Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-14 19:49:56    
Siku ya China kwenye Chuo kikuu cha Egerton nchini Kenya

cri

Wasikilizaji wapendwa, ulizosikia sasa hivi ni nyimbo za kichina ambazo ziliimbwa na wakenya. Katika siku za karibuni Chuo Kikuu cha Egerton pamoja na ubalozi wa China nchini Kenya walishirikiana kuandaa shughuli inayoitwa "Siku ya China" katika chuo kikuu hicho.

"Leo kuna maonesho mazuri kuhusu China, Leo unaweza kuona wewe mwenyewe China ikoje, na ukiwa na nafasi, ungeenda kwenye baadhi ya sehemu ambazo zinaoneshwa katika picha hizo. "

Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Egerton Bw. James Tuitoek alisema hivyo katika ufunguzi ya shughuli hiyo ya "siku ya China", lakini nadhani ni afadhali twende kujionea wenyewe.

Tukifuata bango kubwa ukutani lenye maandishi ya kichina na alama zenye mitindo ya kichina juu yake, tunaingia kwenye chumba kimoja kubwa, ambapo picha nyingi zinaoneshwa huko. Picha hizo zinaonesha jinsi wachina wanavyoishi, wanafanya nini wakati wa burudani, na vipi wanavyojiandaa kwa michezo ya Olimpiki ya 2008 ya Beijing.

Wakati huo huo, muziki ulikuwa unatoka kwenye chumba kingine.

Kumbe kwenye ukumbi wa Kilimo Hall, ambao hauko mbali na chumba cha maonesho ya picha, mashindano ya kuimba nyimbo za kichina yalikuwa yanaendelea, muziki na sauti nyororo zilikuwa zinatoka huko.

Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo, ni wanafunzi wanaosoma lugha ya kichina kwenye chuo kikuu hiki, lakini bila kutarajiwa na watu wote, hatimaye ushindi ulinyakuliwa na mtoto mmoja wenye umri wa miaka 8. Lakini iliwashangaza sana watu kwa kuwa mtoto huyu alikuwa hajifunzi kichina, ila tu alikuwa anajifunza nyimbo za kichina kwa kupitia kutazama vipindi vya televisheni.

Balozi wa China nchini Kenya Bw. Zhang Ming alimtunukia mtoto huyo ambaye anaitwa Florence. Baada ya hapo, alitoa mafunzo maalum kwa wanafunzi, kuhusu "Kusukuma mbele ushirikiano kati ya Afrika na China, ili kutimiza maendeleo ya pamoja". Bw. Zhang Ming, mwenye umri wa miaka zaidi ya 50 ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa, kwenye mafunzo yake, aliwaelezea kwa pande zote historia ya uhusiano kati ya Afrika na China, na maendeleo mapya ya uhusiano huo.

Alisisitiza tena kuwa urafiki kati ya Afrika na China una historia ndefu, mawasiliano yaliyokuwepo zamani kati ya China na nchi za Afrika, ni sehemu muhimu ya maingiliano ya ustaarabu ya dunia nzima.

Katika miaka 50 iliyopita, China na nchi za Afrika zilikuwa zinasaidiana, urafiki ulijengwa katika wakati wa shida, ambapo pande zote zilikuwa ni nchi changa. Ilipofika miaka ya karibuni, urafiki huo umepata maendeleo mapya. Alichukua Kenya kama mfano akisema kwamba tangu mwaka 2002, ushirikiano kati ya Kenya na China umezaa matunda mapya, viongozi wa nchi mbili wanatembeleana mara kwa mara na ushirikiano upo katika nyanja mbalimbali.

Bw. Zhang alisema, amani na maendeleo ni mwelekeo wa dunia ya leo, Afrika na China zote ni nguvu muhimu kwa amani na maendeleo ya dunia nzima, kuendeleza kwa kina urafiki wa jadi na kuongeza ushirikiano kati ya Afrika na China kunaambatana na nia ya watu wa pande mbili na pia ni matakwa ya zama hizi.

Kuhusu suala la nishati kama mafuta, Bw. Zhang alieleza kwa utaratibu kwamba, China ni nchi ambayo inazalisha mafuta kwa wingi kiasi ambacho kinachukua asilimia 90 ya mahitaji yake, na China pia inaagiza mafuta kutoka sehemu nyingine duniani ikiwemo Afrika, lakini mafuta inayoagiza si mengi. Mwaka 2006, katika jumla ya mafuta yaliyoagizwa kutoka Afrika, China iliagiza asilimia 8.7 tu kutoka Afrika, , ambapo asilimia 36 na asilimia 33 zilienda Ulaya na Marekani, na tukiangalia kwa ujumla dunia nzima, kiasi cha mafuta yanayoagizwa na China kinachukua asilimia 6 tu ya mafuta ya soko la dunia. Kwa hiyo si sahihi na wala hakuna msingi wowote kusema kwamba kuingiza mafuta kwa China kunasababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani, na wala si sahihi kukosoa ushirikiano wa nishati kati ya China na Afrika.

Bw. Zhang alisema kuna sababu mbalimbali kwa urafiki na ushirikiano kati ya Afrika na China kufika kiwango cha juu cha leo, kwanza waafrika na wachina wote wanapenda amani na kutathimini urafiki kati yao; pili, China na Afrika zinaendeleza uhusiano kati yao kwa msingi wa kuheshimiana, bila kuingilia mambo ya ndani ya upande mwingine, kunufaishana na kusaidiana katika mambo ya dunia; na tatu ni kwamba wachina na waafrika wote wanakabiliwa na changamoto ya kuendeleza uchumi na kuboresha kiwango cha maisha ya wananchi, kwa hiyo kusaidiana na kujifunza kutoka kwa upande mwingine ni muhimu sana. Bw. Zhang alisema mwishoni kuwa?

"Wachina wanajivunia kuwa na urafiki na waafrika, China ni rafiki na ndugu wa Afrika toka zamani na leo, na katika siku za usoni hali hiyo haitabadilika."

Wasikilizaji wapendwa, mkitembelea Beijing, mji mkuu wa China, kwenye Subway mtaona picha nyingi kubwa kuhusu Kenya, watu wa Kenya, mazingira ya Kenya, na wanyama wa Kenya. Kutokana na kuangalia picha hizo, wachina wanaielewa zaidi Kenya, na watu kutoka nchi nyingine wanaelewa zaidi Kenya; kwa wakati mmoja, nchini Kenya, shughuli kama "Siku ya China" inatoa fursa nzuri kwa wakenya kuelewa China, hiyo ni nchi gani, jinsi wachina wanavyoishi, na wamepata maendeleo gani katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya 2008. Kuelewana ni msingi wa urafiki, kuelewana kwa lugha, kuelewana kiutamaduni, ndipo urafiki unajengwa na kuzidi kuimarika. (Ishia hapa)