Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-30 19:50:08    
Suala la mateka wa Korea ya Kusini latazamiwa kutatuliwa kabisa

cri

Tarehe 29 kundi la Taliban kwa vikundi vitatu liliwaachia huru mateka 12 wa Korea ya Kusini. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa tarehe 28kati ya serikali ya Korea ya Kusini na kundi la Taliban, tarehe 30 mateka saba waliobaki wataachiwa huru. Hadi sasa suala la mateka wote wa Korea ya Kusini walioshikiliwa kwa wiki saba linatazamiwa kutatuliwa kabisa.

Tarehe 29 Wizara ya Mambo ya Nje na biashara ya Korea ya Kusini ilithibitisha kuwa siku hiyo kundi la Taliban kwanza liliwaachia huru mateka wanawake watatu, na alasiri liliwaachia huru mateka watano akiwemo mwanaume mmoja, mateka hao wote wako katika hali nzuri, baadaye Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilithibitisha kuwa siku hiyo kundi la Taliban liliwaachia huru mateka wengine wanne. Hivi sasa mateka hao 12 waliachiwa huru wamekabidhiwa kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kupitia mkuu mmoja wa kabila na baadaye kuikabidhi serikali ya Korea ya Kusini.

Kuachiwa huru kwa mateka 12 kumewafariji sana watu wa Korea ya Kusini, na jamaa wa mateka hao wamefurahi zaidi. Kaka wa mateka mmoja mwanamke alisema, wazazi wake wamefurahi sana na hata walipiga kelele "binti yetu atarudi!". Umoja wa Mataifa pia umefurahia tukio hilo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kusini alisema akiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametumia nguvu zake zote katika utatuzi wa suala la mateka hao, kwa hiyo aliposikia habari hiyo alifurahi mno.

Tarehe 29 naibu msemaji wa baraza la mawaziri la Marekani Bw. Tom Casey alisema amefurahishwa na kitendo cha Taliban kuwaachia huru mateka wa Korea ya Kusini baada ya mazungumzo kati ya Taliban na mjumbe wa serikali ya Korea ya Kusini. Alisisitiza kuwa kukataa kurudi nyuma katika mapambano dhidi ya ugaidi ni msimamo wa Marekani kwa siku zote. Alikanusha kuwa makubaliano ya kuwaachia huru mateka yana maana ya kwamba Korea ya Kusini inatambua uhalali wa kisiasa wa kundi la Taliban. Habari kutoka vyombo vya habari vya Marekani zinasema pande mbili za serikali ya Korea ya Kusini na kundi la Taliban zote zimekanusha kwamba kulikuwa na suala lolote la kifedha katika utatuzi wa suala hilo.

Suala la mateka wa Korea ya Kusini limekuwepo kwa wiki sita. Tarehe 19 Julai, watu wenye silaha wa kundi la Taliban waliwateka nyara watu 23 wa Korea ya Kusini kwenye barabara moja mkoani Ghazni. Kundi la Taliban liliitaka serikali ya Korea ya Kusini iondoe askari wake zaidi 200 kutoka Afghanistan, ama sivyo litawaua mateka hao. Baada ya tukio kuzuka, serikali ya Korea ya Kusini kwa upande mmoja iliahidi itaondoa askari wake kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa, kwa upande mwingine ilituma mjumbe kwenda Afghanistan kushughulika na tukio hilo. Baada ya tukio hilo kutokea serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban walifanya mazungumzo mara nyingi, lakini mazungumzo hayakupata mafanikio yoyote. Ndani ya kundi la Taliban kulikuwa na maoni tofauti, moja ilitaka kubadilisha mateka kwa watu wa Taliban waliofungwa na jeshi la muungano wa Marekani na Afghanistan, na nyingine ilitaka serikali ya Korea ya Kusini ilipe fedha nyingi. Kutokana na kuwa Marekani na serikali ya Afghanistan zinashikilia kutowaachia huru watu wa Taliban waliofungwa, kundi la Taliban liliwaua mateka wawili wanaume. Tarehe 10 Agosti kwa mara ya kwanza wajumbe wa Korea ya Kusini na Taliban walifanya mazungumzo ya ana kwa ana mjini Ghazni, tarehe 13 kundi la Taliban liliwaachia huru mateka wawili wanawake. Tarehe 27 jeshi la Korea ya Kusini lilisisitiza kuwa litaondoa askari wake 200 kutoka Afghanistan kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.

Tarehe 28 kwa mara nyingine tena pande mbili zilifanya mazungumzo mjini Ghazni na pande mbili zilifikia makubaliano ikiwa ni pamoja na kuondoa askari wa Korea ya Kusini kabla ya mwisho wa mwaka huu, kuondoa vikundi vyote vya huduma za jamii, kutotuma tena wamisionari na kuahidi kutotumia nguvu za kijeshi dhidi ya Taliban kabla ya mateka kuachiwa huru.

Wachambuzi wanaona kuwa utatuzi huu wa amani hauwezi kutengana na msimamo wa serikali ya Korea ya Kusini kushikilia njia ya amani, na huku kundi la Taliban linafahamu kwamba Korea ya Kusini haiwezi kukidhi mahitaji yake ya kubadilisha mateka kwa wafungwa ,na ikishikilia msimamo huo Taliban ingejikuta kwenye hali ya kusakamwa. Kwa hiyo kulegeza masharti lilikuwa ni chaguo la busara. Ukweli wa mambo umethibitisha kuwa mazungumzo ndio njia nzuri ya kutatua migogoro yote.