Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-22 16:28:37    
Kwa nini Iran imeonesha ishara nzuri katika suala la nyuklia?

cri

Mazungumzo ya duru la tatu kati ya Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki yalimalizika tarehe 21 jioni huko Tehran. Baada ya mazungumzo pande zote mbili zilisema mazungumzo hayo yamepata maendeleo, na zimefikia makubaliano kuhusu masuala yaliyotakiwa kutatuliwa katika muda maalum kwenye mpango wa nyuklia wa Iran.

Mazungumzo hayo yalifanyika kwa muda wa saa 15. Baada ya mazungumzo naibu katibu wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Iran Bw. Javad Vaeedi alisema, baada ya kufanya mazungumzo mara tatu katika miezi miwili, mwishowe pande mbili zimeafikiana kimsingi kuhusu masuala yaliyobaki, na zimepata maendeleo yenye maana. Naibu katibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Olli Heinonen alisema, mazungumzo ni ya kujenga, pande mbili zimeafikiana kimsingi kuhusu "mpango wa utekelezaji".

Watu wanasema ushirikiano mzuri wa Iran katika mazungumzo hayo unatokana na sababu mbili:

Moja ni kuzuia Umoja wa Mataifa usipitishe azimio la tatu la kuiwekea vikwazo Iran. Katibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Mohamed el Baradei mwezi Septemba atatoa ripoti mpya kuhusu suala la nyuklia la Iran kwa bodi ya wakurugenzi ya kamati yake. Wakati huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya uamuzi kama litachukua hatua mpya za kuikwamisha Iran au la kwa mujibu wa ripoti hiyo. Kwa hiyo Iran ni lazima ioneshe ishara nzuri kwa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki ili kamati hiyo iisemee vizuri katika ripoti hiyo.

Sababu nyingine ni kwamba hali ya kukwama kwa muda mrefu kuhusu suala la nyuklia ni mzigo mzito kwa Iran, na Iran inaelewa kwamba bila kurudi nyuma hali hiyo itaendelea bila kikomo. Baada ya mazungumzo naibu katibu wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Iran Bw. Javad Vaeedi aliwaambia waandishi wa habari kwamba, Iran itatoa ushirikiano kwa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki katika kazi ya ukaguzi wa nyuklia nchini Iran na kufanya kinu cha maji mazito kilichoko Arak na kituo cha kusafisha uranium kilichoko Natanz viwe wazi zaidi. Mwandishi mmoja wa habari wa Shirika la Habari la Marekani alisema, Iran imefungua mlango wa kinu cha maji mazito ambacho ni nyeti, hii inaashiria kwamba Tehran iko tayari kuziweka zana za nyuklia chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kwamba serikali ya Iran inataka kuvunja hali ngumu ya kukwama kwa kulegeza masharti.

Marekani haitilii maanani makubaliano kati ya Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, yenyewe inaona kuwa Iran haifai kusimama kwenye ushirikiano kati yake na shirika hilo, bali ni lazima isimamishe shughuli za kusafisha uranium, ambazo zinatia wasiwasi jumuyia ya kimataifa. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Nicholas Burns tarehe 20 alisema, kwa makusudi Iran inarefusha muda. Alisema, Iran ni nchi isiyoaminika, na Marekani haiwezekani kuacha juhudi za kulifanya Baraza la Usalama liiwekee vikwazo kwa sababu tu inaonesha ushirikiano kwa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki.

Kuhusu msimamo wa Marekani, mjumbe wa kwanza wa mazungumzo wa Iran Bw. Ali Larijan alisema, iwapo nchi fulani italisukuma Baraza la Usalama lipitishe azimio la kuiwekea vikwazo Iran, basi Iran itasimamisha juhudi zake na kuchukua "hatua za mapambano". Rais wa Iran Bw. Mahmoud Ahmadinejad pia alisema, Iran "imenyakua" kilele cha teknolojia ya nyuklia, mtu yeyote hataruhusiwa kuwekeza vikwazo kwenye njia ya maendeleo ya nyuklia, na Iran haitasujudu kwa shinikizo lolote na kusimamisha shughuli zake za kusafisha uranium.

Hali iliyoelezwa inaonesha kuwa utatuzi wa suala la nyuklia la Iran unaweza kupatikana kwa njia ya amani, lakini bado kuna matatizo mengi, jumuyia ya kimataifa inatakiwa kuendelea na juhudi.