Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-03 16:53:04    
Moja ya mbinu 36: Kumshawishi chui aondoke kwenye mlima wake

cri

Nchini China, watu wanaona chui ni "mfalme wa wanyama", na katika zama za kale, mara kwa mara chui walikuwa wanakula watu. Ili kuwaangamiza, watu walikuwa wanatumia mbinu ya kuwafanya chui waondoke milima yao ili wapoteze tegemeo lao. Baadaye watu wanaiita mbinu hiyo kuwa ni "kumshawishi chui aondoke kwenye mlima wake" ikimaanisha kuwashawishi maadui waondoke kwenye kambi yao wanayoitegemea ili kuwashinda.

Kitabu cha kale cha "Mbinu za Kivita" cha Sun Zi kunaeleza kuwa, ni kitendo cha kijinga kushambulia ngome bila kuzingatia hali yako na ya maadui. Kwani maadui wanakuwa wamepata sehemu nzuri ya kufanyia mapambano na wanakuwa tayari kwa mapambano dhidi yako, wakati huo haifai kupambana nao moja kwa moja. Mbinu sahihi ni kuwashawishi maadui kwa chambo, ili waondoke kwenye sehemu yao waliyojiimarisha kwa ulinzi, hivyo hali yako iliyozidiwa na maadui itakuwa nzuri baada ya maadui kuacha ngome yao. Katika historia ya China kuna mifano mingi ya kutumia mbinu hiyo katika vita.

Mwanzoni mwa karne ya pili, China ilikuwa katika kipindi cha madola matatu ya kifalme Wei, Shu na Wu. Katika kipindi hicho wababe wa vita walipambana ili kupanua maeneo waliyotawala. Mbabe wa vita wa dola la Wu jemadari Sun Ce aliumezea mate mji wa Lujiang, mji ambao ulikuwa muhimu kwa vita kwa sababu kijiografia, ilikuwa ni rahisi kufanya mashambulizi kutoka kwenye mji huo, na ilikuwa vigumu kushambuliwa. Mbabe wa vita aliyeukalia mji huo jemadari Liu Xun alikuwa na tamaa nyingi kutokana na nguvu zake kubwa za kijeshi. Sun Ce alielewa fika kuwa akipambana moja kwa moja na Liu Xun hakika atashindwa. Alishauriana na maofisa wenzake na kuamua kutumia mbinu ya "kumshawishi chui aondoke kwenye mlima wake". Kutokana na kuwa Liu Xun alikuwa ni mtu mwenye uchu wa zawadi, Sun Ce alituma mtu kwenda kumpa Liu Xun zawadi nono, na kwenye barua alimsifu sana na kutaka kuwa rafiki yake, huku aliomba msaada kutoka kwa Liu Xun kutokana na nguvu yake ilikuwa dhaifu. Alisema, jemadari wa sehemu ya Shangliao mara kwa mara alimshambulia, lakini kutokana na nguvu yake dhaifu alishindwa kupambana nao, aliomba Liu Xun atume askari kumwadhibu. Jemadari Liu Xun alifurahi sana kwa kusifiwa na kuheshimiwa hivyo, na Shangliao kweli ni sehemu tajiri, na Liu Xun alikuwa akiitamani kwa siku nyingi, baada ya kusoma barua ya Sun Ce, Liu Xun aliamua kuishambulia sehemu ya Shangliao. Msaidizi Liu Hua alimshawishi Liu Xun aache nia hiyo, lakini Liu Xun hakusikia, kwani wakati huo alikuwa amevimba kichwa kwa kupata zawadi kubwa na kusifiwa kwa maneno matamu. Sun Ce alisubiri kwa hamu na alipopata habari kwamba Liu Xun aliondoka mji wa Lujiang na askari wake elfu kumi kadhaa kwenda kuishambulia Shangliao, alifurahi sana kwa kuwa mji wa Lujiang ulikuwa umebaki tupu. Kwa haraka bila kuchelewa aliushambulia mji huo na kuunyakua bila upinzani wowote. Liu Xun aliishambulia Shangliao kwa siku nyingi bila kushinda. Alipofahamu kwamba Sun Ce ameuteka mji wa Lujiang alijuta sana, lakini majuto ni mjukuu, alikuwa hana la kufanya ila kwenda kujisalimisha kwa dola jingine.

Katika zama hizi, mbinu hiyo pia inatumika mara nyingi. Katika miaka ya 40 ya karne iliyopita, Japan ilianzisha vita dhidi ya China. Kwa kutegemea zana bora za kisilaha, jeshi la Japan lilinyakua maeneo mengi muhimu nchini China na kujenga ngome zake wakati ambapo jeshi la wananchi lililoongozwa na Chama cha Kikomunisti cha China lilikuwa haliwezi kupambana na wavamizi wa Japan moja kwa moja kutokana na hali mbaya ya kisilaha. Ili kuwaua askari wa Japan jeshi la wananchi lilitumia kila njia ili kuwafanya maadui waondoke kutoka kwenye ngome zao na kuwaangamiza kikundi kwa kikundi kwa vita vya msituni.

Hapo nyuma tuliwahi kueleza mbinu za "Kufanya kishindo upande wa mashariki na kushambulia upande wa magharibi" na "Kuliokoa dola la Zhao kwa kulizingira dola la Wei", mbinu ya "kumshawishi chui aondoke kwenye mlima wake" inafanana na mbinu hizo mbili. Mbinu ya "kufanya kishindo upande wa mashariki na kushambulia upande wa magharibi" ina maana ya kuwababaisha maadui na kuwazamisha katika hali mbaya; na mbinu ya "kuliokoa dola la Zhao kwa kulizingira dola la Wei" ina maana ya kukwepa kupambana na nguvu kubwa ya maadui moja kwa moja na kuishambulia sehemu yake yenye nguvu dhaifu ili kuwanasa maadui na kupata ushindi. Mbinu hiyo ya "kumshawishi chui aondoke kwenye mlima wake" pia ina maana ya kuwaondoa maadui kutoka kwenye mazingira wanayotegemea ili uwashinde, yaani kuwaondoa kwanza na kuwaangamiza baadaye.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-03