Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-19 18:29:17    
China yatoa maelekezo kwa matumizi ya vitafunwa kwa watoto

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii na mabadiliko ya muundo wa chakula, vitafunwa vimejitokeza miongoni mwa chakula cha kila siku kwa watoto. Ili kuelekeza watu wote wafahamu barabara hadhi ya vitafunwa katika chakula cha watoto, idara za huduma za afya za China zimeshirikisha wataalamu husika na kutunga maelekezo ya matumizi ya vitafunwa kwa watoto.

Vitafunwa ni vyakula au vinywaji vidogo vinavyotumiwa katika muda usio nyakati za mlo, na vitafunwa haviepukiki katika chakula cha watoto. Katika miaka kumi iliyopita, kiasi cha jumla cha matumizi ya vitafunwa kwa watoto wa China kimekuwa kinaongezeka, hasa kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004. Kwa mujibu wa uchunguzi maalum uliofanywa mwaka huu na idara ya usalama wa vyakula na virutubisho katika kituo cha udhibiti na kinga dhidi magonjwa cha China, zaidi ya asilimia 60 ya watoto wenye umri kutoka miaka mitatu hadi miaka 17 wanatumia vitafunwa kila siku.

Katika miaka mingi iliyopita, wazazi wengi wa China wanaona kula vitafunwa ni tabia mbaya. Lakini wataalamu wanaona kuwa, watu wa China wana mtizamo usio sahihi kuhusu vitafunwa, matumizi ya vitafunwa pia yana manufaa yake. Dk. Yu Dongmei alisema:

"kutokana na mtazamo wa kisayansi, vitafunwa vinatoa athari mbili kwa watoto. Kwa upande mmoja, vitafunwa kweli si vizuri, kwa kuwa vinaweza kuathiri milo ya kawaida ya watoto, pia vinaweza kusababisha tatizo la utapiamlo au tatizo la kuwa na uzito kupita kiasi. Kwa upande mwingine, vinaweza kupunguza njaa kati ya milo, na kuzuia watoto wasishibe kupita kiasi wakati wa milo."

Wataalamu wanasema, vitafunwa vinaweza kuwa nyongeza kwa milo ya kawaida, pia vinaweza kuongeza virutubisho kiasi fulani kwa watoto, hasa wale wanaokua kwa kasi. Kwa mujibu wa uchunguzi, katika chakula cha watoto wenye umri kati ya miaka mitatu hadi 17, vitafunwa vinatoa asilimia 18.2 ya cellulose, asilimia 17.9 ya Vitamin C, asilimia 9.9 ya calcium na asilimia 9.7 ya Vitamin E.

Kutokana na hali halisi ya matumizi ya vitafunwa kwa watoto wa China, ili kuwafanya watoto watumie vitafunwa kwa njia ya kisayansi na mwafaka na kuhimiza ukuaji wao, wataalamu wa China hatimaye walitunga maelekezo ya matumizi ya vitafunwa kwa watoto baada ya kufanya uchunguzi wa makini na kujifunza kutoka kwa kanuni za matumizi ya vitafunwa zilizowekwa na nchi na sehemu nyingine duniani, zikiwemo Marekani na Hong kong. Maelekezo hayo yamegawanya watoto kwenye makundi matatu, yaani kundi la miaka kati ya mitatu na mitano, miaka sita hadi kumi na mbili na miaka 13 hadi 17, na kutoa maelekezo ya kisayansi yanayoeleweka kwa urahisi, ambayo ni pamoja na maelekezo ya jumla, kwa mfano kuchagua vitafunwa vibichi na vya kimaumbile, maziwa na matunda, pia yanatoa mapendekezo maalum kwa makundi tofauti ya watoto, mtafiti wa taasisi ya virutubisho na usalama wa vyakula katika kituo cha kinga na udhibiti wa magonjwa cha China Bi. Zhai Fengying alisema:

"watoto wenye umri wa miaka kati ya mitatu na mitano, wana uwezo mkubwa wa kuiga, hasa kwa wazazi na walimu, vitendo vya kula chakula kwa watu hao vina athari kubwa kwa watoto hao. Kama wazazi wakisema ladha ya karoti si nzuri, watoto hawawezi kula tena. Kwa hivyo wazazi wanapaswa kufahamu mambo kuhusu vitafunwa, ili kuelekeza watoto watumie vitafunwa vyenye manufaa kwa afya."

Bi. Zhai Fengying alisema, watoto wenye umri wa miaka kati ya sita hadi 12 wanapaswa kuzingatia usafi wa mdomo, na kudhibiti kiasi cha vitafunwa wanavyotumia kila siku, kwa kawaida vitafunwa havipaswi kutumiwa zaidi ya mara tatu kwa siku. Watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wanapaswa kujifunza kuchagua vitafunwa vyenye manufaa kwa afya, na wala hawapaswi kupunguza uzito kwa njia ya kutumia vitafunwa.

Imefahamika kuwa ili kusaidia wazazi na watoto wafahamu vizuri namna ya kuchagua vitafunwa, maelekezo hayo yako pamoja na picha nyingi za vitafunwa vinavyopatikana sokoni. Mtafiti wa taasisi ya virutubisho na usalama wa chakula katika kituo cha kinga na udhibiti wa magonjwa cha China Bw. Zhang Bing alisema:

"picha za vitafunwa zimegawanyika katika makundi 10, sasa tumekusanya picha za vitafunwa vya aina zaidi ya mia nne, pia tunaweka alama maalum kwa virutubisho tofauti."

Kwenye msingi wa mkusanyiko wa picha, maelekezo hayo yamegawanya vitafunwa kwa ngazi tatu, yaani vitafunwa vinavyofaa kutumiwa mara kwa mara, vinavyotumiwa kwa kiasi kinachofaa, na vinavyotumiwa kwa udhibiti. Vitafunwa vya aina vya sukari laini, chocolate, na vyakula viliyoumuliwa, vyote vipo kwenye ngazi ya vyakula vinavyotumiwa kwa udhibiti, maelekezo hayo yanapendekeza wazazi wadhibiti matumizi ya vitafunwa hivyo kwa watoto wao, na ni afadhari vitumiwe kwa mara isiyozidi moja kila wiki. Vipande vya nyama vya ng'ombe, chocolate nyeusi na kahawa ni vitafunwa vinavyopaswa kutumiwa kwa kiasi kinachofaa, in bora vitumiwe kwa mara 1 au 2 kila wiki, mayai, maziwa, na viazi vya kuokwa vinaweza kutumiwa kila siku.

Aidha wataalamu pia wamependekeza makampuni ya kuzalisha vitafunwa yachapishe ngazi za vitafunwa nje ya mifuko ya vitafunwa hivyo, kama ilivyochapishwa "uvutaji sigara unadhuru afya" kwenye mfuniko wa pakiti ya sigara. Kwa njia hiyo, utaratibu wa kuweka ngazi kwa vitafunwa utaweza kuenezwa hatua kwa hatua.