Tarehe 23 Agosti kwa saa za Costa Rica, ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Jamhuri ya Costa Rica ilizinduliwa rasmi, ambapo kwa mara ya kwanza bendera ya taifa la Jamhuri ya Watu wa China ikapandishwa juu kwenye mlingoti nchini Costa Rica. Kwenye sherehe iliyofanyika siku hiyo, wachina wengi wanaoishi huko waliposikia wimbo wa taifa la China na kuangalia bendera ya taifa la China walitokwa na machozi. Bwana Huang Yanting ni mchina anayeishi kwa miaka mingi nchini Costa Rica, ambaye ni mkurugenzi wa heshima wa Shirikisho kuu la viwanda na biashara la China na Costa Rica alisema:
"sisi wachina tunaoishi nchini Costa Rica tunafurahia sana kuona matarajio yetu ya miaka mingi yametimizwa, yaani China na Costa Rica zimeanzisha uhusiano wa kibalozi, na pia tunafurahia zaidi nguvu ya taifa letu China inayoongezeka siku hadi siku".
Kwenye sherehe hiyo, msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bwana He Yafei alisema, kuanzishwa kwa uhusiano kati ya China na Costa Rica ni jambo kubwa lenye umuhimu mkubwa, ambalo limeonesha kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeingia katika kipindi kipya cha maendeleo. Serikali ya China inatilila maanani kuendeleza uhusiano na Costa Rica, na inapenda kukuza na kupanua zaidi ushirikiano wa kunufaishana kati ya pande hizo mbili katika sekta mbalimbali kwa msingi wa kuheshimiana, kuwa na usawa na kunufaishana. Akisema:
"katika siku za baadaye, Ubalozi wa China nchini Costa Rica utakuwa daraja kubwa la uhusiano kati ya nchi mbili, nina imani kuwa ubalozi wa China utatoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili".
Watu wa sekta mbalimbali wa China na Costa Rica wapatao zaidi ya 200 walishiriki kwenye sherehe hiyo ya kuzinduliwa kwa ofisi ya ubalozi wa China nchini Costa Rica. Balozi wa Argentina nchini Costa Rica Bwana Juan Josea Arcuri aliwaambia waandishi wa habari akisema:
"Costa Rica kuanzisha uhusiano wa kibalozi na China, ni uamuzi unaofuata hali halisi ya sasa, kwani China ni moja kati ya nchi zenye nguvu kubwa duniani. Kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili kutaleta maslahi mengi kwa pande hizo mbili".
Mwandishi wa habari wa kituo kimoja cha televisheni cha Costa Rica Bibi Monic alisema:
"mambo ya uchumi na biashara ni mambo makubwa sana kwa Costa Rica, rais wetu anafanya juhudi kutafuta ufunguaji mlango kwa makundi mengi ya kiuchumi, na China ni chaguo lake moja zuri kabisa. Kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Costa Rica na China hakika kutasukuma mbele zaidi maendeleo ya uchumi wa Costa Rica, hivyo naunga mkono uamuzi huo wa rais wetu".
Rais Oscar Arias wa Costa Rica aliwahi kusema kuwa, kuanzisha uhusiano wa kibalozi na China ni uamuzi wa kidiplomasia wa Costa Rica katika mchakato wake wa kuimarisha uhusiano na nchi za Asia. Kwani Costa Rica haipaswi kupuuza tena uhusiano na China, ambayo ni kundi la uchumi lililo muhimi zaidi duniani.
Baada ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Costa Rica tarehe 1 Juni mwaka huu, serikali ya Costa Rica imetoa msaada mkubwa kwa kazi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa ofisi ya ubalozi wa China nchini humo. Balozi wa kwanza wa China nchini Costa Rica Bwana Wang Xiaoyuan alisema: "Serikali ya Costa Rica na wananchi wake wana matarajio makubwa juu ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili, wanatumai kutumia fursa hii kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uhusiano kati ya Costa Rica na nchi za nje. Na wafanyabiashara wa nchi hiyo wanapenda kuendeleza uhusiano na China".
Costa Rica ni nchi ya kwanza ya Amerika ya kati iliyoanzisha uhusiano wa kibalozi na China katika miaka ya hivi karibuni, tukio hili lina umuhimu maalum. Watu wa China na Costa Rica wana imani kuwa, kutokana na juhudi za pamoja na utunzaji wa pamoja, urafiki kati ya China na Costa Rica utaimarishwa siku hadi siku.
|