Waziri wa ulinzi wa Afrika ya kusini Bwana Mosiuoa Lekota tarehe 29 Agosti alisema kwenye Mkutano uliofanyika huko Cape Town, mji mkuu wa Afrika ya kusini kuwa, Bara la Afrika halifurahii kuwepo kwa jeshi la nchi za nje, hasa kupinga Marekani kujenga makao makuu ya jeshi lake barani Afrika yaliyo kama kituo chake cha kijeshi. Bwana Lekota alitangaza kuwa, jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika yenye nchi 14 wanachama zikiwemo Afrika ya kusini, Namibia na Zambia zimetoa uamuzi kuwa, nchi yoyote ya mwanachama wa umoja huo haitalipokea jeshi la Marekani.
Tarehe 6 Februali mwaka huu jeshi la Marekani lilitangaza kujenga makao makuu yake barani Afrika, ambayo yatashughulikia usimamizi na uratibu wa shughuli zote za kijeshi za Marekani barani Afrika isipokuwa Misri, na jeshi la Marekani linapanga kufanya ujenzi wa makao makuu hayo kuanzia tarehe 30 Septemba mwakani. Wizara ya ulinzi ya Marekani iliweka jukumu la makao makuu hayo ya jeshi la Marekani ni kufanya ushirikiano na nchi mbalimbali za Afrika na mashirika ya barani Afrika ili kuisaidia Afrika kujenga utulivu na usalama wa kikanda.
Marekani ikifanya vitendo vya kijeshi katika sehemu muhimu kwake kimkakati kama vile Afghanistan na Iraq inanyanyua juu bendera za "kupambana na ugaidi" na "kujenga utulivu na usalama wa kikanda". Kwa Marekani, nchi nyingi za Afrika ziko katika hali ya umaskini na vurugu za kivita kwa muda mrefu, na Bara la Afrika limekuwa sehemu zenye shughuli nyingi za ugaidi, hivyo kujenga makao makuu ya jeshi lake barani Afrika kunaweza kuzuia "nchi nyingine ya Afghanistan isijitokeze". Katika miaka kadhaa iliyopita, ujumbe wa wizara ya ulinzi ya Afrika siku zote umekuwa unafanya ziara katika nchi za Afrika, ili kuzishawishi nchi zinazohusika zikubali mpango wake huo. Lakini nia yake hiyo kweli ni ya peke yake tu.
Mwezi Machi mwaka huu, Algeria ilitangaza hadharani kuwa, haitairuhusu Marekani kujenga makao makuu ya jeshi lake kwenye ardhi ya nchi hiyo, pia haitakubali nchi yoyote kujenga kituo chake cha kijeshi nchini Algeria. Baadaye, Morocco na Libya pia zilieleza kupinga Marekani kujenga makao makuu ya jeshi lake kwenye ardhi za nchi hizo mbili. Aidha Algeria na Libya pia zilieleza wazi kupinga jeshi la Marekani kujenga makao makuu yake katika nchi yoyote ya jirani zao.
Na siku hizi nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika zote zinasusia hatua hiyo ya Marekani, hii imeonesha kuwa nchi za Afrika zimekuwa na msimamo wa pamoja siku hadi siku kuhusu hatua hiyo ya Marekani, kwani zimetambua nia halisi ya makao makuu ya jeshi la Marekani barani Afrika, kwamba kusudi halisi ni kuimarisha nguvu ya kijeshi ya Marekani barani Afrika ili kudhibiti maliasili za kimkakati barani Afrika.
Takwimu mpya zilizotolewa na serikali ya Marekani zimeonesha kuwa, mwaka 2006, kila siku Marekani iliagiza mafuta ghafi mapipa milioni 2.23 kwa siku kutoka barani Afrika, hivyo Afrika imekuwa sehemu kubwa kabisa kwa Marekani kuagiza mafuta ghafi. Wataalamu wa Marekani wamekadiria kuwa, ifikapo mwaka 2010, uzalishaji wa mafuta wa Afrika huenda utachukua zaidi ya asilimia 20 ya ule wa jumla wa dunia nzima, na asilimia 25 ya mafuta yatakayohitajiwa na Marekani katika miaka 10 ijayo itatoka kwenye sehemu za kusini mwa Sahara barani Afrika.
Kabla ya kuanzisha makao makuu ya jeshi barani Afrika, jeshi la Marekani limeongeza uingiliaji wake wa kijeshi barani Afrika kwa njia ya kufanya luteka za pamoja. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2006, Jumuiya ya NATO inayoongozwa na Marekani iliwahi kufanya luteka kubwa nchini Cape Verde, nchi ya visiwa vya Afrika ya magharibi, hii ni mara ya kwanza kwa majeshi ya NATO kufanya shughuli za kijeshi katika sehemu ya Afrika. Aidha, jeshi la Marekani limejenga kituo cha kudumu nchini Djibouti, ambapo limeweka jeshi lake lenye watu 1700 hivi ili kudhibiti sehemu ya mlango wa kuingia Bahari ya Sham na kutekeleza jukumu la kukusanya upelelezi wa mapambano dhidi ya ugaidi.
Nchi za Afrika siku zote zinashikilia kuwa masuala ya Afrika yapaswa kutatuliwa na waafrika wenyewe kupitia Umoja wa Afrika, na hayapaswi kuingiliwa na nchi za nje, ndiyo maana hakika zinaweza kupinga wazi hatua ya Marekani ya upanuzi wa kijeshi utakaonyang'anya maliasili chini ya kisingizio cha kupambana na ugaidi kote duniani.
|