Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-11 16:06:15    
China yaimarisha usimamizi wa sifa na usalama wa vyakula

cri

Sifa na usalama wa vyakula ni suala linalofuatiliwa na dunia nzima, pia ni suala linalotiliwa maanani na China. Serikali na makampuni ya China yanachukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha sifa na usalama wa vyakula.

Idara ya usimamizi na ukaguzi wa sifa ya bidhaa na karantini ya China ni moja ya idara zinazosimamia usalama wa vyakula nchini China. Kwenye mkutano mmoja na waandishi wa habari kuhusu sifa ya bidhaa na usalama wa chakula uliofanyika mwezi Julai, mkurugenzi wa idara hiyo Bw. Li Changjiang alisema,

"Naona vyakula vingi zaidi vya China vinafikia viwango vinavyotakiwa, na sifa zake zimekuwa nzuri zaidi. Hivi karibuni tulifanya ukaguzi kuhusu baadhi ya vyakula, asilimia 85.1 ya vyakula vimefikia viwango, asilimia 91.5 ya vyakula ambavyo ni mahitaji ya kila siku ukiwemo mchele, unga wa ngano na mafuta ya kupikia vimefikia viwango, na asilimia 97.5 ya baadhi ya maji ya matunda yamefikia viwango. Kwa ujumla sifa zake ni nzuri."

Bw. Li Changjiang alisema, katika miaka mingi iliyopita, China ilitunga sheria na kanuni nyingi kuhusu sifa za vyakula ambazo zinaendana na hali halisi nchini China; pia ilianzisha utaratibu wa usimamizi wa sifa na usalama wa chakula. Habari zinasema China inatekeleza utaratibu wa utoaji wa idhini ya kuingia kwenye soko la vyakula, na kusimamia idhini zilizopewa, kila mwaka China inakagua baadhi ya vyakula na kutangaza matokeo ya ukaguzi kwa wananchi. Aidha, China inatekeleza utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa bidhaa viwandani, ili kuhakikisha sifa na usalama wa bidhaa zitakazouzwa masokoni.

Makampuni mengi ya vyakula ya China yanazingatia sana sifa na usalama wa bidhaa zao. Kampuni ya Huiyuan ni kampuni kubwa inayotengeneza vinywaji vya matunda nchini China. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, bidhaa zilizozalishwa na kampuni hiyo ilichukua asilimia 46 ya mgao kwenye soko la maji ya matunda. Maji ya matunda na vinywaji vya watoto vinavyotengenezwa kwa maji ya matunda vya kampuni hiyo vinauzwa katika zaidi ya nchi na sehemu 20 zikiwemo Marekani, Australia, New Zealand, Asia ya Kusini Mashariki na Afrika. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Zhu Xinli alisema,

"Kampuni ambayo haitilii maanani usalama wa vyakula na sifa za bidhaaa haitaendelezwa kwa muda mrefu, hivyo sifa za bidhaa ni jambo kubwa kabisa kwa kampuni moja."

Alieleza kuwa, katika karakana ya usindikaji ya kampuni hiyo, chembechembe za mavumbi kwenye futi moja ya ujazo zilikuwa chini ya mia moja. Wafanyakazi wanaotaka kuingia kwenye karakana hiyo ni lazima waondoe vumbi na vijidudu kama madaktari wanaotaka kuingia chumba cha operesheni.

Kampuni ya Yili ambayo ni kampuni maarufu ya kutengeneza bidhaa za maziwa nchini China pia ina utaratibu sawasawa na Kampuni ya Huiyuan kuhusu sifa za bidhaa. Hivi sasa asilimia 99 ya maziwa yanayozalishwa katika kampuni hiyo yamefikia viwango vinavyotakiwa. Katika malisho ya ng'ombe wa kampuni hiyo, vifaa vya kurekodi afya ya ng'ombe vimewekwa kwenye sikio la kila ng'ombe. Meneja wa malisho ya kampuni ya Yili Bw. Yu Yongqiang alisema,

"Vifaa hivyo vinaweza kugundua ng'ombe wenye matatizo, na kuhakikisha kuwa maziwa yasiyofikia viwango hayatatumiwa kwenye uzalishaji."

Serikali na makampuni ya China yanayowajibika yanafanya sifa za vyakula vya China ziinuliwe siku hadi siku. Mkuu wa idara ya usimamizi na ukaguzi wa sifa ya bidhaa na karantini ya China Bw. Li Changjiang alisema, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, asilimia 99 ya vyakula vya China vilivyouzwa nchini Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan vilifikia viwango.

Bw. Li pia alisema, China bado ni nchi inayoendelea, kiwango cha usalama wa vyakula na maendeleo ya viwanda vya vyakula bado yako nyuma kuliko nchi zilizoendelea. Kuinua sifa na usalama wa vyakula bado ni kazi ngumu. Hivi sasa kuna masuala kadhaa katika usalama wa vyakula. Hali ya uzalishaji ya makampuni na karakana ndogo bado haijafikia viwango. Bw. Li Changjiang alisema idara ya usimamizi na ukaguzi wa sifa ya bidhaa na karantini ya China itaendelea kuchukua hatua kubadilisha hali hiyo. Alisema,

"Hali ya uzalishaji kwa baadhi ya makampuni na karakana ndogo za vyakula iko nyuma, na sifa za bidhaa za kampuni na karakana hizo hazina uhakikisho, na baadhi ya bidhaa hazifikii vigezo vinavyotakiwa. Tutaendelea kuchukua hatua kufunga kampuni ndogo ambazo zinazalisha bidhaa zisizofikia viwango kwa muda mrefu na hata zinazalisha bidhaa bandia."

Kabla ya muda mfupi uliopita serikali ya China ilitoa waraka wa hali ya sifa na usalama wa vyakula nchini China. Waraka huo unaonesha kuwa, baada ya kuchukua hatua kadhaa, mwaka jana asilimia 70 ya vyakula vilivyotengenezwa na karakana ndogo vilifikia viwango vilivyotakiwa; hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, China ilikuwa imefunga karakana zaidi ya elfu 5, kusimamisha uzalishaji wa karakana zaidi ya 8800, na karakana zaidi ya elfu 5 zimefikia vigezo vya kuingia masokoni baada ya marekebisho.

Mkuu wa idara ya sayansi ya chakula wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China Bw. Luo Yunbo alipohojiwa na waandishi wa habari alisema,

"China ni nchi inayoagiza na kuuza bidhaa nje kwa wingi, pia ni nchi inayozalisha vyakula kwa wingi, kununua vyakula kwa wingi na kuuza vyakula nje kwa wingi. Usalama wa vyakula vya China unafuatiliwa na watu wengi. Katika hali hiyo, kutoa waraka kwa wakati na kuelekeza hali ya usalama wa vyakula nchini China na hatua zinazochukuliwa kwa usimamizi wa usalama wa vyakula ni hatua ya kuwajibika."

Waraka huo unasema, kutimiza usalama wa chakula ni lengo la pamoja la binadamu, pia ni wajibu wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa, China ikiwa ni nchi inayoagiza na kuuza bidhaa nje kwa wingi, inapenda kushirikiana na kuwasiliana na nchi mbalimbali duniani, na kuendelea kufanya juhudi katika usimamizi wa usalama wa vyakula na kusukuma mbele maendeleo ya biashara ya vyakula duniani.