Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-05 15:08:03    
Wakulima wa China watumia dawa kwa usalama na urahisi zaidi

cri

Katika muda mrefu uliopita, dawa zimekuwa hazipatikani kwa urahisi kwenye baadhi ya sehemu za vijiji nchini China. Kubaki nyuma kiuchumi, kuwa mbali na kusambaa kwa watu ni sababu kubwa inayofanya vijiji vingi visiwe na maduka ya dawa. Lakini kwenye sehemu zenye maduka ya dawa, matatizo mengi yapo katika shughuli za usambazaji wa dawa na uhakikisho wa sifa ya dawa.

Ili kuwawezesha wakulima watumie dawa kwa urahisi na kwa usalama, mwaka 2003, serikali ya China iliweka mpango wa kuanzisha mitandao miwili ya utoaji na usimamizi wa dawa vijijini. Baada ya miaka minne, je matatizo hayo bado yapo au yameondolewa? Hivi karibuni, mwandishi wetu wa habari alitembelea baadhi ya sehemu za vijijini na kuangalia hali hiyo.

Kijiji cha Nanmafang kiko mjini Zibo mkoani Shandong, kijiji hicho kina wakazi elfu moja tu. Zamani kijiji hicho kilikuwa hakina duka la dawa, wanakijiji walikuwa wanapaswa kwenda kwenye wilaya au vijiji vya jirani kununua dawa. Mwaka 2004 mwanakijiji Bi. Xie Jinhong alianzisha duka pekee katika kijiji hicho. Alisema:

"nilianzisha duka hilo kwa kuwa serikali imetoa sera ya kuondoa kodi kwa shughuli hiyo. Nilipanga nyumba hii kwa bei rahisi, Yuan mia moja tu kwa mwezi, duka hilo halitumii maji, na gharama za umeme ni Yuan 2 tu kwa mwezi, hakuna gharama nyingine."

Sera anayoitaja Bi. Xie Jinhong ni hatua iliyochukuliwa na serikali ya mji wa Zibo kuondoa kodi mbalimbali kwa watu walioanzisha maduka madogo ya dawa kwenye tafara au vijiji. Pato la jumla la duka la Bi. Xie Jinhong ni Yuan elfu 5 au 6 kwa mwaka. Wakati hakuna shughuli nyingi, pia anaweza kufanya kazi za shambani. Bi. Xie anaridhika na shughuli zake na jirani yake mama Li Junfeng pia anafurahia shughuli hiyo. Kumbe mume wa mama Li ana magonjwa ya mishipa ya damu kwenye ubongo na kisukari, na ni lazima aendelee kutumia dawa. Duka hilo limemletea urahisi sana. Mama Li alisema:

"zamani nilikuwa ninaenda kwa baiskeli kwenye kijiji jirani cha Xiguan kilichoko kilomita 2 tu kutoka kijiji kwetu ili kununua dawa. Tangu Bi. Xie aanzishe duka hilo, nanunua dawa katika duka lake."

Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa chakula na dawa ya mji wa Zibo Bw. Wang Mouchang alisema, hivi sasa mji huo umeanzisha maduka 2,200 madogo ya dawa kwenye tarafa na vijiji vyenye idadi ndogo ya watu. Dawa zinazouzwa katika maduka hayo zinatolewa moja kwa moja na makampuni ya biashara ya jumla ya dawa yanayotimiza masharti husika, hali hiyo imepunguza utaratibu wa usambazaji na pia kupunguza kiasi bei ya dawa. Hivi sasa mtandao wa usambazaji wa dawa vijijini unahusisha asilimia 98 ya vijiji mjini Zibo.

Wakati wa kuanzisha maduka ya dawa vijijini, serikali ya mji huo pia imeimarisha ukaguzi na usimamizi wa sifa ya dawa. Zamani idara za usimamizi wa dawa mjini humo zinafikia mpaka ngazi ya wilaya tu, lakini hivi sasa idara hizo pia zimeanzishwa katika tarafa na serikali pia imewaajiri watu 3000 wa huko kusaidia kazi ya usimamizi wa dawa vijijini na kutoa ruzuku kwa watu waliotoa ripoti kuhusu dawa bandia. Hatua hizo zimeleta mabadiliko mazuri. Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa chakula na dawa ya wilaya ya Fenghuang mjini Zibo Bw. Bian Liguo alisema,

'tangu tulipoanza kuchukua hatua hizo, wachuuzi wa dawa bandia hawaji tena. Zamani walikuwa wako wengi sana na walikuja wakiwa wamebeba mifuko au kusukuma baiskeli, lakini hivi sasa hawapo tena."

Kwenye sehemu inayojiendesha ya kabila la Wazhuang ya Guangxi, ujenzi wa mitandao ya usambazaji na usimamizi wa dawa vijijini pia umepata maendeleo. Kwa mfano kwenye wilaya ya Jingxi mjini Baise na wilaya ya Lipu mjini Guilin, mitandao hiyo yote miwili inahusisha kila sehemu katika wilaya hizo. Tofauti na hali ilivyokuwa mkoani Shandong, kutokana na matatizo ya mawasiliano barabarani yanayoathiri shughuli za usambazaji wa dawa mkoani humo, serikali ya huko imechukua hatua za kisera kuyahamasisha makampuni kujenga mtandao wa usambazaji wa dawa unaofunika sehemu zote za vijijini.

Katika wilaya ya Lipu mjini Guilin, kuna kijiji kimoja cha Huangzu ambacho kiko mbali sana kutoka wilaya, wakazi wa huko wakitaka kwenda wilayani, lazima watembee kwa miguu kwa saa mbili, halafu kupanda  mashua kwa saa mbili na kupanda gari kwa saa moja. ili kuhakikisha utoaji wa dawa kwenye vijiji vya mbali kama hicho, kutokana na kazi ya uratibu wa serikali ya huko, kampuni moja ya huko ilisaini mkataba na vituo zaidi ya 140 vya usambazaji wa dawa kote wilayani na kuwajibika na kazi zote za usambazaji wa dawa katika wilaya hiyo. Maneja wa kampuni hiyo Bw. Guo Deliang alisema,

"Kampuni yetu inasambaza dawa kwa vijiji vyote wilayani, vikubwa au vidogo, vyote tunavishughulikia kwa usawa."

Bw. Guo alisema, kwa ujumla shughuli hizo zinanufaisha pande zote mbili za serikali na kampuni. Mabadiliko yaliyotokea mkoani Shandong na Guanxi ni mfano wa hali ilivyo nchini China. Msemaji wa idara kuu ya usimamizi wa chakula na dawa ya China Bi. Yan Jiangying alisema, ili kusaidia kuendeleza na kuimarisha vituo vya usambazaji wa dawa kwenye vijiji vya mbali, serikali za sehemu mbalimbali zimeweka sera kuhamasisha vijiji na wilaya zijenge vituo hivyo. Pamoja na hayo, mitandao ya usimamizi wa dawa katika ngazi tatu za wilaya, tarafa na vijiji inafikia hatua kwa hatua sehemu zote za vijijini nchini China, wachuuzi wa dawa bandia na hali ya matumizi ya dawa zilizopitwa na wakati zimepungua sana. Hivi sasa vituo vya afya na maduka mengi ya dawa vijijini yamejiunga na mtandao wa usambazaji wa dawa, hali hiyo imehakikisha zaidi sifa ya dawa zinazopatikana vijijini. Katika siku za baadaye, idara husika za serikali ya China zitaendelea kufanya juhudi ili kuwawezesha wakulima watumie dawa kwa usalama na urahisi zaidi. Bi. Yan alisema:

"kutokana na juhudi za miaka ya karibuni, hivi sasa asilimia 85 ya vijiji vyote zaidi ya laki 6 kote nchini China vimejiunga na mtandao wa usimamizi na usambazaji wa dawa. Usalama wa matumizi ya dawa kwa wakulima umehakikishwa ipasavyo. Tunapanga kuwa, ifikapo mwaka 2010, mtandao wa usambazaji wa dawa utavifikia vijiji vyote na mtandao wa usimamizi wa dawa pia utaimarishwa zaidi."

Idhaa ya kiswahili 2007-09-05