Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-22 15:23:27    
China yaimarisha hatua kwa hatua shughuli za kutoa mafunzo kwa mbwa wanaoongoza watu wasioona

cri

Katika miaka miwili iliyopita, shughuli za kutoa mafunzo kwa mbwa wanaoongoza watu wasioona zimekuwa zinaendelea hatua kwa hatua nchini China, na zimerahisisha sana maisha ya watu hao. China ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watu duniani, pia ni nchi yenye idadi kubwa ya watu wasioona duniani, ikiwa imefikia zaidi ya milioni 12. Matatizo yanayowakabili watu wasioona maishani hayawezi kufikirika kwa watu wanaoona. Mbwa wanaowaongoza watu wasioona, ambao ni wasaidizi wazuri kabisa wa watu hao ambao wanaweza kuwasaidia watu wasioona kuishi maisha ya kawaida.

Katika mtaa wa biashara wa wilaya ya Shuangdao kwenye eneo la Lushunkou mjini Dalian mkoani Liaoning, kila siku wakazi wa huko wanamwona mwanamke mmoja asiyeona akitembea mtaani huku akiwa anaongozwa na mbwa. Bibi Zhang Shujun, na mume wake wote hawaoni na wameishi maisha ya upweke kwa zaidi ya miaka 40. Nusu ya mwaka iliyopita, mbwa mmoja anayeongoza watu wasioona aitwaye Maomao alianza kuishi familia hiyo na kuwaletea furaha.

"Bi. Zhang: Maomao, niletee viatu! Haya, weka chini! Vizuri sana! Sasa namchukulia Maomao kama mtoto wangu, na kumtunza zaidi.

Mwandishi: kila siku unakwenda naye nje?

Bi. Zhang: ndiyo, kila siku ninakwenda kununua chakula na kutembea naye mara moja au mbili.

Mwandishi: zamani bila mbwa huyo, uliweza kwenda kununua chakula peke yako?

Bi. Zhang: sikuweza, nilikuwa nasaidiwa na majirani na watoto tu."

Bi. Zhang pia alisema kwa furaha kuwa, hivi karibuni alirudi peke yaka kwenye maskani yake yenye umbali wa kilomita mia kadhaa kutoka mji wa Dalian kwa garimoshi akiongozwa na mbwa wake Maomao. Alisema:

"najisikia sina tofauti na watu wanaoona, na nina matumaini makubwa kwa maisha. Nikitaka kufanya jambo lolote, naweza kufanya mara moja peke yangu, naona kweli ni rahisi sana."

Mbwa Maomao aliyeleta urahisi kwa maisha ya Bi. Zhang anatoka kwenye kituo cha mafunzo ya Mbwa wanaoongoza watu wasioona katika chuo kikuu cha udaktari cha Dalian, ambacho ni kituo cha kwanza cha aina hiyo nchini China. Mkurugenzi wa kituo hicho ambaye ni daktari wa elimu ya vitendo vya wanyama Bw. Wang Jingyu alisema, hivi sasa vituo zaidi ya 80 vya mafunzo kwa Mbwa wanaoongoza watu wasioona vimejengwa katika nchi 27 kote duniani, na Mbwa zaidi ya elfu 20 waliopewa mafunzo wanahudumia watu wasioona kote duniani. Idadi ya watu wenye ulemavu huo nchini China ni zaidi ya milioni 12, hivyo China itahitaji Mbwa wengi waliopewa mafunzo hayo.

Bw. Wang Jingyu alisema, kituo hicho kilianzishwa mwezi Mei mwaka 2005. Mbwa waliopewa mafunzo wanaweza kusaidia maisha ya watu wasioona, kuwaongoza watu hao wakitembea na kutoa tahadhari kuhusu vizuizi njiani. Kutokana na misaada ya Mbwa hao, watu wasioona wanaweza kushiriki kwenye maisha ya kijamii kama kawaida na kurejesha nia ya kujiamini na kujithamini. Kuhusu uchaguzi wa aina za Mbwa na utaratibu wa mafunzo, Bw. Wang Jingyu alisema:

"tunachagua Mbwa aina ya Labrador na Golden Retreaver, kwa kuwa mbwa wa aina hizo mbili wanatambuliwa duniani kuwa aina zinazofaa kuwa mbwa wanaoongoza watu wasioona. Mbwa wa aina hizo mbili wana ukubwa na uzito wa wastani, mwendo wao wa kutembea pia unafanana na ule wa binadamu, pia Mbwa hao wana uwezo kiasi wa kufanya uamuzi."

Tangu mbwa kuchaguliwa kutoka sokoni, watapelekwa nyumbani kwa watu wanaojitolea siku 45 baada ya kuzaliwa, baada ya mwaka mmoja, watarudishwa kwenye kituo cha mafunzo na kuanza kupewa mafunzo rasmi. Mafunzo hayo yanafanyika kwa muda wa nusu mwaka, kwa kawaida, asilimia 60 hadi 70 za mbwa wanashindwa kufuzu mafunzo hayo, wale wanaotimiza masharti wataanza kuishi na watu wasioona kwa miezi miwili. Mwishowe wanapelekwa nyumbani kwa watu wasioona na kuwahudumia bure. Baada ya miaka 6 hadi 8, kipindi cha kutoa huduma cha mbwa kitamalizika na mbwa hao hurudishwa tena kwenye kituo cha mafunzo na kupelekwa kwa watu wanaojitolewa kuwafuga.

Kituo cha mafunzo kwa mbwa wanaoongoza watu wasioona cha Dalian kina watoa mafunzo 23, wengi wao ni vijana waliohitimu elimu ya wanyama chuoni, wote wanapenda wanyama na kupenda kazi hiyo. Kwenye kituo hicho, mtoa mafunzo Bi. Jiang Dan alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kazi hiyo si rahisi. Alipoanza kazi hiyo, alikuwa anadhani kuwa anaweza kucheza na mbwa, lakini mafunzo rasmi yalipoanza aliona ugumu wake. Bi. Jiang Dan alisema, ingawa kazi hiyo ni ngumu, lakini akiona mbwa wanaendelea kupata maendeleo atafurahi sana. Kama mbwa wanaweza kuwasaidia vizuri watu wasioona, ni vizuri kuvumilia ugumu huo.

Hivi sasa shughuli za mafunzo kwa Mbwa wanaoongoza watu wasioona bado zinakabiliwa na matatizo mbalimbali, yakiwemo nadharia zisizo kamili kuhusu mafunzo kwa mbwa, ukosefu wa uzoefu na upungufu wa fedha. Kinachofurahisha ni kuwa mwishoni mwa mwaka 2007, serikali ya China itaweka sheria husika ili kuunga mkono kisheria matumizi ya mbwa wanaoongoza watu wasioona.

Mwezi Mei mwaka 2007, mbwa wawili kutoka kituo hicho walishiriki kwenye shughuli husika za michezo ya 7 ya walemavu ya China. Naibu waziri mkuu wa China Bw. Hui Liangyu aliyehudhuria michezo hiyo alisema, kwa uhakika China itatoa uungaji mkono wa kisheria na kijamii kwa maendeleo ya shughuli za mafunzo kwa Mbwa wanaoongoza watu wasioona. Kutokana na uhakiki pamoja na uungaji mkono wa serikali na ufuatiliaji wa jamii, shughuli hizo zinaendelea na kupanuliwa zaidi.