Mkutano wa pili wa Marekani na Korea ya Kaskazini ulimalizika alasiri ya tarehe 2 mwezi Septemba huko Geneva, Uswisi. Mwakilishi wa kwanza wa Marekani kwenye mazungumzo ya pande sita ambaye ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje Bw. Christopher Hill alisema, Korea ya Kaskazini imekubali kuripoti mpango wake wa nyukilia na kuondoa uwezo wa zana zake zote za nyukilia kabla ya mwishoni mwa mwaka huu. Anaona kuwa hayo ni makubaliano muhimu sana, na pia ratiba iliyotolewa mara ya kwanza katika utekelezaji wa mpango wa kuondoa silaha za nyukilia wa kipindi cha pili wa Korea ya Kaskazini.
Mazungumzo hayo yalianza saa 4 ya tarehe 1 asubuhi, ambayo yatafanyika kwa siku mbili kwenye maskani ya ujumbe wa Marekani na wa Korea ya Kaskazini mjini Geneva. Wawakilishi 9 wa Marekani na wawakilishi 8 wa Korea ya Kaskazini walishiriki kwenye mazungumzo hayo. Kikundi cha utekelezaji wa pande mbili za Korea ya Kaskazini na Marekani, ni moja ya vikundi vitano vilivyoko chini ya mazungumzo ya pande sita kuhusu suala la nyukilia la peninsula ya Korea. Kutokana na mpango uliowekwa, mazungumzo ya safari hiyo yanahusu mambo mawili. La kwanza ni kujadili kuhusu Korea ya Kaskazini kutoa ripoti kamili kuhusu mpango wake wa nyukilia na kutekeleza mpango wa kuondoa nyukilia wa kipindi cha pili wa kuondoa uwezo wa zana zake za nyukilia kwa kufuata "waraka wa pande mbili wa tarehe 13 Februari"; La pili ni kujadili suala la kurudisha uhusiano wa kawaida wa nchi hizo mbili, ambalo Marekani itafuta jina la nchi ya Korea ya Kaskazini katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Marekani ilieleza msimamo wake na kuishinikiza Korea ya Kaskazini. Bw. Hill alisema baada ya Korea ya Kaskazini kuacha mpango wake wa silaha za nyukilia mambo mengi yatawezekana, lakini endapo mafanikio katika kuacha silaha za nyukilia hayataonekana, basi uhusiano kati ya pande hizo mbili hautaweza kuboreshwa kimsingi. Alisema hatua za kufanya uhusiano uwe wa kawaida hazitatekelezwa vizuri kabla ya Korea ya Kaskazini kutoa ripoti kamili kuhusu mpango wake wa nyukilia, na kuondoa uwezo wa zana zake za nyukilia.
Baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya siku ya kwanza, Bw Hill alikutana na waandishi wa habari, na alisema mazungumzo yalikuwa na maendeleo makubwa. Ingawa Korea ya Kaskazini haikushiriki kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, lakini mwakilishi wa kwanza wa ujumbe wa Korea Kaskazini ambaye ni naibu waziri wa mambo ya nje Bw. Kim Kye-Gwan alipojibu swali la mwandishi wa habari nje ya mkutano huo alisema, "Mazungumzo yaliendelea vizuri, na wanatarajia kupata mafanikio."
Kutokana na ratiba iliyotolewa na Marekani, mazungumzo hayo yangemalizika tarehe 2 adhuhuri, lakini mazungumzo yao yaliendelea mpaka zaidi ya saa kumi. Sawa na siku iliyotangulia, Bw Hill aliitisha tena mkutano na waandishi wa habari baada ya kurudi kwenye maskani ya ujumbe wa Marekani. Alisema "Tumekubaliana kuhusu Korea ya Kaskazini kutoa ripoti kamili kuhusu mpango wa nyukilia na kuondoa uwezo wa zana zake za nyukilia kabla ya mwishoni mwa mwaka huu."
Bw Hill alisema maendeleo hayo ni muhimu sana, ambayo yatasawazisha njia ya kufanikisha mazungumzo ya pande sita ya kipindi kijacho yatakayofanyika Beijing. Bw Hill alisema suala la nyukilia la peninsula ya Korea hakika litatatuliwa kwenye mazungumzo ya pande sita. Mchakato wa kufanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na silaha za nyukilia siyo wa pande mbili za Marekani na Korea ya Kaskazini, kutimiza lengo hilo kunahitaji jitihada za pande sita. Aliishukuru China kwa mchango wake kuhusu mazungumzo ya pande sita.
Kuhusu ratiba iliyotangazwa na Bw Hill, Korea ya Kaskazini haikusema wazi kuhusu mpango huo, mwakilishi wa Korea Kaskazini Bw Kim Kye-gwan alisema, pande mbili ziliafikiana kuhusu mambo mengi, alisema Korea ya kaskazini imeeleza wazi kuhusu kufanya ushirikiano, hivyo inastahili kupewa fidia za kisiasa na kiuchumi. Aliongeza kuwa fidia ya kisiasa ni kubadilisha sera ya uhasama dhidi ya Korea ya Kaskazini, na fidia ya kiuchumi ni pamoja na msaada wa nishati na umeme.
|