo upendo alioonao kwa Radio China Kimataifa umemfanya ajitolee sana na kuweka maslahi yake kando na kuwa na upendo kwa Radio China kimataifa. Wakati wa kipindi cha mwisho yaani kuanzia saa mbili hadi saa tatu usiku, mpangilio wa vipindi unampa nguvu na furaha, kwani ni vizuri sana na wakati mwingine kipindi cha salamu zenu kinawekwa mwisho.

Kuhusu burudani ya muziki anasema ni jambo nzuri iwapo kama itawezekana nyimbo ziwe za mchanganyiko wa kiafrika na kichina. Mapendekezo yake kwa Radio China Kimataifa kwa sasa ni kuajiriwa wahariri wengi na Afisa uhusiano ambaye atashughulikia uhusiano kati ya wasikilizaji na wafanyakazi wa Radio China Kimataifa. Pia naona kwa sasa mawasiliano yameimarika sana japokuwa shida ipo katika jarida la urafiki kwani toka mwaka jana mpaka sasa bado halijatoka. Anamaliza barua yake kwa kusema kuwa juhudi zake za kutaka kukutana na mhariri wa Nairobi ili aweze kutoa maoni na mapendekezo yake bado hazijafanikiwa, lakini ataendelea.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sharif kwa mapendekezo aliyotoa kuhusu matangazo yetu. Tunafurahia kama anafurahishwa na matangazo yetu, kwani hilo ndio lengo letu hasa. Na kuhusu suala la Ofisa anayeshughulikia uhusiano kati yetu na wasikilizaji wetu, yupo na anafanya kazi kwa bidii kila siku akishughulikia barua pepe, barua, kutuma majarida na zawadi mbalimbali pamoja na kadi za salamu kwa wasikilizaji wetu, kwa hiyo usiwe na hofu na hilo .