Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-29 15:36:20    
Viongozi wa Palestina na Israel wajadili kwa mara ya kwanza hatma ya Palestina

cri

Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert tarehe 28 walikutana huko Jerusalem na kujadili masuala kuhusu hatma ya Palestina ikiwa ni pamoja na masuala ya mipaka, haki ya wakimbizi wa Palestina kurudi nyumbani na udhibiti wa mji wa Jerusalem. Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kujadili masuala hayo. Na mazungumzo yao pia ni maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa masuala ya Mashariki ya Kati utakaofanyika katika majira ya Autumn mwaka huu.

Kwa mujibu wa maelezo ya maofisa wa Palestina na Israel, viongozi hao walifanya mazungumzo peke yao kwa muda wa saa moja na nusu mjini Jerusalem. Ofisa mmoja mwandamizi wa ofisi ya waziri mkuu wa Israel alisema pande hizo mbili zilifanya majadiliano ya kina kuhusu masuala yanayotokea katika migogoro kati ya Palestina na Israel kwa mfano udhibiti wa mji wa Jerusalem na suala la wakimbizi wa Palestina. Ofisa mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema, pande mbili zinatumai kuwa zingeweza kufikia makubaliano kabla ya mwisho wa Oktoba na masuala hayo yatakuwa mada muhimu ya makubaliano hayo, ili kuweka msingi imara kwa ajili ya mkutano wa kimataifa wa masuala ya Mashariki ya Kati.

Vyombo vya habari vinaona kuwa mazungumzo kati ya Bw. Abbs na Olmert ni mazungumzo yaliyopata maendeleo makubwa kuliko mazungumzo yote yaliyofanyika katika miezi kadhaa iliyopita.

Vyombo vya habari vinaona kuwa mazungumzo kati ya Bw. Abbas na Olmert ni mazungumzo yaliyopata maendeleo makubwa kuliko mazungumzo yote yaliyofanyika katika miezi kadhaa iliyopita. Vyombo vya habari vinasema kabla ya hapo, pande mbili zilikuwa zinatofautiana kuhusu kujadili au kutojadili suala la hatma ya Palestina. Bw. Olmert alikataa kufanya mazungumzo yoyote kuhusu suala hilo, na Palestina ilikuwa inashikilia kufanya mazungumzo hayo. Kwenye mazungumzo ya tarehe 28 ingawa pande mbili hazikujadiliana sana masuala hayo matatu, lakini mazungumzo kuhusu masuala hayo yameanza. Ofisa wa Israel alisema Bw. Olmert atakutana na Bw. Abbas mara mbili au tatu ndani ya wiki kadhaa, na kisha pande mbili zitaunda kikundi cha utekelezaji na kuendelea na mazungumzo ili hatimaye zifikie makubaliano ya kimsingi.

Aidha, vyombo vya habari pia vinaona kuwa ingawa hali ya mambo inavyoendelea inasaidia mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, lakini kufanikisha mkutano huo kunahitaji safari ndefu. Kwanza, pande mbili zina matumaini tofauti kuhusu mkutano huo. Palestina inatumai kuwa pande mbili zingeweza kupata makubaliano ya makini. Mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Abbas alisema, kama mkutano huo ukishindwa kupata njia ya kutatua suala la hatma ya Palestina na kama utatoa "taarifa ya kikanuni" tu, basi mkutano huo ni wa "kupoteza wakati tu".

Mbali na hayo, hali ya kisiasa kati ya Palestina na Israel pia inaleta athari mbaya kwa ufanisi wa mkutano huo. Palestina iko katika hali ya mfarakano, kundi la Hamas linalodhibiti ukanda wa Gaza na kundi la Fatah linalodhibiti ukingo wa magharibi yanapingana na hayawezi kufikia makubaliano katika muda mfupi. Msemaji wa kundi la Hamas Bw. Abu Zuhri tarehe 28 alishutumu mazungumzo kati ya viongozi wa Palestina na Israel kuwa yana nia ya kulitenga kundi la Hamas, na kusema iwapo Israel ikiendelea kuikalia Palestina mazungumzo kama hayo hayawezi kufanikiwa. Zaidi ya hayo serikali ya Israel pia inapinga kabisa usuluhishi kati ya Bw. Abbas na Hamas, na kutishia kuwa kama Bw. Abbas atalihusisha kundi la Hamas kwenye serikali, basi Israel itasimamisha mazungumzo yote.

Kadhalika vyombo vya habari pia vinaona kuwa ingawa kuna changamoto nyingi, lakini pande mbalimbali zitakazoshiriki kwenye mkutano huo wa kimataifa zinaendelea kufanya juhudi ili kufanikisha mkutano huo, na hasa pande mbili za Palestina na Israel ambazo zinafanya juhudi kuwasiliana na zimepata maendeleo fulani. Nchi inayoitisha mkutano huo, Marekani, pia inashinikiza Palestina na Israel. Kabla ya mazungumzo hayo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliwasiliana na viongozi wa Palestina na Israel akisema atafanya ziara nchini Palestina na Israel kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa ili kuhakikisha mkutano unapata mafanikio.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-29