|
Mkutano wa 9 wa wafanyabiashara wachina wa sehemu mbalimbali duniani unaoendelea huko Japan umeonesha dhahiri mtindo wake pekee wa sanaa na utamaduni wa China, ambapo maonesho ya michoro ya kichina, maandiko ya Kichina yanafanyika pia wakati wa mkutano huo. Shughuli mbalimbali za maingiliano ya utamaduni zimeongezwa kwenye Mkutano huo chini ya Bwana Ding Kaien ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa Shirikisho la wafanyabiashara wachina wa sehemu mbalimbali duniani. Bwana Ding alisema:
"wakati wa kufanyika kwa Mkutano huo, pia zinafanyika shughuli mbalimbali za maingiliano ya kiutamaduni, hali hii haikuwahi kutokea kwenye mikutano iliyopita. Kwa mfano, kufanyika kwa maonesho ya michoro ya kichina, kufanyika kwa shughuli za Mwaka wa China, na kadhalika, shughuli hizo zimetoa mchango mkubwa, mawasiliano ya kiutamaduni na maingiliano ya kiraia kwenye mambo mbalimbali yanachangia sana kufanikiwa kwa Mkutano huo".
Kwenye sehemu unapofanyika mkutano huo, Maonesho ya michoro na maandiko ya Kichina ya watu wa vizazi vitatu wa familia moja Wu Ying, Wu Zuguang na Wu Huan yanawavutia watazamaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. Bwana Wu Ying alikuwa mchoraji wa kwanza wa China aliyeingiza ustadi wa uchoraji wa kimagharibi kwenye uchoraji wa michoro ya kichina. Bwana Wu Zuguang alikuwa mwanafasihi na mwanatamthiliya maarufu nchini China, na ustadi wake wa kuandika maandiko ya Kichina pia ni wenye mtindo peke yake. Na Bwana Wu Huan ni mwenyekiti wa Shirikisho la wachoraji wa Hong Kong ambaye ni msanii wa kiwango cha juu kwenye maandiko ya Kichina na michoro ya kichina. Bwana Wu Huan anaona kuwa Mkutano huo una umuhimu mkubwa katika kuwawezesha wachina wanaoishi sehemu mbalimbali duniani washikamane, na kwenye sanaa yake anataka kuonesha pia wazo kuhusu hali ya masikilizano. Alisema:
"wachina wanaoishi sehemu mbalimbali duniani wanapaswa kuungana chini ya bendera kubwa ya masikilizano, tunafanya juhudi za kukuza mambo ya uchumi, na kirohoni pia tuna wazo la masikilizano kuhusu mambo mbalimbali. Tunatarajia kuwa maonesho yanayofanyika sasa yatahimiza utamaduni wa China uenee nchini Japan na kwenye nchi mbalimbali duniani. Ni matumaini yetu kuwa Mkutano kama huo utafanyika mara kwa mara ili kusaidia mawasiliano na urafiki kati ya wananchi wa China na nchi mbalimbali duniani, pia utasaidia kuinua uwezo na sifa ya wafanyabiashara wachina wa sehemu mbalimbali duniani".
Maonesho ya wachoraji 9 ambao ni maarufu kabisa nchini China yameonesha kiwango cha juu kabisa cha michoro ya kichina na maandiko ya Kichina. Mwandaaji wa maonesho hayo Bwana Wang Deshui ambaye ni mchoraji wa China anayeishi nchini Japan alieleza matumaini yake kuwa, kufanyika kwa maonesho hayo kutawawezesha watu wengi zaidi waelewe uzuri wa utamaduni wa jadi wa China. Alisema:
"hii ni mara ya kwanza kwa Maonesho kama haya kufanyika katika historia ya wafanyabiashara wachina wa sehemu mbalimbali duniani, siku za baadaye tutaendelea kufanya maonesho kama haya wakati wa Mkutano wa wafanyabiashara wachina duniani unapofanyika".
Mwenyekiti mtendaji wa maonesho hayo ya michoro ya kichina Bibi Lu Juan alisema, kufanyika kwa mafanikio maonesho hayo ya michoro ya kichina kumeonesha kiini cha utamaduni wa China, tunataka maonesho yetu yasaidie kueneza utamaduni wa jadi wa taifa la China. Alisema kueneza utamaduni wa taifa la China duniani ni jambo zuri, sisi tunafanya shughuli za biashara duniani, lakini tunatakiwa kuvumbua utamaduni wa kampuni zetu katika biashara, badala ya kufanya biashara peke yake. Utamaduni wa China umekuwa na historia ya miaka kati ya elfu 4 hadi elfu 5, kila mwananchi wa China anabeba jukumu la kueneza na kuonesha utamaduni wa China kwa dunia nzima.
|