Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-30 15:29:01    
Watu waliojitolea kuwasaidia wengine wapata msaada

cri

Huko Changchun, mji wa kaskazini mashariki mwa China, kuna shirika moja la kiraia liitwalo shirika la kumsaidia Lei Feng, ambalo linatoa misaada ya hali na mali kwa watu wanaojitolea kuwasaidia wengine.

Lei Feng alikuwa askari wa jeshi la China, alifariki mwaka 1962 kwenye ajali alipokuwa na umri wa miaka 22 tu. Lakini alipokuwa hai alikuwa anawasaidia sana watu wengine kwa moyo wa dhati. Aliwahi kusema, "Maisha ya binadamu ni mafupi, lakini napenda kutumia muda wote wa maisha yangu katika kuwatumikia umma." Hadi hivi sasa, Lei Feng amekuwa ni mfano wa kuigwa katika jamii ya China, na jina lake pia ni tafsiri ya tabia nzuri za kuwasaidia wengine kwa upendo.

Mwazilishi wa "shirika la kumsaidia Lei Feng" ni Bw. Wu Shaoli aliyezaliwa mwaka 1956.

Bw. Wu alisema aliwakuta watu wengi wenye tabia ya kuwasaidia wengine kwa moyo wa dhati. Akikumbusha alisema "Nakumbuka siku moja ya miaka minane au tisa iliyopita, wakati huo nilikuwa naendesha teksi. Nilikumbwa na theluji kubwa na gurudumu la gari langu likapasuka. Mtu mmoja alinikuta, alisimama na kunisaidia kubadilisha gurudumu. Nilimshukuru sana, lakini baadaye nilishindwa kumpata. Wazo moja likanijia kwamba, nitakapokuwa na uwezo nitaanzisha shirika moja la kuwasaidia watu waliowahi kujitolea kuwasaidia wengine bila kudai malipo na wala hawataki majina yao kujulikana."

Mwezi Aprili mwaka 2006 Bw. Wu Shaoli alitoa Yuan elfu 50 kuanzisha "shirika la kumsaidia Lei Feng", ambalo ni la kwanza la namna hiyo nchini China.

Shirika hilo liliwavutia wafanyakazi wanaojitolea, ambao kwa kupitia vyombo vya habari na kufanya uchunguzi, walichagua watu wanaostahili kusaidiwa. Kwa kawaida hao ni watu waliojitolea kuwasaidia wengine, lakini wao wenyewe wanakabiliwa na shida au matatizo ya kifedha. Wafanyakazi wa shirika hilo wanawapelekea watu hao mahitaji ya maisha na fedha, na kuwatembelea mara kwa mara.

Mzee Yang Qingheng ni mkazi wa mji wa Changchun. Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, alikuwa anajitolea kufanya kazi mbalimbali kwenye mtaa wa makazi anakoishi, kama vile kukarabati barabara na kupanda maua, majani na miti. Bila kujali shida za kiuchumi zilizokuwa zinamkabili, mzee huyo alibana matumizi yake mwenyewe na kuwasaidia majirani waliokumbwa na matatizo ya kiuchumi. Shughuli alizofanya mzee Yang zililivutia "shirika la kumsaidia Lei Feng", ambalo lilimpelekea msaada wa Yuan 300 na vyakula vyenye virutubisho, pamoja na hati moja ya kumsifu.

Hivi sasa mzee Yang amejiunga na shirika hilo. Alisema "Hisia zangu ziliguswa sana na msaada wa shirika hilo, kwani jambo kama hilo halijawahi kutokea. Nilipofanya shughuli hizo nilikuwa sitarajii kupata faida yoyote. Nitafanya juhudi zaidi kutokana na upendo na ufuatiliaji wa jamii."

Katika muda wa mwaka mmoja, wafanyakazi wa "shirika la kumsaidia Lei Feng" walitembelea sehemu zote za mkoa wa Jilin ambao mji wa Changchun upo. Na watu zaidi ya 20 walikuwa wamesaidiwa na shirika hilo.

Shirika hilo lina wafanyakazi zaidi ya 60, ambao wote ni watu wanaojitolea. Miongoni mwao mkubwa zaidi ni mzee mwenye umri wa miaka 71 na mdogo zaidi ni mtoto mwenye umri wa miaka minane. Katika shughuli za shirika hilo wanaeneza upendo kwenye jamii, wao wenyewe pia wanapata furaha.

Mfanyakazi mmoja Bibi Guo Shuhua aliwahi kuwa mtoto yatima. Alisema tangu siku alipozaliwa, alikuwa anapata ufuatiliaji na upendo wa jamii, kwa hiyo aliamua kujiunga na shirika hilo, ili kueneza upendo kwa wengine kama alivyosaidiwa na wengine.

Alisema, "Kila ninapowaona watoto yatima na wale wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi, wananikumbusha siku zile nilipokuwa mtoto. Naona ninatakiwa kutoa upendo wangu kwa jamii. Sasa kwenye shirika hilo, tunashikamana kuwa kitu kimoja na kila mmoja anatoa mchango wake, fedha au nguo, tunaeneza upendo kwenye jamii. Hili ni jambo la maana."

Katika utamaduni wa China, kuwasaidia wengine kama alivyofanya Lei Feng ni vitendo visivyolenga kupata faida. Kwa hiyo watu Fulani walitia mashaka juu ya kitendo cha Bw. Wu Shaoli, walisema huenda kitapotosha vitendo vya kuwasaidia wengine. Bw. Wu alisema, "Baada ya kuingia kwenye zama za uchumi wa soko huria, limetokea pengo kati ya watu wenye matatizo ya kiuchumi na matajiri. Hivi sasa nina uwezo wa kuwasaidia, basi nawasaidia kwa kadiri ya uwezo wangu. Naona kufungamanisha vitu vya kimali na kihali, kunaweza kukamilisha mfumo wa uchumi wa soko huria. Naona tunatakiwa kuvumbua njia mpya katika shughuli za kuwasaidia wengine kama alivyofanya Lei Feng."

Kabla ya kumaliza mahojiano hayo, Bw. Wu alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi karibuni shirika lake litaanzisha tawi katika mji wa Tangshan, mkoani Hebei, kaskazini mwa China. Yeye ana matumaini kuwa, shirika hilo na shughuli zake zitasambazwa kote nchini China na kuenzi moyo wa Lei Feng kwenye jamii ya China.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-30