Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-24 16:57:51    
Mpigapicha wa China asifiwa na shirika la UNEP kutokana na juhudi zake katika kuhifadhi mazingira

cri

Sehemu ya hifadhi ya maumbile ya Nakuru nchini Kenya ambayo inajulikana duniani kutokana na kuwa na flamingo, katika mlango wa sehemu hiyo umewekwa ubao mmoja ulioandikwa kwa Kichina na Kiingereza kuwa "Msanii wa Jamhuri ya watu wa China Bw. Luo Hong ni mfadhili wa utekelezaji wa kipindi cha mwanzo cha mradi wa kuhifadhi flamingo". Juu ya maneno hayo kuna alama ya bendera za Kenya na China, na alama ya Shirika la Mipango ya mazingira la Umoja wa Mataifa.

Bw. Luo Hong ni meneja mkuu wa Kampuni ya Holiland ambayo inajulikana sana nchini China kutokana na utengenezaji wa keki, sasa kampuni hiyo imekuwa na mtaji wa zaidi ya Yuan za Renminbi bilioni moja na matawi zaidi ya 600 kote nchini.

Tarehe 18 mwezi Julai kwenye kando ya ziwa Nakuru, Bw. Luo Hong na balozi wa China nchini Kenya Bw. Zhang Ming pamoja na naibu waziri wa mazingira wa Kenya Bi. Jane Kihara walihudhuria sherehe ya kuzindua mradi huo wa kuhifadhi mazingira, wenye lengo la kuzuia kupungua kwa idadi ya flamingo. 

Maofisa wa Shirika la Mipango ya Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP waliohudhuria sherehe hiyo walimsifu Bw. Luo kutokana na kitendo chake. Mkurugenzi wa sehemu ya Afrika ya shirika hilo Bw. Sekou Toure alitoa hotuba kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Bw. Achim Schteiner akisema, mchango wa Bw. Luo Hong unaonesha kuwa, mbali na serikali watu binafsi pia wanashiriki kwenye miradi ya kuhifadhi mazingira ya Umoja wa Mataifa, hii pia ni hatua muhimu kwa Shirika la UNEP kuendeleza uhusiano na China.

Naibu mkurugenzi wa Idara ya ushirikiano wa kikanda katika Shirika la UNEP Bi. Wang Zhijia alisema, fedha zilizotolewa na Bw. Luo Hong zilisaidia mipango ya mazingira ya Umoja wa Mataifa iweze kutekelezwa zaidi. Kama vile kuanzisha tovuti ya Kichina ya Shirika la UNEP, kuunga mkono michezo ya Olimpiki ya Beijing, kutoa mafunzo kwa maofisa wa Asia na Afrika wanaoshughulikia kuhifadhi mazingira.

Bw. Luo Hong kwenye sherehe hiyo alisema Ziwa Nakuru lina mandhari nzuri, flamingo milioni kadhaa na ndege wengine hapa ni marafiki zangu. Wananifanya niwe shabiki wa kupiga picha za wanyama wa Afrika. Alisema kila mwaka anakwenda kwenye ziwa hilo kuwatembelea flamingo.

Ziwa Nakuru ni sehemu nzuri ya kuwaangalia ndege. Wakati alipogundua kuwa idadi ya flamingo inapungua siku hadi siku, Bw. Luo Hong alisikitika sana na kuamua kutoa mchango wa fedha ili kuwahifadhi flamingo.

Luo Hong husema matumaini yake makubwa ni kuonyesha mandhari nzuri ya kimaumbile kwa kutumia picha zake, na kuwafanya watu wapende dunia ya maumbile na maisha yao, na kushirikiana kuhifadhi dunia hii ambayo ni maskani ya pamoja ya binadamu.

Mwezi Novemba mwaka jana, Bw. Luo Hong aliahidi kuanzisha "mfuko wa kuhifadhi mazingira wa Luo Hong" wenye yuan za Renminbi milioni 10 kwenye Shirika la UNEP, ambapo yuan milioni moja kati ya hizo zitatumika katika kuwahifadhi flamingo.

Hali ya maisha ya flamingo nchini Kenya inakuwa mbaya siku hadi siku. Katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, idadi ya flamingo nchini Kenya ilifikia milioni 3, lakini sasa imepungua hadi kufikia milioni 2. Idadi ya flamingo barani Afrika imepungua kati ya milioni 1.5 na 2.5 kutoka milioni 5 ya mwaka 1974. Wataalamu wanakadiria kuwa mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi wa mazingira na shughuli za binadamu ni sababu zinazofanya idadi ya flamingo liungue.

Mtafiti wa Shirika la UNEP alifahamisha kuwa, kupungua kwa ya idadi ya flamingo ni ishara ya mabadiliko ya hali ya uwiano ya mazingira ya viumbe, hivyo kuhifadhi flamingo kuna umuhimu mkubwa kwa kuhifadhi aina tofauti za viumbe vingine katika Ziwa Nakuru.

Mwezi Oktoba mwaka 2001, Bw. Luo Hong alikwenda Afrika kwa mara ya kwanza kupiga picha za mandhari ya kimaumbile na wanyama pori. Mji wa kwanza aliotembelea Bw. Luo Hong barani Afrika ni Cape Town, Afrika kusini. Alitembelea bustani ya kitaifa ya wanyama pori, na kupiga picha nyingi za wanyama pori. Aliona kuwa bara la Afrika si kama tu lina mandhari nzuri, bali pia lina wanyama pori wengi wanaopendeza sana, kuanzia hapo akawapenda wanyama pori hao.

Mwaka 2002, Bw. Luo Hong alikwenda Kenya kutembelea mbuga ya Masai Mara na kwanda Namibia. Baada ya kurudi kutoka Afrika alianza kufanya utafiti kuhusu mambo ya Afrika ili afahamu hali ya hewa, hali ya kijiografia ya nchi za Afrika na tabia za wanyama.

Bw. Luo Hong amewahi kutembelea nchi 6 za Afrika, na kukutana na wakazi wengi wa kawaida, picha nzuri aliyopata kuhusu watu wa Afrika ni kwamba, watu wa Afrika wanaishi kwa furaha, tabia zao za kuwa na furaha zilimfurahisha, hivyo kila anapokwenda kwenye nchi za Afrika yeye mwenyewe hufurahi. Alisema kuwa, akiwa na nafasi mwaka huu, atakwenda tena barani Afrika.

Bw. Luo Hong aliangalia na kufurahia uzuri wa Afrika kwa kutumia kamera yake. Mwaka 2005 picha zake zilianza kuoneshwa ndani ya vituo vya subway mjini Beijing. Mwaka huu ili kuadhimisha siku ya mazingira duniani ya tarehe 5 Juni, shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP lilimwalika Bw. Luo Hong aende Nairobi kufanya maonesho ya picha, ambazo zilisifiwa sana na watazamaji.

Bwana Luo Hong anajishughulisha na mambo anayoyapenda kwa moyo wake wote. Katika miaka mitano iliyopita, kwa jumla alitembelea bara la Afrika mara 11, ili kupiga picha za wanyama pori.

Mambo aliyojifunza Bw. Luo Hong katika safari zake barani Afrika ni kuwa, wanyama pori wengi wa Afrika ni wema kwa binadamu, lakini sharti ni usiwabugudhi kwa kusumbua maisha yao ya kawaida.

Akiwa shabiki wa upigaji picha anayefuatilia suala la mazingira, Bw. Luo Hong alieleza matumaini yake kuwa, watu wanapofurahia picha zake, wataweza kusikia mwito wa dunia ya maumbile kutoka kwenye picha alizopiga. Alisema:

"Natarajia kuwa tutaonesha shukurani kwa dunia ya maumbile, na kufanya mambo mazuri kwa dunia ya maumbile, tutaishi pamoja na wanyama na dunia ya maumbile kwa masikilizano."

Idhaa ya kiswahili 2007-08-24