Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-28 15:53:15    
Barua 0828

cri
Msikilizaji wetu Mbarak Mohamed Abucheri wa sanduku la Posta 792 Kakamega, nchini Kenya ametuandikia barua akiunga mkono ushirikiano kati ya China na Afrika, na hivyo kutoa maelezo yake kuhusu ushirikiano huo ambapo yeye anoana ni ushirikiano wenye mafanikio na manufaa.

Anasema Mnamo tarehe 3 hadi 5 Novemba, mwaka 2006 mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mjini Beijing, ambapo nchi na wawakilishi zaidi ya 40 walihudhuria katika mkutano huo, na wajumbe karibu ya 200 nao walihuhudhuria. Anasema bara la Afrika ni la pili kwa ukubwa duniani ambapo linachukua karibu asilimia 23 ya jumla ya eneo lote duniani.

Kwa upande wa idadi ya watu, bara la Afrika lina watu wanaokaribia milioni 900 ya idadi ya watu duniani, ambao wanafurahia mambo mengi mazuri ya bara hilo, ikiwa pamoja na ubinadamu na ustaarabu. Anasema mchango wa bara la Afrika katika uchumi wa dunia ni asilimia moja tu pamoja na kuwa bara hilo ni lenye utajiri mkubwa na maliasili nyingi. Hivyo idadi kubwa ya watu katika bara hilo, bado hawapati huduma ya maji, umeme, elimu na kadhalika.

Anaendelea kusema kuwa Afrika ni bara lenye tofauti kubwa ya watu, kimaumbile, utamaduni na imani. Katika bara la Afrika unaweza kukutana na watu tofauti wenye uwanja mpana wa utamaduni na historia, lakini vile vile unaweza kusikia makumi kadhaa ya lugha mbalimbali na lahaja. Anasema mpaka sasa katika karne hii unaweza kukuta sehemu zenye machifu au vijijini kabisa watu bado wanaishi kama ilivyokuwa miaka mia moja iliyopita, na miji mikuu yenye vifaa vya kisasa.

Kwa upande wa China na Afrika anasema ni sehemu mbili zinazofahamiana vizuri, na kwa kweli historia ya uhusiano kati ya China na Afrika inaanzia miaka 3,000 iliyopita na tangu wakati huo sehemu hizo mbili zimekuwa zikifurahia uhusiano huo ambao ni wa kiutamaduni na kiuchumi. Lakini kwa bahati mbaya katika kipindi cha miaka 60, kuanzia karne ya 20 kumekuwa na kurudi nyuma kidogo kwa uhusiano huo.

Hatimaye baada ya miongo minne iliyopita China imetambua umuhimu wa bara la Afrika na kukuza mawasiliano na nchi za Afrika, lakini pia kuwa na mawasiliano katika masuala ya siasa, uchumi na utamaduni. Utulivu ni kitu kinachopewa kipaumbele katika bara la Afrika. Wote tunafahamu nchi za magharibi mara zote mazungumzo hayo makubwa yamekuwa kuhusu demokrasia kwa bara la Afrika na suala hilo limekuwa likiipa shinikizo kubwa bara la Afrika.

Kwa bara la Afrika anasema demokrasia, hadhi ya utu na maendeleo ya uchumi ni masuala ya maana sana na juhudi zimefanyika kwa ajili ya masuala hayo bila kusita, pamoja na ugumu na vikwazo kutoka katika nchi za magharibi. Hivyo anathamini uelewa na msaada wa nchi ya China na kama taifa, kwa bara la Afrika.

Kwa hiyo anasema tena kuwa wito wa umoja na ushirikiano wa kunufaishana na hasa kwa watu wa waafrika unawafanya kujitoa kwa mara nyingine katika kufanya juhudi kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini pia kwa ajili ya mustakabali mzuri wa bara la Afrika. Anasema na kwa moyo huo huo anaomba demokrasia iheshimiwe na kuwa na utamaduni wa kufanya kazi, ili bara la Afrika lifikie malengo ya milenia.

Anamaliza barua yake kwa kusema China na Afrika zimekuwa na uhusiano wa kubadilisha na endelevu katika kukuza uchumi na biashara na vile vile uungaji mkono wa pande zote mbili na kushirikiana kwa karibu katika masuala ya kimataifa. Urafiki wa sehemu hizo mbili umekuwa wa kusisimua na nguvu. Kutokana na sehemu hizo mbili kuwa na ushirikiano wa kunufaishana, uaminifu na kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la maendeleo.

Tunamshukuru sana Mbarak Mohamed Abucheri kwa barua yake inayotueleza mengi kuhusu urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, na umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya pande hizo mbili. Kweli sisi na wasikilizaji wetu tuna matumaini ya pamoja uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Afrika utaendelea zaidi siku hadi siku, na wananchi wa China na nchi za Afrika watapata manufaa halisi kutokana na mafanikio ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Msikilizaji wetu mwingine ni Bw. Ray Nzalusi Makokha wa sanduku la Posta 1 Mungatsi, nchini Kenya. Ametuletea barua yake ambayo anasema yeye anapenda kuwa mwandishi wetu nchini Kenya. Anasema kabila lake ni mluhya kutoka magharibi mwa Kenya, ana mke na watoto na ana umri wa miaka 60. Kuhusu elimu anasema yeye ana elimu ya Sekondari, na amefanya kazi akiwa karani mkuu wa mahesabu na baadaye kufanya kazi akiwa mhasibu katika makampuni ya kibiashara. Kazi zake kubwa anasema ni kuangalia vitabu vyote vya mahesabu na kukaimu mikutano yote ya meneja wake ambayo hufanyika katika ngazi ya wilaya na majimbo. Hivyo hupata nafasi ya kuzungumza na watu mbalimbali na kuweza kukusanya habari ambazo zinaweza kutangazwa.

Msikilizaji wetu wa sasa ni Pendo Lameck wa sanduku la Posta 100 Tabora, nchini Tanzania. Ameanza barua yake kwa kusema kuwa yeye ni msichana mwenye umri miaka 18 na anasoma katika shule inayoitwa New Era, mkoani Tabora, kwa sasa yuko kidato cha nne. Anasema lengo la barua yake ni kutoa ombi lake kwetu kumsaidia angalau kwa vyovyote vile ili apate mfadhili atakayeweza kumsomesha na mambo mengine. Anasema amefikia uamuzi huu baada ya kutafuta kila njia bila mafanikio, kwani aliyekuwa akimlipia ada sasa naye amesema amefikia mwisho na anakaribia kustaafu, kwa hiyo anaona ni vizuri kutunza fedha kwa ajili ya watoto wake.

Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa sanduku la Posta 69 injinia, North Kinangop, nchini Kenya. Yeye anaanza barua yake akiwa na matumaini makubwa kuwa sisi sote ni wazima. Anasema yeye pia na familia yake huko Injinia hawajambo. Ana furaha kubwa kuwa yeye siyo tu msikilizaji wa Radio China Kimataifa, bali pia ni mmoja wa wanachama, ambao hutajwa katika vipindi vya salamu mara kwa mara. Pia hufurahia sana kuchangia maoni na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha matangazo yetu.

Kuhusu zawadi anasema, anapendezwa na zawadi mbalimbali anazozipokea kutoka kwetu, ambazo zinampa hamasa kubwa. Kinachomfurahisha zaidi ni kuwa Radio China Kimataifa, ni chombo ambacho kimefanikisha nchi ya China ijulikane katika bara la Afrika.

Anasema kabla ya Radio China Kimataifa kuanza kurusha matangazo yake katika bara la Afrika, nchi ya China haikujulikana kama inavyojulikana sasa. waliobahatika kidogo kujua machache kuhusu China ni wale tu waliosoma historia, ambayo pia waandishi wake hawakuielewa vizuri. Mfano anasema kama historia ya Confucius, dini ya kibudha na wamongolia. Mwisho anamaliza barua yake kwa kutuomba tuendelee kuwafafanulia zaidi taswira ya nchi ya China, nchi iliyojaa mandhari ya kuvutia, kupitia kipindi cha Safari nchini China na anaomba tumtumie jarida la China Pictorial.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu wote wanaotuletea barua na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu vipindi vyetu. Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kusikiliza na kufuatilia kwa makini matangazo yetu na tufanye juhudi kwa pamoja kuandaa vipindi vizuri zaidi. Wasikilizaji wetu wenye maombi kuhusu misaada ya udhamini wa masomo, tunasikitika kwa sisi tunashughulika na mambo ya matangazo. Kwa bahati mbaya mambo yanayohusu udhamini wa masomo kutoka hapa China yanashughulikiwa na idara nyingine zinazoleta nafasi za udhamini kwa serikali za nchi mbalimbali, tunaomba mtuelewe.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-28