Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-03 16:24:50    
Nyumba za jadi za wenyeji wa Beijing

cri

Nyumba zenye umaalumu zaidi za wakazi wa Beijing ni nyumba za kijadi za wenyeji wa Beijing, ambazo zinajengwa kuwa na pande nne za ua. Kutokana na ujenzi na matengenezo ya kupamba nyumba baada ya kuendelezwa katika miaka mia kadhaa iliyopita, nyumba hizo zimekuwa nyumba zenye mtindo maalumu wa kibeijing.

Hoteli ya Lusongyuan ya Beijing iko kwenye eneo la hifadhi ya utamaduni wa mji wa kale wa Beijing, hoteli hiyo ni nyumba yenye mtindo maalumu za kibeijing. Nyumba hiyo iliyojengwa kwa matofali na kuezekwa kwa vigae vya rangi ya kijivu inaonekana ya mtindo wa kizamani, viti vilivyotengenezwa kwa fito nyembamba vimewekwa kwenye mianzi na mizabibu iliyopandwa kwenye nyua wa nyumba hizo, ambavyo vinafanya nyumba hizo ziwe na umaalumu wa kijadi wa wenyeji wa Beijing. Meneja wa hoteli ya Lusongyuan, Bw. Wei Jinyuan alisema, nyumba hizo zilijengwa zamani sana, na zimehifadhiwa vizuri, zamani nyumba hizo zilikuwa za ndugu ya mfalme wa enzi ya Qing.

"Nyumba hizo zenye eneo la mita za mraba 2,400, zilijengwa miaka 150 iliyopita, nyumba hizo zina vyumba kiasi cha 60. Samani, utamaduni, mavazi, mapambo na chakula vyote ni vya jadi ya kibeijing. Wageni wanaokaa humo wengi ni kutoka nchi za Ulaya na Marekani, ambao wanafika Beijing kufanya utafiti kuhusu utamaduni wa kibejing."

Bw. Wei alisema, hoteli ya Lusongyuan si kama tu ina nyumba zenye mtindo wa jadi kibeijing, bali pia vyombo vilivyowekwa katika vyumba vyake ni tofauti, vikiwemo meza za kuwekea vinanda, makabati ya nguo, meza na viti vya mtindo wa kichina, taa za mtindo wa kale zilizofunikwa kwa kitamba cha hariri cha shashi na vitanda vilivyotengenezwa kwa mbao za aina ya mti mgumu unaojulikana kwa rosewood, pamoja na vyandarua vya mtindo wa kichina. Wafanyakazi wa hoteli hiyo wanavaa nguo walizokuwa wanavaa wenyeji wa mji wa Beijing mwanzoni mwa karne ya 20, ambao wanawafahamisha watalii mambo ya asili ya Beijing na kuwakaribisha chakula cha wenyeji wa Beijing. Ikiwa wageni wanataka, wao watawatembeleza kwenye vichochoro vya maeneo ya karibu ya makazi ya jadi.

Kila mwaka wageni wanafika kwenye hoteli ya Lusongyuan, vyumba vya hoteli hiyo vinapaswa kuagizwa kabla, katika baadhi ya nyakati vinapaswa kuagizwa kabla ya mwezi mmoja. Bw. Aronud Teissier kutoka Ufaransa ni mara ya kwanza kwake kutembelea Beijing, kutokana na ushauri wa rafiki yake, yeye na mchumba wake walichagua hoteli ya Lusongyuan, na wameridhika kabisa baada ya kufika huko.

"Likizo yetu ilikuwa ya furaha sana katika hoteli ya Lusongyuan yenye umaalumu wa kibeijing. Wafanyakazi wa hoteli hiyo wanatuhudumia vizuri sana, tena kila mmoja wao anapenda kutusaidia. Ikilinganishwa na sehemu nyingine za Beijing, wafanyakazi wa hoteli hiyo wanazungumza vizuri lugha ya Kingereza. Mazingira ya hoteli hiyo yanakaribia kiwango cha hoteli nzuri duniani, na hatuwezi kusahau wakati mzuri tuliokaa kwenye hoteli hiyo."

Kama alivyosema Bw. Aronud Teissier, watalii wengi wanaotoka sehemu mbalimbali duniani na kuishi katika hoteli hiyo, wanataka kujaribu maisha ya asili ya wenyeji wa Beijing. Huko unaweza kuona mara kwa mara watalii wakiota jua huku wakishika chupa za bia au vikombe vya kahawa, au wakisoma na kucheza chess kwenye ua wa matofali ya rangi ya kijivu, na kustarehe katika mazingira tulivu. Bibi Zhang Yan aliyefanya kazi huko kwa karibu miaka 20, bado anakumbuka hali aliyoiona kwenye hoteli ya Lusongyuan wakati alipokuja Bw. Seiji Qzawa, mwongoza bendi maarufu kutoka Japan wakati aliposhiriki kwenye maonesho ya muziki ya Beijing.

"Alisema, 'endapo ninakaa kwenye hoteli ya kiwango cha juu zaidi, sitajua mahali nilipo baada ya kuamka kutoka usingizini, kwani ni namna moja tu katika nchi yoyote ile. Ni hapa tu, baada ya kuamka, ninajua niko China.' Hapa tunazingatia sana mazingira ya kizamani, mazingira maalumu ya kiutamaduni na kuzingatia umaalumu wa wenyeji wa zamani wa Beijing."

Wasikilizaji wapendwa, sasa tunawafahamisha kuhusu hoteli nyingine ijulikanayo kwa jina la Chunqiuyuan, ambayo inaonekana kama nyumba za wakazi zenye ukimya mwingi. Hoteli ya Chunqiuyuan, ambayo iko katika sehemu ya magharibi ya Beijing, ni nyumba ya mtindo wa jadi ya wenyeji wa Beijing yenye ua katikati ya nyumba iliyojengwa kwa kuzungushiwa hoteli hiyo ina vyumba vinane tu vya wageni. Kwenye ua wa hoteli hiyo kuna mipera, vyungu vikubwa vya kufugia samaki za kuangalia wenye rangi ya dhahabu, pamoja na mfereji na vilima vya mandhari. Meneja wa hoteli ya Chunqiuyuan Bw. Zhu Jinsheng alizaliwa na kukua katika nyumba hiyo, na alikuwa na ufahamu mkubwa kuhusu nyumba za jadi za wenyeji wa Beijing, alisema hoteli ya Chunqiuyuan imedumisha mtindo wa nyumba za jadi za wenyeji wa Beijing na pia imedumisha mtindo wa maisha wa jadi wa wenyeji wa Beijing.

"Umaalumu mkubwa wa nyumba za jadi za wenyeji wa Beijing ni kupanda mipera, kuweka vyumba vikubwa vya kufugia samaki wenye rangi ya dhahabu na kufuga mbwa kwenye ua wa nyumba. Kwa kawaida mlango wa nyumba za aina hiyo uko kwenye kona ya kusini mashariki, wanaamini kuwa inawaletea bahati nzuri, vyumba vyenye milango inayoelekea upande wa kusini ni vya wenye nyumba, chumba cha upande wa mashariki ni jiko, chumba cha upande wa kusini ni msalani, baadhi ya nyumba za jadi za wenyeji kuna chumba kilichojengwa kwenye upande wa magharibi, ambazo ni kwa ajili ya watoto wao."

Vyumba vya hoteli ya Chunqiuyuan si vikubwa, lakini vimejengwa kwa ufundi mkubwa, nguzo na boriti za nyumba huchorwa michoro mizuri kwa rangi za aina mbalimbali. Hata magogo yanayotumika katika kujenga nyumba yanapitia mchakato wa kazi za aina 13 kwa kufuata mbinu ya zamani, ambayo hayapasuki hata baada ya kupita miaka mingi. Kwenye chumba cha kulala, kuna kitanda kilichochongwa nakshi nzuri za kupendeza, shuka la kitandani lina picha nzuri iliyotarizwa kwa nyuzi za hariri, na mavazi ya kulalia pia ni ya kitambaa cha hariri, wageni wakikaa kwenye hoteli za namna hiyo, watajisikia raha ya maisha ya wenyeji wa Beijing.

Hoteli ya Chunqiuyuan ina chumba cha kuwekea vitu na picha nyingi kuhusu maisha ya wenyeji wa Beijing zikiwemo nguo zinazovaliwa na maharusi katika sherehe, ambazo zinaonesha umaalumu wa maisha ya wenyeji wa Beijing wa zamani. Katika hoteli hiyo, wageni wanaweza kupiga picha wakiwa wamevaa nguo za wenyeji wa zamani wa Beijing, kushiriki kwenye shughuli zilizoandaliwa na hoteli zikiwemo kuangalia kazi ya sanaa ya ukataji karatasi, utarizi, kutengeneza sanamu kwa unga maalumu, na sanamu zenye uwazi katikati zilizopulizwa kwa uji wa sukari zilizoyeyushwa, tena wanaweza kujaribu wao wenyewe.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-03