Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-10 19:45:49    
Matembezi kwenye mji wa Kuche, mkoani Xinjiang

cri

Wasikilizaji wapendwa, kila mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uigur ulioko kaskazini magharibi mwa China unapotajwa, watu hukumbuka watu wachangamfu wa makabila madogo madogo pamoja na muziki wenye umaalumu wa kikabila. Lakini leo tutawafahamisha kuhusu sehemu ya Kuche, ambayo ni mabaki ya mji maarufu wa kale mkoani humo.

Kuche ni neno la Kiuigur, maana yake ni historia ya miaka mingi. Katika zama za kale nchini China, watu walikuwa wanaiita sehemu hiyo Guizi. Kuche iko kwenye sehemu ya kati ya mteremko wa kusini wa mlima wa Tian na pembezoni mwa kaskazini mwa bonde la Talimu, sehemu ambayo ni chanzo cha "utamaduni wa Guizi". Guizi ilijulikana sana kama "mji mkuu wa muziki wa sehemu ya magharibi", "maskani ya nyimbo na ngoma" na "sehemu ya asili ya matunda meupe ya apricot", na pia ni "nchi ya wanawake" katika kitabu cha riwaya kinachojulikana kama "Kwenda magharibi kuhiji", ambacho ni moja kati ya vitabu vinne maarufu nchini China. Mtalii aliyetoka sehemu ya bara ya China Bw. Ma Xingtian, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Kuche, alisema,

"Xinjiang ina mandhari nzuri ajabu. Mandhari ya Kuche ni tofauti na ya sehemu nyingine. Watu wanachoona wakiwa Kuche, kinawafurahisha na hata kuwafanya wasiamini kama wanayoona ni ya kweli. Mandhari nzuri ya hapa ni ya ajabu sana na ya kufurahisha mno."

Sehemu ya Kuche iko kwenye njia ya kati ya hariri, na ni sehemu yenye utamaduni mkubwa wa sehemu za kati na magharibi. Huko kuna dini ya kibudha iliyoendelea kwa zaidi ya miaka 2,000, michoro mingi iliyochorwa kwenye mapango ya mawe ya milima, ambayo inachukua nafasi ya kwanza kwenye sehemu ya magharibi ya Dunhuang, pamoja na muziki na ngoma zinazopendwa sana za Guizi.

Kuche ni moja ya miji na wilaya nne maarufu za kiutalii, Kuche ina sehemu zaidi ya 80 za mabaki ya kiutamaduni yakiwemo ya mapango ya mawe, majengo makubwa ya zamani yenye ngome, pamoja na majengo marefu ya kupasha habari kuhusu hali ya hatari kwa moto na moshi, mapango ya mawe zaidi ya 500 na michoro iliyochorwa kwenye kuta za mapango yenye mita za mraba zaidi ya elfu 20 kwa jumla. Kati ya hayo pango lenye sanamu za budhaa elfu moja la Kumutula na pango lenye sanamu za budhaa elfu moja la Kesil ni mapango maarufu sana nchini China, ambayo yalijengwa katika kipindi cha toka enzi ya Jin ya magharibi hadi enzi ya Jin ya mashariki, na pango la Kesil limetoa ombi la kuorodheshwa katika orodha ya mabaki ya kale ya utamaduni wa wabinadamu duniani ya Umoja wa Mataifa.

Bw. Teng Shaozhen ni ofisa wa shirika la utalii nchini Australia, alifunga safari mahususi kutembelea sehemu ya Kuche, anaona kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa Xinjiang ni umaalumu mkubwa wa utamaduni wa Xinjiang.

"Ni kweli hapa kuna sehemu nyingi zinazopendeza. Kitu muhimu zaidi ni kuwa, Xinjing kuna vitu vingi vya kiutamaduni, mbali na mandhari nzuri ya kimaumbile. Kuwafahamisha walimwengu kuhusu historia ya China ni fahari ya taifa la China. Kwa hiyo nitapiga picha nyingi zaidi, na kuwafahamisha wateja wangu baada ya kurudi, wateja wa nchi za nje wanapenda sana utamaduni wa China. Ninaona utalii wa Xinjiang una mustakabali mzuri."

Tamasha la 4 la utalii wa kimataifa na utalii wa utamaduni wa Guizi lilifanyika mwezi Julai mwaka huu katika mji wa Kuche, Xinjiang. Wafanyabiashara zaidi ya elfu moja kutoka nchi 22 na sehemu mbalimbali za China pamoja na wakazi wa makabila mbalimbali wa huko waliburudishwa kwa umaalumu wa utamaduni wa Guizi. Mara tu baada ya kushuka kutoka kwenye ndege, walivutiwa sana na utamaduni pamoja na mandhari nzuri za huko walisema, Xinjiang ni sehemu yenye vivutio vingi vya utalii nchini China, ina uwezo mkubwa wa kukuza mambo ya utalii katika siku za baadaye, hakika huko itakuwa sehemu itakayofuatiliwa na watu duniani katika mambo ya utalii.

Watalii waliotoka sehemu za nje wakifika Kuche, mkoani Xinjiang, wanavutiwa na matunda za aina mbalimbali pamoja na vyakula mbalimbali vya kijadi vya huko. Visu vidogo, makofia yaliyotengenezwa kwa vitambaa vyenye picha za maua, ngozi za kondoo wachanga, mazulia na apricot zinajulikana nchini China na katika nchi za nje, hususan matunda meupe ya apricot yaliyokomaa yanaonekana yaking'ara kama kioo, ukiitafuna mdomoni mwako kutajaa maji matamu kama asali. Huko kuna msemo unaosema, "Zabibu za Tulufan, matikiti ya Hami na kondoo wa Kuche vinatia fora". Kondoo wa Kuche ni kondoo wanaoishi kwenye jangwa la huko, ambao wanakunywa maji yenye magadi. Kila siku asubuhi, wenyeji wa kabila la Uigur wanaweka viungo kwenye nje na ndani ya mwili wa kondoo waliochinjwa, kisha wanawatia ndani ya shimo lenye moto, ili nyama ya kondoo iokwe, na harufu tamu ya nyama inajaa kwenye mtaa mzima, ambapo watu wanaosikia harufu nzuri huimezea mate.

Nyimbo na ngoma ya Kuche ni maarufu sana kutoka zamani. Hivyo mji wa Kuche pia unajulikana kama "maskani ya nyimbo na ngoma". Nyimbo na ngoma ya Guizi ni maarufu sana katika sehemu ya magharibi, ambazo ziliwahi kuenezwa na kuwa na athari nchini Japan, Korea, Uajemi, Vietnam, India pamoja na nchi za kiarabu na Afrika ya kaskazini. Zaidi ya hayo zinaathiri sana ustawi na maendeleo ya muziki, ngoma, michezo na sarakasi za China.

Naibu mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uigur Bw. Hu Wei anaona kuwa, mambo ya utalii ya Xinjiang yatakuwa na mustakabali mzuri.

"Utalii ni kiungo ambacho kinaimarisha urafiki kati ya watu wa makabila mbalimbali wa China na watu wa nchi mbalimbali duniani, kinaongeza nafasi ya kuaminiana na kufanya ushirikiano. Tunawaalika marafiki wengi zaidi wa nchi mbalimbali kwa moyo wa dhati waje kuitembelea Xinjiang, kufahamu historia, utamaduni, mandhari nzuri pamoja na ustawi na maendeleo ya Xinjiang.