Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-06 18:44:58    
Tishio la ugaidi lakaribia nchini Ujerumani

cri

Mkurugenzi mkuu wa Idara ya uendeshaji wa mashitaka ya Ujerumani Bibi Monika Harms tarehe 5 alitangaza kuwa, idara ya usalama ya Ujerumani tarehe 4 ilivunja njama ya magaidi ya kujaribu kushambulia vikali kwa mabomu kituo cha Marekani nchini Ujerumani. Alisema kama mashambulizi hayo yangefanyika, basi yangekuwa ni mashambulizi makubwa kabisa ya kigaidi katika historia ya Ujerumani.

Habari zinasema kikosi cha kupambana na ugaidi cha Ujerumani tarehe 4 usiku kilifanya msako kwenye sehemu ya mpaka kati ya Jimbo la Hessen na Jimbo la North rhine-westphalia, na kuwakamata watu watatu ndani ya jumba moja la mapumziko wakati wa likizo, na kukamata mapipa 12 ya maji ya Hydrogen peroxide yenye uzito wa kilo 730 yanayoweza kutumika kutengeneza mabomu. Magaidi walipanga kushambulia kwa mabomu Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Frankfurt na kituo cha jeshi la anga la Marekani kilichoko Ramstein nchini Ujerumani.

Bibi Harms alisema watuhumiwa watatu waliokamatwa ni wa tawi la jumuiya ya kigaidi ya kimataifa ya "Shirikisho la mapigano ya jihad la kiislamu" nchini Ujerumani, tawi hilo lina uhusiano wa karibu na kundi la Al Qaeda. Mtuhumiwa mmoja kati yao alitoka Uturuki, wengine wawili wana pasipoti za Ujerumani, na wote waliwahi kupewa mafunzo kwenye kambi ya mazoezi ya kigaidi iliyoko nchini Pakistan. Habari zinasema kuwa, wakati wa kutimia miaka 6 tangu tukio la ugaidi la "tarehe 11 Septemba" nchini Marekani, magaidi wanafanya mpango wa kuanzisha mashambulizi makubwa ya ugaidi kwa mfululizo dhidi ya mashirika ya Marekani nchini Ujerumani na wamarekani, shabaha ya mashambulizi hayo pia ni viwanja vya ndege, mikahawa na klabu za disco nchini Ujerumani. Kutokana na hali hiyo, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Bwana Wolfgang Schaeuble alisema, tishio la ugaidi limekaribia nchi ya Ujerumani.

Katika miaka ya hivi karibuni, Ulaya imekuwa inakabiliwa na tishio la ugaidi linalozidi kuwa mbaya siku hadi siku. Kwa mfano mlipuko wa "tarehe 11 Machi" uliotokea huko Madrid, Hispania, mlipuko wa kigaidi wa "tarehe 7 Mwezi wa Julai" uliotokea kwenye subway huko London, Uingereza na mlipuko uliotokea mwezi Juni mwaka huu kwenye uwanja wa ndege wa Glasgow, Scotland na kadhalika. Aidha polisi wa Uingereza pia walivunja njama mbili za kuanzisha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya sehemu ya katikati ya mji wa London. Wataalamu wamedhihirisha kuwa, kutokana na hatua kali za Marekani za mapambano dhidi ya ugaidi baada ya tukio la "Tarehe 11 Septemba", magaidi hawajaweza kuanzisha mashambulizi tena nchini Marekani, hivyo nchi za Ulaya zilizo washirika wa Marekani zimekuwa shabaha kubwa katika mashambulizi ya kigaidi siku hadi siku. Kwa Ujerumani ingawa jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan siku zote linasumbuliwa na mashambulizi ya kigaidi, lakini tukio kubwa la mashambulizi ya kigaidi halijawahi kutokea hapo kabla nchini Ujerumani. Hata hivyo mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea mara kwa mara barani Ulaya yalitoa onyo kwa serikali ya Ujerumani. Habari zinasema katika miezi kadhaa iliyopita, idara za mapambano dhidi ya ugaidi na idara za usalama za Ujerumani zimefanya kwa makini usimamizi na ufuatiliaji juu ya watuhumiwa wanaopanga mashambulizi ya mabomu, hata watu wanaohusika wa Ujerumani walibadilisha kisiri maji ya kemikali yatakayotumiwa na watuhumiwa kutengeneza mabomu. Ndiyo maana kuvunja njama hii siyo tukio la bahati, na Chansela wa Ujerumani Bibi Angela Markel alisifu kazi nzuri iliyofanywa na idara husika chini ya ushirikiano barabara.

Wachambuzi wanaona kuwa, ingawa majaribio ya mashambulizi hayo hayalengi hasa wajerumani, lakini hili ni tishio halisi la mashambulizi ya kigaidi kuikabili Ujerumani, na limeonesha zaidi kuwa jumuiya ya ugaidi ya kimataifa inaota mizizi katika nchi mbalimbali, na serikali ya Ujerumani inapaswa kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na tishio hilo.