Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-04 17:20:10    
Ban Ki-moon afanya ziara kwenye nchi tatu za Afrika ili kusukuma mchakato wa kisiasa wa Darfur

cri

Kuanzia tarehe 3 katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon ameanza kufanya ziara rasmi ya siku sita nchini Sudan na nchi jirani Chad na Libya. Tangu Bw. Ban Ki-moon awe katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa siku zote ana matumaini ya mafanikio fulani kwa juhudi zake katika utatuzi wa suala la Darfur. Kwenye mkutano wa kimataifa uliofanyika mjini Arusha mwanzoni mwa mwezi Agosti, wajumbe wa makundi kadhaa ya upinzani walikubali kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan kwa msimamo mmoja katika muda wa miezi miwili hadi mitatu, hali hiyo ilileta matumaini mapya kuhusu utatuzi wa suala la Darfur kwa njia ya amani. Bw. Ban Ki-moon anadhamiria kuimarisha zaidi mafanikio hayo ya mkutano wa Arusha na kusukuma zaidi mchakato wa kutatua suala la Darfur. Ziara ya yake katika nchi hizo tatu inalenga hasa masuala matatu ikiwa ni pamoja na kusukuma mchakato wa kisiasa unaoshirikishwa na pande mbalimbali, suala la kupanga jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na suala la wakimbizi.

Kwanza ni kusukuma mchakato wa kisiasa wa Darfur na kuhimiza pande mbalimbali zirudishe mazungumzo. Kutokana na nia yake hiyo, akiwa nchini Sudan atakwenda kwenye sehemu ya Darfur na kutembelea kambi za wakimbizi na pia kufanya mazungumzo na rais Omar al-Bashir wa Sudan. Kadhalika atakutana na viongozi kadhaa wa sehemu ya Darfur na kuwahimiza waheshimu makubaliano ya amani yaliyopo. Atakapokuwa ziarani nchini Libya Bw. Ban Ki-moon atamwomba kiongozi wa Libya aendelee na juhudi zake ili kuzifanya pande mbalimbali zirudishe mazungumzo.

Pili, kufanya maandalizi kwa ajili ya kupanga jeshi la mseto lenye askari elfu 26 la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Kutuma jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ni hatua ya Umoja wa Mataifa inayochukuliwa kwenye maeneo yenye hali ya utatanishi. Kutokana na mazingira mabaya ya usalama, uhaba wa maji na hali duni ya mawasiliano ya habari, hatua hiyo haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na serikali ya Sudan. Kwa hiyo katika ziara yake nchini Sudan atahimiza serikali ya Sudan kutoa ushirikiano.

Tatu, kuzishawishi pande husika zitoe ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kuwasaidia wakimbizi waweze kurudi nyumbani. Bw. Ban Ki-moon atatembelea Chad ambayo imepokea wakimbizi wa Darfur zaidi ya laki mbili, nia ya kutembelea nchi hiyo ni kuishawishiiweze kuwasaidia zaidi wakimbizi wanaopangwa na Umoja wa Mataifa.

Wachambuzi wanaona kuwa tatizo la wakimbizi na kupanga jeshi la kulinda amani ni haja ya utatuzi wa suala la Darfur, lakini sharti la kwanza na la msingi la kutatua suala la Darfur kwa amani, ni kusukuma mchakato wa kisiasa wa Darfur. Kwa hiyo kurudisha mapema mazungumzo ya pande mbalimbali ni lengo kuu la ziara ya Bw. Ban Ki-moon. Lakini Bw. Ban Ki-moon ni wazi amechukua tahadhari katika ziara yake ya nchi hizo tatu za Afrika. Msaidizi wake alisema, ziara yake haina uhusiano na nia ya kupata "maendeleo ya hatua kubwa" na hivi sasa sio kipindi cha kupata "maendeleo ya hatua kubwa".

Wachambuzi wanaona kuwa hii inaonesha kuwa Bw. Ban Ki-moon anatambua kwa busara utatanishi wa suala la Darfur. Hivi sasa katika sehemu ya Darfur kuna makundi zaidi ya kumi yanayoipinga serikali, na kila kundi lina matakwa yake kuhusu ugawaji wa madaraka na maliasili, hali hiyo ikiwa pamoja na mvutano unaoendelea kati ya makundi hayo, tofauti kati yao inazidi kuwa kubwa katika masuala ya ugawaji wa madaraka na maliasili, hatua za usalama, ardhi na misaada ya kibinadamu. Na matatizo yote hayo kwa pamoja yanampasa Bw. Ban Ki-moon achukue tahadhari kuwa makini zaidi katika ziara yake.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-04