|
Tarehe 11 Septemba mwaka 2001 kundi la Al-Qaeda liliishambulia Marekani kwa shambulizi kubwa la kigaidi ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Marekani, na kusababisha vifo vya watu karibu 3,000, baadaye Marekani ilianzisha vita dhidi ya Afghanistan na Iraq na huku nchini ikiwa imeimarisha vitendo vya kusikiliza kisirisiri mawasiliano ya watu, na kuchukua hatua kali za usalama. Lakini je, baada ya vita dhidi ya ugaidi kote duniani kwa miaka kadhaa, Marekani imekuwa salama zaidi? Wakati tukio la "Septemba 11" linapotimiza mwaka wa sita, suala la usalama limerudi tena kwenye mazungumzo ya wananchi wa Marekani.
Serikali ya Rais George Bush inadai kuwa miaka sita iliyopita ni miaka yenye mafanikio kwenye mapambano dhidi ya ugaidi. Mantiki ya kusema hivyo ni kwamba, katika muda wa miaka sita iliyopita, mashambulizi kama tukio la "Septemba 11" hayakutokea nchini Marekani. Waziri wa usalama wa ndani wa Marekani Bw. Michael Chertoff hivi karibuni alipokuwa anaongea kwenye mkutano wa bunge alisema, "Kwa vyovyote vile hayo ni mafanikio makubwa." Lakini watu wengi wana maoni tofauti na mantiki hiyo.
Ripoti kuhusu hali ya taifa ya Marekani iliyotolewa mwezi Julai mwaka huu inaonesha kuwa, hivi sasa tishio la ugaidi linaloikabili Marekani linalingana na lile lililokuwepo mwaka 2001. Kundi la Al-Qaida lina matawi nchini Iraq na matawi hayo yanajitahidi kuwakusanya na kuwaandikisha watu wake, na huku kutokana na athari ya fikra za Al-Qaida magaidi wamekuwa wakiongezeka siku baada ya siku katika sehemu mbalimbali duniani. Ripoti inasema kundi la Al-Qaida limekuwa na uwezo karibu wote wa kufanya mashambulizi nchini Marekani, na kiongozi wa kundi hilo Osama bin-Laden anaendelea kuwa huru kabisa, na hata siku za karibuni ametoa kanda yake ya video kuishambulia Marekani kisaikolojia, hii ni dhihaka kwa vita vya Marekani dhidi ya ugaidi.
Katika siku chache zilizopita, jarida la "Sera za kidiplomasia" la Marekani lilifanya mazungumzo na wataalamu na wanadiplomasia 100 wa Marekani, kati yao asilimia 92 wanaona kuwa dunia imekuwa hatari zaidi kwa Marekani, na asilimia 84 wanaona Marekani haijafanikiwa kikweli katika vita dhidi ya ugaidi, na asilimia 80 wanaona kuwa Marekani itakumbwa tena mashambulizi kama tukio la "Septemba 11" katika muda wa miaka 10 ijayo.
Mwenyekiti na naibu wake wa kamati ya zamani ya kufanya uchunguzi wa tukio la "Septemba 11" waliandika makala wakisema, kutokana na makosa ya sera mfululizo za serikali ya George Bush, hali ya usalama wa Marekani haijaboreshwa. Baadhi ya watu wanasema, badala ya kuweza kuboresha hali ya usalama katika muda wa miaka sita iliyopita, athari ya sera mbaya za mapambano dhidi ya ugaidi imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku. Kashfa ya kuwadhalilisha wafungwa kinyume na makubaliano ya Geneva, na Shirika la Upelelezi la Marekani kuwa na magereza nje ya nchi imeshusha hadhi ya Marekani, sura ya kimataifa ya Marekani imeharibika, hasira za kupinga Marekani zimekuwa zikiongezeka duniani. Na athari mbaya zaidi ya sera za serikali ya George Bush kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi ni kuanzisha vita dhidi ya Iraq kwa kisingizio cha "mapambano dhidi ya ugaidi". Vita dhidi ya Iraq licha ya kutawanya nguvu za Marekani za kupambana na ugaidi, badala yake imesababisha kuongezeka kwa magaidi, na kuifanya Iraq iwe ni pepo na chimbuko la magaidi.
Aidha, wataalamu wanasema ingawa Marekani imekuwa na tahadhari sana na hayakutokea matukio ya ugaidi katika miaka kadhaa iliyopita, lakini tishio la ugaidi limekuwa kama upanga uliokaa kwenye shingo ya Marekani, na wakati wowote upanga huo ungeweza kudondoka. Maoni yaliyokusanywa kutoka kwa watu wazima 2,372 yanaonesha kuwa, 55% ya watu walioulizwa wanaona Marekani haijawa salama zaidi baada ya vita vya Iraq. Na maoni yanaonesha kuwa asilimia 30 ya watu wanahofia kusafiri, wanaona kuwa ingawa serikali imechukua hatua za usalama ili kuwashawini wasiwe na wasiwasi na safari zao lakini hakuna mtu yeyote aliyethibitisha kuwa sera hizo ni za uhakika.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-11
|