Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-17 15:54:11    
Matembezi kwenye mlima waYuntai mkoani Henan

cri

Nchini kuna sehemu nyingi zenye mandhari nzuri, mlima wa Yuntai ulioko kwenye mkoa wa Henan, katikati ya China ni sehemu moja yenye mandhari nzuri ya milima na mito. Mlima wa Yuntai uko katika wilaya ya Xiuwu, ya mji wa Jiaozuo, mkoani Henan, ambao ni moja katika kundi la kwanza la bustani za jiolojia zilizothibitishwa na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa. Sehemu hiyo yenye mandhari nzuri ina eneo karibu kilomita za mraba 200, ina milima mingi yenye chemchemi.

"Kwenye mlima wa Yuntai, maji yako ndani ya milima na inangoja kugunduliwa na watalii. Watu wanasifu maji mengi ya milimani kwa kusema, mtu akipiga hatua tatu hakosi kuona chemchechemi, akipiga hatua tano anaona maporomoko ya maji, na akipiga hatua kumi anaweza kuona bwawa la maji. Kwenye mlima wa Yuntai, kuna maji yanayoanguka kutoka juu kwa zaidi ya mita 300, mtu akinyanyua kichwa na kuangalia juu, anaona maji kama yanaanguka kutoka mbinguni, kwa hiyo jina la maporomoko hayo ya maji linaitwa "maporomoko ya maji ya mbinguni". Tunawashauri watalii wanaofika kwenye mlima wa Yuntai, wakae siku chache kwenye nyumba za wageni zinazoendeshwa na familia za wenyeji wa huko. Nyumba za wageni hizo ni safi na za bei rahisi, lakini watalii wanaweza kujiburudisha kwa maisha ya raha ya milimani kwenye sehemu safi. Bw. Wang jianfeng alifika mara kadhaa kwenye mlima wa Yuntai, na kila mara alikuwa anakaa kwenye nyumba za wageni za familia za wenyeji.

"Nimefika kwenye mlima wa Yuntai mara mbili, tatu, naona nyumba hizo za wageni ni nzuri, mazingira yake ni mazuri, lakini bei ni nafuu. Niliwaambia marafiki zangu wengi, na walisema, watakuja kutembelea hapa."

Kwa watalii wanaofika mlima wa Yuntai, kitu cha kwanza cha kuangalia ni milima ya huko, milima mizuri inaungana pamoja kwenye eneo la kilomita mia kadha. Mlima mrefu zaidi kwenye sehemu hiyo ni mlima wa Zhuyu wenye urefu wa zaidi ya mita 1,300 kutoka usawa wa bahari. Kama mtu akipanda mlima kwa kufuata ngazi zilizotengenezwa, anaweza kuona kama anatembea kwenye mawingu. Baada ya kufika kileleni na kutazama mbali, mtu anaweza kuona mandhari nzuri ya mawingu, ambayo ni kama bahari kubwa, vilele vya milima vinaonekana kwenye sehemu ndogo ya juu tu, kama mawimbi ya baharini. Ukitupia macho kwenye mto Manjano, utaona mto huo unaonekana kama mkanda mmoja wa hariri ulioko ardhini.

Sehemu yenye mandhari nzuri kwenye mlima wa Yuntai ni kubwa sana, mtu akitaka kumaliza kutembelea sehemu moja itamchukua muda wa kutoka nusu saa hadi saa tatu hivi, akitaka kutazama sehemu zote itamchukua muda mrefu zaidi. Ili kupunguza muda unaotumika kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine zenye mandhari nzuri, idara ya usimamizi kwenye sehemu ya mlima wa Yuntai imeweka cable-car kwa watalii bila malipo, licha ya hayo, sehemu zote za utoaji huduma zimeweka vituo vya cable-car na ramani ya sehemu za utalii, ili kuwarahisishia watalii. Ili kupunguza matumizi ya fedha kwa watalii, kiingilio cha sehemu ya mlima wa Yuntai kinatumika kwa siku mbili. Naibu mkurugenzi wa idara ya usimamizi Bw. Li Jie alituambia kuwa mtalii akikata tikiti ya kiingilio, anaweza kutembelea sehemu hiyo kwa siku mbili kwa kutumia tikiti hiyo.

"Kiingilio cha sehemu ya mlima wa Yuntai kinatumika siku mbili, kwa kawaida tikiti za kiingilio kwa sehemu nyingine za utalii zinatumika siku ile ile moja tu. Idadi ya watalii wanaotembelea sehemu yetu ni karibu milioni 1 na laki 5 kwa mwaka, na kiasi cha 70% ya watalii wanaingia sehemu ya mandhari katika siku ya pili."

Utaratibu huo wa kufikiria mahitaji ya watalii unawafurahisha watalii wanaotembelea huko, dada Song Lin kutoka mkoa wa Shandong anaona, kiingilio kinachotumika siku mbili kinawanufaisha watalii. Dada Song alisema,

"Utaratibu huo ni mzuri sana. Kwani sehemu ya mandhari ni kubwa, watalii wengine wanashindwa kuangalia sehemu zote kwa siku moja. Kama kiingilio kinatumika kwa siku mbili, tunaweza kuitembelea katika siku ya pili. Tunaona mpango huo una lengo la kufikiria mahitaji ya watu."

Mlima wa Yuntai una sehemu nyingi zenye mandhari nzuri, kila siku unapokea wageni elfu kadhaa kutoka nchini na nchi za nje, lakini watalii hawana wasiwasi wa kupotea njia. Kwenye sehemu ya mlima wa Yuntai vimewekwa vibao vingi vya kuelekeza njia, kutoa onyo na maelezo kuhusu mandhari, tena kwenye vibao hivyo yameandikwa kwa maneno ya lugha nne za Kichina, Kiingereza, Kikorea na Kijapan, hivyo licha ya kuwarahisishia watalii waliotoka sehemu nyingine za China, pia vinawasaidia sana watalii wa kigeni. Naibu mkurugenzi wa idara ya usimamizi, Bw. Li Jie alisema,

"Asilimia 70 ya vibao vya kuelekeza njia, vimeandikwa kwa maneno ya lugha za aina nne za Kichina, Kiingereza, Kijapan na Kikorea. Watalii wanapotembela sehemu ya mandhari, hata kama wamepoteana na waongoza watalii, wanaweza kukutana na watu wa vikundi vyao kwa haraka kwa kufuata maelekezo ya vibao hivyo vilivyowekwa njiani."

Mfumo wa kituo cha usimamizi wa teknolojia ya tarakimu kilichojengwa hivi karibuni kwenye sehemu ya mlima wa Yuntai, umefunika sehemu zote za mandhari pamoja na baadhi ya njia muhimu. Idara ya usimamizi inaweza kupanga vizuri magari na wafanyakazi kwa kufuata idadi ya watalii walioko kwenye sehemu mbalimbali. Endapo watalii wakipoteana na vikundi vyao, mfumo wa usimamizi unaweza kuwaona watalii hao kwa haraka.

Aidha kwenye milango ya kuingilia kwenye sehemu mbalimbali za vivutio, kuna ujia uliosetiriwa na aina ya mimea inayotambaa inayoitwa Chinese wistaria, ambapo ni mahali pa kupumzika kwa watalii, tena kwenye upande mwingine wa ujia, kuna chumba cha kuvutia sigara kwa ajili ya wavutaji sigara. Mbali na hayo, kwenye lango la sehemu ya mlima wa Yuntai kuna kituo cha huduma za watalii, watalii wanaweza kuweka kwa muda vitu wasivyovitumia kwenye matembezi. Kuna huduma nyingi nyinginezo zinazotolewa kwa watalii kwenye sehemu ya vivutio ya mlima wa Yuntai, mpango wote huo ni kuwarahisishia watalii na kuwawezesha wawe na furaha katika matembezi. Bw. Huang Weishen anayeishi nchini Malaysia, aliridhika sana na huduma zinazotolewa na idara ya usimamizi ya sehemu ya vivutio ya mlima wa Yuntai, alisema,

"Ninaona sehemu ya mandhari ya mlima wa Yuntai ni nzuri sana, licha ya kuwa na mandhari nzuri, sehemu zote ni safi. Kufanya matembezi hapa ninaona furaha kubwa, tena huduma zao ni nzuri sana."

Idhaa ya kiswahili 2007-09-17