Hivi karibuni kauli ya kumkosoa waziri mkuu wa Iraq Bw. Nouri al-Maliki imekuwa inasikika sana nchini Marekani, na hata baadhi ya wanachama wa Chama cha Democrat wanataka afukuzwe madarakani. Lakini Bw. Nouri al-Maliki hakuonekana kama ni mnyonge, bali alijitokeza na kuwajibu moja kwa moja watu hao wa Chama cha Democrat na kuipiga kijembe serikali ya rais Bush. Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya wanasiasa wengi kumshambulia waziri mkuu huyo inatokana na mapambano ya kisiasa yanayoongezeka kuwa makali kati ya vyama viwili kabla ya uchaguzi mkuu. Majibu makali kwa watu wa Chama cha Democrat yanaonesha kuwa Bw. Maliki anataka kujipatia muda mrefu zaidi ili aweze kutatua matatizo ya kisiasa yanayomkabili kama rais Bush.
Dalili zote zinaonesha kuwa ingawa rais George Bush amefahamu kwamba kutokana na matatizo ya Iraq, chama chake cha Republican hakika kitashindwa na Chama cha Democratic katika uchaguzi mkuu, lakini hana nia ya kubadilisha sera zake kuhusu Iraq. Ili kuzitetea sera zake ambazo zimethibitishwa kuwa zinashindwa na kubadilisha ufuatiliaji wa wananchi wa Marekani, alimfanya Bw. Maliki awe mtu wa kutupiwa lawama na kusema makosa yote yanatokana na uongozi mbaya wa Bw. Maliki. Na shambulio la Chama cha Democrat dhidi ya Bw. Maliki kwa kweli linailenga serikali ya Rais Bush na Chama cha Republican. Wanachama wa Chama cha Democrat wamegundua kwamba katika miezi miwili iliyopita mauaji ya kimadhehebu yamepungua, na baadhi ya vikundi vya madhehebu ya Suni vimeanza kushirikiana na jeshi la Marekani na kuanza kupinga mauaji yanayofanywa na kundi la Al-Qaida kulenga raia wasio na hatia. Kutokana na hali hiyo wanachama wa Chama cha Democrat wamehamishia nguvu zao kwenye mambo ya kisiasa kutoka mambo ya kijeshi, na serikali ya Maliki imekuwa shabaha yao.
Sababu ya Bw Maliki ya kutilia mkazo mashambulizi yake kwa watu wa Chama cha Democrat ni kuwa watu wa Chama cha Democratic wanataka kumwangusha kwa lengo la kuingia tena kwenye ikulu. Tarehe 26 alipojitetea alisema, "suluhisho la kisiasa unahitaji muda mrefu sana, na toka zamani serikali ya Iraq imeweka mpango wa kupata suluhisho wa kisiasa, lakini viongozi wa makundi mbalimbali ya Iraq hawawezi kuelewa." Serikali ya rais Bush pia iliwahi kujitetea kama hivyo, ikisema, "Bado tuko katika mwanzo wa kutekeleza sera mpya, mafanikio yaliyopatikana katika miezi kadhaa iliyopita yanaonesha kuwa hali ya Iraq inaweza kubadilika, hatuwezi kutamani hali ibadilike kwa usiku mmoja tu." Wachambuzi wanaona kuwa majibu ya Bw. Maliki kwa watu wa Chama cha Democrat yanalingana na mahitaji ya rais Bush katika matatizo fulani.
Kwanza, Bw. Maliki anahitaji kuungwa mkono na serikali ya Bw Bush, hataki sera za Marekani zibadilike kutokana na shinikizo la kisiasa nchini Marekani. Kuwashambulia watu wa Chama cha Democrat licha ya kuonesha kuwa Bw. Maliki anaunga mkono serikali ya Chama cha Republican kinachoongozwa Rais George Bush, na pia kunaiasa Marekani kwamba kama sera za Marekani zikibadilishwa kutokana na shinikizo la watu wa Chama cha Democrat, nguvu za makundi mbalimbali nchini Iraq zitavurugika na kusababisha serikali ya Iraq izame katika hali mbaya, na pia Iraq itafarakana zaidi.
Pili, Sababu ya Bw. Maliki kuthubutu kukabiliana uso kwa uso na watu wa Chama cha Democrat inatokana na mafanikio muhimu yaliyopatikana katika juhudi zake za kusukuma mbele usuluhisho wa kisiasa nchini Iraq. Viongozi wa madhehebu ya Shia, Suni na wa waKurd tarehe 26 walitangaza kuwa wamefikia makubaliano kuhusu hatua kadhaa muhimu za kusukuma mbele suluhisho la maafikiano ya kitaifa. Maendeleo ya mchakato wa suluhisho ni kigezo muhimu cha kupima hali ya kisiasa ya Iraq kilichowekwa na Marekani. Serikali ya Rais George Bush mara ilitoa pongezi na kusema "hayo ni mafanikio ya juhudi za pande zote kwa ajili ya maslahi ya watu wa Iraq."
Wachambuzi wanaona kuwa maendeleo ya mchakato wa usuluhisho wa kisiasa hakika yanasaidia sana kupunguza shinikizo la kuitaka serikali ya Bush iondoe jeshi kutoka Iraq, na serikali ya Bw. Maliki inaweza kuendelea kupata uungaji mkono na misaada kutoka Marekani, na serikali ya Chama cha Republican kinachoongozwa na Rais George Bush pia inaweza kujinasua kutoka katika hali mbaya ya kisiasa katika mapambano kati ya vyama viwili. Lakini cha muhimu ni kwamba, je ushirikiano kati ya Bw George Bush na Bw. Maliki unaweza kudumu kwa muda gani? Sera za serikali ya Bush kuhusu Iraq na serikali ya Bw. Maliki zinaweza kufika mbali kiasi gani? Na Mchakato wa usuluhisho unaweza kufika mbali kiasi gani?
Idhaa ya kiswahili 2007-08-28
|