Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-19 16:39:17    
Nyumba ya kuwahudumia Wazee Waislamu katika mji wa Huhehaote

cri

Katika mtaa wa makazi ya wazee waislamu mjini Huhehaote,mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ya China,kuna nyumba ya kuwahudumia wazee waislamu,ambayo ni nyumba pekee ya aina hiyo nchini China.Ofisa husika wa nyumba hiyo, Bwana Qiao Zhiming, alisema.

"Nyumba hiyo ilianza kujengwa mwaka 2000 kwa fedha zilizotolewa na serikali na mchango wa makampuni kadhaa"

Bw.Qiao Zhiming alisema nyumba hiyo ina eneo la mita za mraba 4700,ni jengo lenye ghorofa moja na vyumba 56,vyumba hivyo vinaweza kuwapokea wazee 124.Mazingira mazuri na matunzo bora kutoka kwa watumishi yamewawezesha wazee waislamu waishi huko kwa furaha. Bw. Qiao alisema,kutokana na kupewa ruzuku na serikali,wazee waishio katika hiyo hawana haja ya kutoa malipo makubwa. Alisema.

"Nyumba yetu inalenga kuwahudumia wazee wanaohitaji msaada,hivyo tunawatoza pesa kidogo tukilinganisha na nyumba za kawaida za kuwahudumia wazee."

Mwandishi wetu wa habari alitembelea chumba wanachokaa mke na mume,ingawa chumba hicho hakina nafasi kubwa,lakini kinaonekana kisafi sana.Bw. Li Shiliang na mke wake wanaoishi katika chumba hicho ni wachangamfu,walipoulizwa ni kwa nini walichagua kuishi kwenye nyumba hiyo badala ya kuishi pamoja na watoto wao, Bw.Li alisema.

"Tumeishi hapa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja,tunaishi vizuri hapa. Hivi sasa vijana wengi hawawezi kuelewa maana halisi ya kuwapeleka wazee wao katika nyumba ya kuwahudumia wazee.Watoto wote wana shughuli zao wenyewe,hawana muda wa kutushughulikia,mke wangu anaumwa, ni kazi kubwa kwangu mimi kumhudumia mke wangu.

Hivyo tumechagua kuishi katika nyumba hii,hapa tunahudumiwa vizuri,hatuna haja ya kufanya shughuli yoyote ila tu kujiburudisha pamoja na wazee wengine waishio hapa.Naona katika siku zijazo kutakuwa na mwelekeo wa wazee kuishi katika nyumba za kuwahudumia wazee."

Licha ya vyumba vya kukaa,pia nyumba hiyo ina ukumbi wa burudani,chumba cha kusomea na chumba cha kufanya mazoezi ya kujenga afya,wazee wanaweza kucheza mpira wa tenisi wa mezani(Pingpong),kucheza chesi,kusoma magazeti na majarida,na kufanya shughuli nyingine za kujiburudisha.Nyumba hiyo pia ina zahanati ambayo kila siku inawahudumia wazee kwa kupima shinikizo la damu na afya zao.Na vitanda vyote vimewekwa kengele ya kuwaita watumishi wanapohitaji msaada kwa dharura.Nyuma hiyo inajitahidi kuwaandalia wazee vyakula kwa makini, mpishi Ma alisema.

"Vyakula na vitoweo vinavyoandaliwa kwa wazee hao vinafanana na vile vya nyumbani,lakini tuna aina nyingi zaidi kuliko vile vya nyumbani."

Hivi sasa nyumba hiyo ina wazee zaidi ya 60 waislamu,wengi wao ni wakazi wa huko,pia kuna wazee wengine kutoka sehemu nyingine.

Ingawa wazee hao hawako pamoja na watoto wao,lakini wanatunzwa vizuri na wanaishi kwa furaha. Mtumishi Li alisema.

"Tuna uhusiano mzuri na wazee hao.Tunawatendea kama wazazi wetu,na wazee hao wanatutendea kama watoto wao."

Jambo muhimu la kuwashughulikia wazee waislamu ni kuheshimu imani yao ya kidini.Kwa hiyo nyumba hiyo ya kuwahudumia wazee waislamu imeanzisha ukumbi tofauti wa kufanyia swala kwa wanaume na wanawake,chumba cha kutawadha na chumba cha kutazama mwezi.

Wazee hao wanaweza kufanya shughuli zao za kidini wakati wowote.Ukumbi wa kufanyia swala kwa wanawake na wanaume umewekwa katika ghorofa tofauti,kwenye sakafu za ukumbi wa kufanyia swala kuna saa tano za ukutani ambapo mkono wa saa hizo unawekwa katika nyakati tofauti za kufanya swala kwa siku.

Wazee waislamu waishio huko wanapenda kumfahamisha mwandishi wetu wa habari mambo yote yanayotokea katika nyumba hiyo,nyuso zao hazioneshi hali ya upweke na uzee,ila zinaonesha tabasamu na furaha.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-19