Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-05 15:11:15    
Je "ramani ya amani ya Iraq" inaweza kuiletea Iraq amani?

cri

Wajumbe wa madhehebu ya Shia na Suni hivi karibuni walifanya mazungumzo ya faragha kwa siku nne nchini Finland na wametunga "ramani ya amani ya Iraq", pande mbili ziliahidi kuwa zitafanya juhudi bila kusita ili kuleta utatuzi wa kudumu wa migogoro nchini Iraq. Wachambuzi wanaona kuwa, wajumbe wa madhehebu mawili kuweza kufikia makubaliano kuhusu suala la Iraq bila ushiriki wa Marekani, ni ishara nzuri kwa watu wa Iraq wanaotamani kujiamulia mustakbali wa taifa lao.

Viongozi wakubwa 16 kutoka madhehebu ya Shia na Suni na wajumbe wa Wakurd walifanya mazungumzo ya faragha kwa siku nne huko Finland, na wajumbe kutoka Ireland Kaskazini na Afrika Kusini walikaribishwa kueleza uzoefu wa michakato yao ya amani kwa lengo la kutafuta njia ya kutatua migogoro kati madhehebu ya Kiislamu. Tarehe 3 mkutano huo ulitangaza waraka uitwao "Makubaliano ya Helsinki" ambayo yametoa mapendekezo 12 na malengo 9 ya kisiasa ikiwemo hatua za kila aina zichukuliwe ili kukomesha vitendo vya mabavu na kutatua matatizo ya kisiasa kwa njia ya amani na ya kidemokrasia. Na katika mchakato wa mazungumzo ni marufuku kwa makundi yote kutumia mabavu na kuanzisha kamati inayokubaliwa na vyama vyote vya kisiasa ili kusimamia mchakato wa kuvunja makundi yenye silaha yasiyo ya serikali. Washiriki wa mazungumzo hayo waliahidi kuendelea na majadiliano kwenye msingi huo ili kuanzisha mazungumzo yanayolenga kufikia mafikiano ya kitaifa.

Wachambuzi wanaona kuwa waraka huo ambao unaitwa "ramani ya amani ya Iraq" umeingiza kanuni za kimsingi za mchakato wa amani wa Ireland ya Kaskazini, na umebaini malengo ya kipindi ya "kukomesha vitendo vya nguvu" na "kuacha silaha". Kama kweli makundi ya madhehebu ya Shia na Suni yanaweza "kusimamisha vita daima", yataleta mazingira ya kimsingi kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa maafikiano ya kitaifa. Lakini wachambuzi wanaona kuwa hivi sasa ni vigumu sana kukomesha vitendo vya mabavu, na lengo la "kuacha silaha" linakabiliwa na changamoto kubwa.

Kwanza, ndani ya madhehebu ya Shia na Suni kuna vikundi vingi vyenye misimamo tofauti na kila kikundi kina jeshi lake, hali hiyo ikiwa pamoja na "kujipenyeza kwa kundi la Al-Qaida" lengo la kukomesha vitendo vya mabavu na kuacha silaha ni vigumu sana kutimizwa.

Pili, kuwepo kwa majeshi ya nchi za nje nchini Iraq ni kikwazo kikubwa kwa lengo la kukomesha vitendo vya mabavu na kuacha silaha. Mauaji yanayotokea nchini Iraq mengi ni mashambulizi yanayofaywa dhidi ya majeshi ya nchi za nje yanayoongozwa na Marekani, kwa hiyo ili mradi tu majeshi ya nchi za nje yakiendelea kuwepo nchini Iraq lengo la kukomesha vitendo vya mabavu halitafikiwa.

Tatu, "Kuacha silaha" kunahusiana moja kwa moja na maslahi ya kiuchumi na ya kisiasa ya kila upande, kama makundi mbalimbali ya Iraq yakishindwa kuafikiana katika kurekebisha katiba, kujenga upya jeshi lake na ugawaji wa maliasili, lengo la "kuacha silaha" ni maneno matupu. Zaidi ya hayo waraka wa "ramani ya amani ya Iraq" haukutoa mapendekezo yoyote kuhusu masuala hayo.

Wachambuzi wanaona kuwa suala la Iraq ni la utatanishi mkubwa, ambalo linahusiana na masuala ya kidini, kihistoria na ya kisasa, ni vigumu sana kupata maendeleo ya hatua kubwa kwa kufanya mazungumzo mara moja au mbili. Taathira ya "ramani ya amani ya Iraq" ni ndogo sana, kwa sababu hali ilivyo nchini Iraq ni ya utatanishi mkubwa kuliko "ramani" hiyo iliyotungwa kwa msaada wa uzoefu wa mchakato wa amani nchini Ireland ya Kaskazini na Afrika Kusini, na hasa "ramani" hiyo haikutoa mapendekezo yoyote kuhusu maafikiano ya kisiasa na maafikiano ya kitaifa. Hata hivyo, malengo yaliyotolewa kwenye "ramani" hiyo ya kukomesha vitendo vya mabavu na kuacha silaha yameweka mwelekeo wa utatuzi wa suala la Iraq. Zaidi ya hayo wajumbe wa madhehebu ya Shia na Suni wameahidi kuwa wataendelea na mazungumzo huko Finland, na hii hakika ni ishara nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-05