Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-18 18:45:42    
Nchi za EU zina maoni tofauti kuhusu kuiwekea vikwazo Iran

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Bw. Maxime Verhagen tarehe 17 Septemba alisema, Uholanzi na Ufaransa zitajitahidi kuzishawishi nchi nyingi zikubali kuiwekea vikwazo Iran vinavyolenga kuilazimisha nchi hiyo iache mpango wake wa nyuklia ukiwemo wa kusafisha uranium nzito. Lakini siku hiyo Ujerumani, Italia na Austria ziliikosoa kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa aliyotoa tarehe 16 kuhusu kujiandaa kwa vita dhidi ya Iran. Ni dhahiri kuwa nchi za Umoja wa Ulaya zina maoni tofauti kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Katika kipindi kirefu msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo, ni kupinga mpango wa Iran wa kusafisha uranium nzito lakini kutofunga kabisa mlango wa mazungumzo. Ufaransa ilikuwa inashikilia msimamo huo wakati ilipoongozwa na rais mstaafu Jacques Chirac. Lakini baada ya Rais Nicolas Sarkozy kuingia madarakani, Ufaransa imekuwa ikianza kufuata sera kali katika suala la nyuklia la Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bw. Bernard Kouchner anaona kuwa, suala la kuiwekea vikwazo Iran linapaswa kutekelezwa tu badala ya kujadiliwa kwenye Umoja wa Mataifa, ambapo Russia ingepiga kura ya veto dhidi ya pendekezo hilo. Alisema endapo nchi nyingi duniani zikikubali kuiwekea vikwazo Iran, basi shinikizo kubwa zaidi litaikabili Iran na kuilazimisha iache mpango wa kusafisha uranium na mpango mwingine nyeti wa nyuklia.

Ufaransa na Ujerumani ni nchi zinazojulikana kama "injini za Ulaya". Mabadiliko ya msimamo wa Ufaransa hakika yataathiri sera ya kidiplomasia ya Umoja wa Ulaya. Mwanadiplomasia mmoja wa umoja huo ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema, "Msimamo wa Ufaransa umebadilika kidhahiri. Zamani Umoja wa Ulaya ulikuwa unashikilia kutafuta ufumbuzi wa suala la nyuklia la Iran ndani ya Umoja wa Mataifa. Lakini hivi sasa watu wanajadiliana wazi pendekezo la kuiwekea vikwazo Iran, ambalo halitawasilishwa kwenye Umoja wa Mataifa."

Hivi sasa kwenye Umoja wa Ulaya, mbali na Uholanzi, pia Uingereza inaunga mkono pendekezo la Ufaransa. Inakadiriwa kuwa Poland na nchi nyingine wanachama kutoka Asia ya Mashariki zinazoiunga mkono Marekani pia zitajiunga na kundi hilo. Lakini Ufaransa, Austria na Italia zinapinga pendekezo hilo, zaidi ya hayo, nchi hizo hazifurahii kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kuhusu kujiandaa vita dhidi ya Iran.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani tarehe 17 alisema, serikali ya Ujerumani inatetea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia, na hivi sasa haitaki kujadili njia nyingine. Siku hiyo hiyo, naibu waziri mkuu wa Italia ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Massimo D'Alema alisema, vita haitaweza kutatua suala la nyuklia la Iran, bali italeta maafa na hatari mpya. Waziri wa mambo ya nje wa Austria pia aliwaambia waandishi wa habari kuwa, suala la nyuklia la Iran halitatuliwa bila kutumia njia ya mazungumzo, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kushikilia kutumia njia hiyo.

Katika suala la vita vya Kosovo mwaka 1999 na vita vya Iraq mwaka 2003, nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa zina maoni tofauti, hali ambayo ilisababisha kupungua kwa nguvu ya umoja huo na hadhi ya kuongoza utatuzi wa masuala hayo kuchukuliwa na Jumuiya ya NATO na Marekani. Hapo baadaye Umoja wa Ulaya ulisisitiza mara kwa mara umuhimu wa mshikamano kati ya nchi wanachama wa umoja huo.

Shirika la nishati ya atomiki la kimataifa litakuwa na mkutano wa kawaida kuanzia tarehe 17 huko Geneva, ambapo kila nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya itatoa maoni yake kwenye mkutano huo, kuhusu suala la nyuklia la Iran, Je nchi hizo zitatoa kauli moja au zitakuwa na maoni tofauti? Hili ni jambo linalofuatiliwa.